THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF
PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512,
2116898
Fax: 255-22-2113425
|
PRESIDENT’S
OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O.
BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais Kikwete: Malaria inapungua
lakini bado hatari sana
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema
kuwa pamoja na kwamba kiwango na maambukizi ya ugonjwa wa malaria yanapungua
kwa kasi ya kuridhisha katika Tanzania, bado mtoto mmoja anapoteza maisha kwa
ugonjwa wa malaria kila dakika moja katika Afrika.
Aidha,
Rais Kikwete ameishukuru Jumuia ya Kimataifa kwa juhudi kubwa za kupambana na
ugonjwa wa malaria ambazo zimepelekea vifo kutokana na ugonjwa huo kushuka kwa
asilimia 25 duniani na kwa asilimia 33 katika Afrika katika miaka 10 iliyopita.
“Ni
jambo la kutia moyo kuwa dunia imefanikiwa kuzuia vifo vya watu 1.1 na
kuondokana na kesi milioni 274 za malaria katika miaka 10 iliyopita.”
Pamoja
na mafanikio hayo makubwa, bado Rais Kikwete amesema kuwa tishio la malaria
bado ni kubwa ni kweli kwa sababu bado ugonjwa huo unasababisha vifo vya watu
650,000 kila mwaka.
“Changamoto
yetu kubwa ni jinsi gani ya kudumisha mafanikio yaliyopatikana na kubakiza kasi
ya sasa ya kukabiliana na malaria ili tupate mafanikio zaidi. Kwa sababu na kwa
hakika, tishio la malaria bado ni kubwa, ni kweli na liko pale pale kwa sababu
bado ugonjwa huo unasababisha vifo vya watu 650,000 kila mwaka,”
amesema Rais Kikwete.
Rais
alikuwa anazungumza kwenye Mkutano wa kuanzishwa kwa mpangokazi wa jinsi gani
wadau mbali mbali wanaweza kushirikiana kupambana na ugonjwa malaria, mkutano
ambao umefanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.
Rais
Kikwete amewaambia wajumbe wa mkutano huo ulioandaliwa na Mpango wa Maendeleo
wa Umoja wa Mataifa (UNDP) na taasisi
ya kimataifa ya Roll Back Malaria
kuwa yamekuwepo maendeleo mazuri ya kupambana na ugonjwa wa malaria katika
Tanzania na katika Afrika kwa jumla hata kama mapambano bado yanahitajika
kupunguza zaidi athari za ugonjwa huo.
“Katika
Tanzania vile vile tumefanikiwa kupata mafanikio ya kutia moyo ambako
maambukizo ya ugonjwa huo miongoni mwa watoto wadogo chini ya umri wa miaka
mitano yamepungua kwa nusu kutoka asilimia 18 mwaka 2007 hadi kufikia asilimia
tisa mwaka jana, 2012,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Katika
Zanzibar, malaria imepungua mno na sasa tuko katika kipindi cha mpito kuelekea
kwenye kumaliza kabisa tatizo hilo Tanzania Visiwani. Niruhusu nichukue nafasi
hii kuwashukuru wadau wetu wa maendeleo kwa misaada yao iliyotufikisha hapo.
Hata hivyo, nataka nitoa neno la onyo. Hii ni mara ya tatu, tunafanikiwa
kumaliza malaria katika Zanzibar na inaweza kurejea tena. Hivyo, tunatakiwa
kuwa macho kwa kuhakikisha kuwa malaria haisafirishwi kutoka Tanzania Bara
kwenda Zanzibar.”
Rais
Kikwete amesema kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado balaa la malaria linatishia
maisha ya watu bilioni 3.3 duniani na kuwa jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba
watoto ndiyo wanaathirika zaidi. “Kwa hakika, kila dakika mtoto mmoja
anapoteza maisha yake kwa ugonjwa wa malaria katika Afrika, Bara ambalo
linabeba mzigo mkubwa zaidi wa ugonjwa wa malaria. Hali ni mbaya zaidi katika
nchi za Afrika, Kusini mwa jangwa la Sahara, ambako asilimia 90 ya vifo
vinavyotokana na malaria vinatokea.”
Rais
Kikwete yuko katika ziara ya kikazi katika Marekani ambako atahudhuria na
kuhutubia mkutano wa mwaka huu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN).
Rais
Kikwete leo alikuwa miongoni mwa viongozi mbali mbali duniani ambao
wamehudhuria kikao cha ufunguzi cha Baraza hilo ambacho kimehutubiwa miongoni
mwa watu wengine ni Rais wa Brazil Mheshimiwa Dilma Rousseff na Rais Barack
Obama wa Marekani.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
24 Septemba, 2013
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF
PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512,
2116898
Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S
OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O.
BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais Kikwete
awaambia wafadhili: Tupeni fedha za
Malengo ya Milenia
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewataka wabia wa maendeleo wa nchi
masikini kutimiza ahadi zao kama njia ya uhakika kuhakikisha Malengo ya Milenia
yanayolenga kuzitoa nchi masikini kwenye uduni na kuziharakishia maendeleo.
Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa
Tanzania itaweza kutekeleza kwa ukamilifu baadhi ya Malengo lakini itakuwa
vigumu kutelekeza Malengo yote manane kama inavyotakiwa chini ya Makubaliano ya
Utekelezaji wa Malengo ya Milenia hayo ifikapo mwaka 2015.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo,
Jumanne, Septemba 24, 2013 wakati alipozungumza kwenye mkutano uliojadili Jinsi
Gani ya Kuongeza Kasi ya Utekelezaji wa Malengo ya Milenia ulioandaliwa na
Mpango wa Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP)
na Benki ya Dunia (WB) na uliofanyika
kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.
Pamoja na Rais Kikwete kuzungumzia
maendeleo ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia katika nchi mbali mbali walikuwa
na Mtawala wa UNDP Mheshimiwa Hellen
Clark, Rais wa Benki ya Dunia Mheshimiwa Jim Kim, Waziri Mkuu wa Bangladesh
Mheshimiwa Sheikh Hasina, Rais wa Ghana Mheshimiwa John Mahama, Rais wa Costa
Rica Mheshimiwa Laura Chinchilla Miranda na Waziri Mkuu wa Tonga Mheshimiwa
Lord Siale’ataongo Tu’ivakano.
Katika kikao ambacho kila mmoja wa
viongozi hao alitoa uzoefu na changamoto za nchi yake katika kutekeleza Malengo
hayo, Rais Kikwete amewaambia wafadhili kuwa wakati nchi zinaendelea na
utekelezaji wa Malengo hayo, ni wajibu wa wafadhili pia kutimiza wajibu wao wa
Lengo la Nane la Milenia ambalo linawabebesha wajibu wafadhili kugharimia
utekelezaji wa Malengo hayo.
Rais Kikwete amesema kuwa kukawia kwa
wafadhili hao kutoa fedha za utekelezaji wa Malengo, zimechangia kwa kiasi fulani
kwa utekelezaji huo kutokuwa na kasi iliyotarajiwa kutokea mwanzo.
Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa
pamoja na kucheleweshwa kwa fedha za kutosha za utekelezaji, Tanzania itaweza kwa
kiasi fulani kufanikisha utekelezaji wa baadhi ya Malengo, lakini ni dhahiri
kuwa Malengo mengine hayataweza kufikiwa ifikapo mwaka 2015 ambao ndiyo mwaka
wa mwisho wa utekelezaji wa Malengo hayo.
“Tunafanya juhudi kubwa na ni dhahiri
kuwa kasi ya jitihada hizo itaongezeka katika miaka miwili iliyobakia. Kwa
jumla ripoti ya utekelezaji wa Malengo hayo katika Tanzania inaonyesha kuwa ni
dhahiri haitawezekana kutekeleza Malengo matatu ambayo ni Lengo la Kwanza la
Kufuta Umasikini wa Kutupwa na Njaa, Lengo la Tano la Kuinua Kiwango cha Afya
na Kupunguza Vifo vya Akinamama, na Lengo la Saba la Kuhakikisha Tanzania Inakuwa
na Mazingira Endelevu,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Malengo ambayo Tanzania itayafikia
bila matatizo ni pamoja na Lengo la Pili la Kuhakikisha kuwa Watoto Wote Wenye
Umri wa Kwenda Shule Wanakwenda Shule, Lengo la Nne la Kupunguza Vifo vya Watoto,
Lengo la Sita la Kupunguza Ukali wa Magonjwa ya Malaria na Ukimwi na Sehemu ya
Lengo la Saba Kuhusu Uongezaji wa Idadi
ya Watu Wanaopata Maji safi na Salama ya Kunywa.”
“Tunaweza pia kufikia Lengo la Tatu la
Kufanikisha Usawa wa Kijinsia na Kuwawezesha Akinamama hasa katika kuhakikisha
kuwa idadi sawa ya watoto wa kike na kiume wanakwenda shule za msingi,
sekondari na vyuo vikuu na kuwa na idadi sawa ya wanawake na wanaume katika
Bunge,”
amesema Rais Kikwete.
Malengo ya Milenia yamekuwa
yanatekelezwa tokea mwaka 2001 na yalenga kuzitoa nchi masikini katika
umasikini na uduni na kuzifungulia njia ya maendeleo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
24 Septemba, 2013
THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF
PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512,
2116898
Fax: 255-22-2113425
|
|
PRESIDENT’S
OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O.
BOX 9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
Kikwete akutana na Melinda Gates
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumanne, Septemba 24, 2013, amekutana na
kufanya mazungumzo na Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Melinda – Gates
Foundation, Bi. Melinda Gates.
Rais Kikwete na Bi. Melinda Gates
wamekutana kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, ambako wote wawili
wamehudhuria mikutano ya kimataifa inayoendelea kwenye makao makuu hayo.
Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete na
Bi. Melinda Gates wamezungumzia miradi mbali mbali ambayo taasisi hiyo inaunga
mkono na kugharimia katika Tanzania katika maeneo ya afya ya jinsi ya kupunguza
na kumaliza vifo vya akinamama na vifo vya watoto wadogo pamoja na shughuli za
kilimo.
Katika mazungumzo hayo, Bi. Melinda Gates amempongeza Rais Kikwete kwa
uongozi wake katika maeneo hayo na pia ameipongeza Tanzania kwa mafanikio
makubwa katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG’s) hasa katika maeneo ya elimu na
chanjo kwa watoto.
“Mheshimiwa Rais, nyie katika
Tanzania mmepata mafanikio ya ajabu kabisa katika suala la elimu na katika
utoaji wa chanjo kwa watoto wadogo kupambana na magonjwa mawili makubwa
yanayoua watoto wadogo, yaani magonjwa ya kuharisha na homa ya mapafu.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
24 Septemba, 2013
No comments:
Post a Comment