Nairobi. Hatua ya Kundi la Al-Shabaab la Somalia kudai kwamba watu 137 lililokuwa limewateka waliuawa kwa silaha za sumu juzi, imezidisha utata wa idadi ya vifo vilivyotokea baada ya shambulizi la kigaidi lililofanyika Westgate, Nairobi, Jumamosi iliyopita.
Taarifa iliyotolewa na kundi hilo kupitia kwenye mtandao wa Twitter jana, ilidai kuwa mateka 137 waliokuwa wanashikiliwa na wafuasi wao kwenye jengo la biashara la ghorofa nne, walifariki baada ya kupuliziwa sumu na vikosi vya usalama vya Serikali ya Kenya.
Hata hivyo, Msemaji wa Serikali ya Kenya, Manoah Esipisu alikanusha vikali madai ya kundi hilo.
Ghorofa tatu kati ya nne za jengo hilo zilianguka jana lakini kumekuwa na utata wa idadi ya waliokuwamo ndani.
Esipisu alisisitiza kuwa kuta za jengo hilo zilianguka baada ya magaidi hao wa Al-Shabaab kuchoma moto bidhaa za maduka hayo. “Hawa jamaa walikusanya vitu vingi kwenye ghorofa ya tatu na kuvichoma moto. Wingi wa vitu ulisababisha kuta na sakafu za ghorofa zile kuzidiwa uzito.
“Kuta za ghorofa ya tatu zikaangukia ghorofa ya pili. Kuta za ghorofa ya pili zikaangukia ile ya tatu ndiyo sababu kuu ya hali hiyo... Al-Shabaab wanajulikana kwa propaganda zao, hakuna ukweli wowote kuhusu habari hizo,” alisema Esipisu.
Kundi hilo la Al-Shabaab lilidai kupitia mtandao wa Twitter kuwa Serikali ilipuliza sumu kabla ya kuanza kubomoa jengo hilo.
Utata wa idadi ya waliokufa
Wakati Kundi la Al-Shabaab likidai kuwa watu 137 wamekufa jana, Serikali ya Kenya imeeleza kuwa watu waliokufa ni 67 tangu shambulizi hilo lilipotokea Jumamosi iliyopita.
Idadi kubwa ya waliofariki ni raia wa Kenya na wageni 18 kutoka Ufaransa, Canada, Uholanzi, Australia, Peru, India, Ghana, Afrika Kusini na China. Raia watano wa Marekani nao wamethibitika kufariki dunia.
Kwa mujibu wa taarifa ya Serikali, watu 175 walijeruhiwa katika shambulizi hilo huku watu 60 wakiwa wamelazwa hospitalini.
Pamoja na watu hao, pia kuna magaidi watano waliouawa wakati wa operesheni hiyo.
Askari wanaendelea na operesheni ya kupekua eneo hilo ili kuona kama kuna uwezekano wa magaidi wengine kujificha.
Marekani, Israel na Uingereza zaongeza nguvu
Marekani, Uingereza na Israel zimeongeza mashushushu ili kusaidia uchunguzi wa tukio hilo.
Hiyo ni baada ya nchi hizo kuongeza maofisa wake wa usalama ambao walishirikiana na vikosi vya usalama vya Kenya tangu, Jumapili iliyopita.
Kazi ya kuondoa miili
Esipisu alisema pia kuwa vikosi vya usalama vinajiandaa kuanza kazi ya kuondoa miili ya watu waliofariki dunia kwenye jumba hilo.
“Kazi hii itaanza pale vikosi vyetu vitakapojiridhisha kuwa kuna hali ya usalama,” alisema Esipisu.
Kuna wasiwasi kuwa bado kuna magadi waliojificha kwenye jumba hilo lililokuwa na maduka ya kampuni mbalimbali, migahawa kadhaa, benki na jumba la michezo ya casino.
Mwananchi
2 comments:
siasa mchezo mbaya weee yani usisikiye ukichunguza kwa undani utajua kwa nini wamewaripua wakenya na wanasingiziwa magaidi yaniii dunii hiii wee acha tuu mwenye akili ataona mbali aliye kuwa na akili za kushikiwa ndo ataona haya
siasa mchezo mbaya weee yani usisikiye ukichunguza kwa undani utajua kwa nini wamewaripua wakenya na wanasingiziwa magaidi yaniii dunii hiii wee acha tuu mwenye akili ataona mbali aliye kuwa na akili za kushikiwa ndo ataona haya
Post a Comment