Ukitaka kuunganishiwa umeme nchini Tanzania ni lazima uache kazi ufanye kazi ya kuunganishiwa huduma hiyo. Hii inatokana na ukweli kwamba kama unataka umeme, huna budi kuacha unachofanya na kutumia muda mwingi kukamilisha huduma hiyo tena kwa gharama kubwa.
Watu wengi wanashauri ni vyema kama unataka huduma ya umeme ukajiandaa kisaikolojia kwa kuwa itakulazimu kutumia fedha nyingi na muda mwingi kupata huduma hiyo.
Kutokana na mazingira hayo, uanzishaji wa biashara kubwa na hata zile ndogo zinazohitaji nishati, wahusika wanalazimika kusubiri huduma ya umeme.
Siku 109 kupata umeme
Kwa mujibu wa ripoti iliyomo katika taarifa ya kufanya biashara ya Benki ya Dunia ya ‘The World Bank’s Doing Business’ ya mwaka huu ambayo iliangalia nchi 185 duniani, ilibaini kwamba inachukua siku 109 na gharama ya asilimia 1,944.1 ya pato la mtu kwa mwaka nchini Tanzania kukamilisha mchakato wa kuunganishiwa umeme.
Pia taarifa hiyo ilibainisha kwamba kuna mambo manne ambayo lazima yafuatwe ili mfanyabiashara kupata ghala lililounganishwa na umeme kwenye maeneo ya kibiashara ndani ya jiji.
Mambo hayo manne yanayopaswa kufuatwa ni; kupeleka maombi kwa kampuni ya ugavi wa umeme ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na inakuchukua siku 11 kupata majibu ya maombi yako.
Fundi umeme aliyesajiliwa anapaswa kuwasilisha hati inayoonesha kazi ya kuweka nyaya za umeme katika eneo husika, imefanyika kwa mujibu wa kanuni na kwa viwango vinavyotakiwa.
Baada ya hapo mteja ananunua transfoma ili kufanya shughuli za maunganisho nje na kazi hiyo inachukua miezi mitatu. Jumla ya gharama zinazotumika hapa ni Sh16 milioni.
Pia kuna fedha zitakazotumika kwa ajili ya kulipia gharama za maunganisho na za dhamana na wakati mwingine mteja analazimika kununua baadhi ya vifaa muhimu vya kuwezesha maunganisho nje.
Muda mrefu unaotumika na vikwazo vinavyojitokeza katika mchakato wa kuingiza umeme katika ghala au sehemu ya biashara imesababisha Tanzania kuwekwa katika nafasi mbaya ya 96 kati ya nchi 185 duniani endapo mtu anahitaji huduma ya kuunganishiwa umeme.
Nafasi ya hiyo kwa Tanzania inatisha kwa kuwa inaonyesha ni jinsi gani wawekezaji wanatumia muda mwingi kutafuta kuunganishiwa umeme huku wengine wakilazimika kutumia majenereta wakati wakisubiri umeme na kuongeza gharama za uzalishaji.
“Baadhi ya viwanda vya saruji jijini Dar es salaam havijaanza kufanyakazi kwa sababu havijaunganishiwa umeme,” anasema Mkurugenzi wa sera na utetezi wa Shirikisho la Viwanda nchini (CTI), Hussein Kamote.
Mkurugenzi huyo anaitaka Tanesco kuondokana na vikwazo vinavyochelewesha maunganisho ya umeme ili kuvutia wawekezaji nchini.
“Hatujafanya utafiti kuhusu upatikanaji wa umeme nchini, lakini tunaamini kwamba ni eneo linalotakiwa kuangaliwa kwa makini,”anasema Kamote.
Kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia, mchakato wa kuunganisha umeme nchini unakuwa mgumu kutokana na sheria na kanuni kadhaa zinazotakiwa kufuatwa kugusa; ubora, usalama, masuala ya kiufundi, ununuzi ni suala la utandazaji wa nyanya ndani ya ghala.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirikisho la wenye Viwanda nchini (CTI ) kwa ufadhili wa Best Ac, mwaka 2011 umeonyesha kwamba kuna matatizo mengi yanayokumba sekta ya nishati nchini Tanzania.
Kwa kukabiliana na tatizo hilo utafiti huo ulishauri Tanesco kugawanya kampuni na kuwa mbili. Kampuni moja kwa ajili ya kufua umeme na kampuni ya pili kwa ajili ua kusambaza umeme.
Kwa mujibu wa utafiti huo, kampuni mbili zitasaidia wateja wa umeme kupata unafuu wa kupata huduma kwa mfano, kuunganishiwa umeme na kulipia huduma ya akra za umeme.
Vilevile kuwapo kwa kampuni mbili, kutachangia kuwa na kasi katika maunganisho ya umeme na kuboresha ukuaji wa kampuni ya Tanesco hasa kutanua wigo wake.
Uwezo huo wa kutanua wigo umedhihirishwa pia katika utafiti uliofanywa wa ‘Provision of Financial Advisory and Modelling Services to Tanesco: Cost of Service’ uliofanywa mwaka 2010, ambao ulibainisha kuwa Tanzania ina kiwango kidogo cha kasi ya uunganishaji umeme na kwa mwaka 2008 ilikuwa ni asilimia 14 wakati idadi ya watu ikiwa ni 42milioni.
Uwapo wa watu wengi kiasi hicho unaweza kuwa nafasi nzuri ya kutanua soko la Tanesco na wanaweza kuingiza wateja wapya 100,000 kila mwaka na kutoa nafasi zaidi ya ukuaji. Hali hiyo haijafikiwa mpakasa sasa.
Kwenye mkutano wa mashirika ya nishati , uliofanyika Februari hadi Machi mwaka huu mjini Washington DC, Marekani ilibainisha kwamba Tanesco ina uwezo wa kuunganisha wateja wapya 90,000.
Januari mwaka huu serikali ilifanya mabadiliko katika gharama hizo na kwa watu walio umbali wa mita 30 kutoka katika laini ya umeme na kuhitaji nguzo moja gharama yake ilipungua kwa asilimia 60 mpaka asilimia 75.
Gharama zimepungua
Kwa wakazi wa mjini gharama za maunganisho zilipungua kwa asilimia 29 mpaka asilimia 60 na kwa Mkoa wa Lindi na Mtwara, wakazi wa huko watatozwa dola 62 za Marekani kwa umeme wa majumbani na viwandani.
Tanesco katika mpango kazi wake ilifanya uamuzi wa kufanya maunganisho 250,000 kwa mwaka kutoka katika gridi ya taifa na kuongeza idadi ya watu wanaopata umeme kutoka asilimia 14 hadi 30 ifikapo mwaka 2015.
Ingawa kuna shida hiyo ya umeme taarifa ya mwaka huu ya Doing Business, Tanzania ilifanya vyema zaidi kuliko Kenya iliyoshika nafasi ya 162, Uganda nafasi ya 127, Msumbiji nafasi ya 174 na Malawi iliyokuwa ya 176. Hata hivyo Tanzania ilifanya vibaya katika baadhi ya maeneo.
Tujadiliane kupitia Ujumbe mfupi SMS kwa 15774 ukianza na neno BIZ na kufuatia ujumbe wako. Ujumbe wako mfupi ni bure, hautozwi.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment