Klabu moja ya Qatar inataka kumsajili Mrisho Ngassa kwa mkataba wa miaka miwili.
Dar es Salaam. Mabingwa wa soka wa Tanzania Bara, Yanga wanaweza kumkosa mshambuliaji wao mahiri Mrisho Ngassa baada ya klabu moja ya Qatar kuonyesha nia ya kumsajili huku mchezaji huyo akikiri kwamba dau walilomuahidi linamshawishi.
Habari za uhakika ambazo Mwananchi ilizipata jana zilisema kuwa, tayari Ngassa amekwishafanya mazungumzo na klabu hiyo ambayo ipo tayari kuilipa Simba SC milioni 45 anazodaiwa na kuifidia Yanga kwa kumuuza mchezaji huyo.
Taarifa hizo zimesema kuwa klabu hiyo inataka kumtumia Ngassa baada ya usajili wa dirisha dogo.Ngassa alithibitisha hilo huku akikataa kutaja jina la timu hiyo kwa sababu za kisheria za usajili wa wachezaji na kuogopa adhabu ya Shirikisho la Soka Kimataifa (Fifa).
Mchezaji huyo alikiri kuwa timu hiyo ipo tayari kumpa mkataba wa miaka miwili na kuzilipa Simba SC na timu yake ya sasa, Yanga.
Alisema kuwa hatua hiyo imekuja baada ya kuona suala lake la kuitumikia Yanga katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara linashika sura mpya kutokana na mvutano wa malipo.
Alifafanua kuwa klabu hiyo imemuahidi donge nono na kuamua kufuta msimamo wake wa zamani wa kutaka kucheza soka hapa nchini kutokana na maslahi anayopata.
“Maslahi yao mazuri na mazingira waliyoniahidi kimkataba, nimevutiwa nao kutokana na ukweli kuwa suala langu la kuichezea Yanga limekumbwa na vipingamizi vingi,” alisema Ngassa.
Alisema kuwa baadhi ya wadau wa Yanga na marafiki zake wana nia njema ya kutaka kumlipia fedha anazodaiwa na Simba, lakini uongozi wa Yanga bado haujatoa jibu la sakata hilo.
“Nimemaliza kifungo cha mechi sita, sasa suala lililobaki ni malipo, viongozi hawajatoa jibu mpaka sasa, ” alisema Ngassa.
Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Clement Sanga alikiri kuwa bado hawajailipa Simba fedha wanazomdai Ngassa kutokana na majadiliano waliyokuwa nayo.
Sanga alisema kuwa wana uhakika kuwa Ngassa ambaye anafanya mazoezi ya nguvu na Yanga, atacheza Jumamosi dhidi ya timu ngumu ya Ruvu Shooting.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment