Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akiwahutubia wanachama wa chama hicho kwenye moja ya mikutano, Kilosa mjini mkoani Morogoro. Picha ya Maktaba
Dodoma. Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete amesema kama rushwa haitakomeshwa ndani ya chama hicho, katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2015 kitaanguka vibaya na iwapo kitanusurika hakitapita kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete amempa jukumu la kushughulikia viongozi wa CCM wanaokula rushwa, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philipo Mangula.
Rais Kikwete, alitoa onyo hilo juzi usiku, alipokuwa akifunga mafunzo maalumu ya siku nne kwa makatibu wa mikoa, makatibu na wenyeviti wa wilaya wa chama hicho nchini.
“Kama hatutabadilika katika suala la rushwa mwaka 2015 tutakuwa na wakati mgumu sana na kama mwaka huo tutafanikiwa kuishika Serikali, basi mwaka 2020 hatutarudi tena madarakani.
“Najua rushwa ipo na mnaendelea kupokea shilingi laki mbili za airtime (muda wa mawasiliano), ndugu zangu hatutafika ama wengine watavuka na wengine kukwama,” alisema Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete.
Hii ni kauli ya kwanza nzito ya Rais Kikwete ya hivi karibuni ya kukionya chama hicho kuhusu uimara wake wa kuendelea kushika dola.
Aliendelea kusema kuwa tatizo la rushwa kwa viongozi wa chama hicho linazidi kuwa kubwa kila siku, hali ambayo inawapotezea imani wananchi ambao ndio wapiga kura wao.
“Viongozi wa chama ndio mmekuwa mawakala wa kusambaza rushwa bila hata aibu. Nawaombeni tubadilike, kama tutaendelea hivi hali yetu itakuwa ngumu sana katika chaguzi mbalimbali, nawaambieni,” alisema Rais Kikwete ambaye alitumia muda wa saa mbili kufunga mafunzo hayo.
Aliwaambia kuwa siku hizi watu wana mbadala wa vyama vingine na siyo CCM peke yao.
Aidha, Rais Kikwete alisema viongozi ambao wanajihusisha na vitendo vya rushwa waondolewe mara moja katika nafasi zao, ili kuwaweka watu watakaokisaidia chama kupata mafanikio.
“Tuna vijana wengi kutoka katika vyuo mbalimbali ambao wanaweza kufanya kazi kwa uadilifu wa hali ya juu, hivyo hatuna budi kuachana na hawa wala rushwa ambao watatupotezea sifa yetu kwa wananchi.
“Tukipoteza urais ndiyo tumekwisha na chama kinaweza kufa.”
Aidha, aliwaonya viongozi ambao wanajihusisha na uuzaji wa mali za chama kama vile viwanja na baadhi yao kuingia mikataba yenye utata.
“Kuna watu wanapoingia mikataba sijui wanakuwa wamelewa...kwanza unashindwa hata kuelewa...kwa mfano utakuta mtu alipangishwa jengo la CCM kwa miaka 264 sasa unawaza huu mkataba wa aina gani kwa sisi tuliopo hapa, miaka 50 ijayo hakuna atakayekuwapo duniani, sasa mmiliki wa lile jengo atakuwa nani?” alisema.
Hata hivyo, aliwataka makatibu hao na wenyeviti wa wilaya na mikoa kuhakikisha wanawatembelea wanachama wao na kutafuta wanachama wapya kwa ajili ya kujiimarisha kwa chaguzi mbalimbali zijazo.
“Viongozi wengi hatuna tabia ya kuwatembelea wanachama wetu na kuwatatulia kero zao, hali ambayo inatugharimu wakati wa uchaguzi kupata kura kidogo tofauti na idadi ya wanachama tulionao,” alisema na kuongeza:
“Wenzenu wakiendelea kutembelea wanachama na kuitisha mikutano, nyie mnabakia kuimba wembe ni uleule ushindi, shauri yenu mtakatwa,” alisema.
Alisema wapinzani wana rekodi ya kufanya vizuri kwa kufanya mikutano kuliko viongozi wa CCM.
Aidha, alisema iwapo hawatafanya kazi vizuri chama hakitaweza kufanikiwa na kuwataka kutumia maarifa waliyopata katika mafunzo hayo kuhakikisha chama kinakuwa imara na chenye uwezo wa kuongoza. “Lazima muendelee kuongeza wanachama siyo kupanda majukwaani na kuimba iyena iyena...Utendaji mpya wa kuongeza wanachama ni kuwatambua na kuwapa majukumu,” alisema.
Alisema chama hicho kina udhaifu wa kuwashawishi watu kujiandikisha katika daftari la kudumu na kwenda kupiga kura.
“Kama ni udhaifu katika chama chetu ni huu kwani tuna wanachama, lakini wakati wa kwenda kupiga kura hatuwafuatilii ni vyema suala hili nyie viongozi muanze nalo sasa.”
Peter Kisumu
Hivi karibuni mwanasiasa na kada mkongwe wa CCM, Peter Kisumo naye alionya kuwa chama hicho kinaweza kuondolewa madarakani kutokana na kunyamazia vitendo vya ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za umma vinavyotokea nchini.
Mzee Kisumo alitoa onyo hilo wiki iliyopita katika mazungumzo maalumu aliyofanya na gazeti hili nyumbani kwake Dar es Salaam kuhusu kumbukumbu ya Miaka 14 ya Kifo cha Mwalimu Julius Nyerere.
Alisema tatizo kubwa la chama hicho ni kwamba kimeendelea kuwa chama dola kikikaa mbali na wananchi, huku kikishindwa kuidhibiti rushwa na kuwawajibisha wahusika wa vitendo hivyo.
“Chama kimebaki kuwa cha walalamikaji, kila mtu amekuwa mlalamikaji. Hata Waziri Mkuu amegeuka mlalamikaji. Sijaona watu wanaowajibishwa kwa ufisadi,” alisema Kisumo na kuongeza:
“CCM haiwezi kujivunia ufisadi unaoonekana nchini. Siwezi kusema imeukumbatia, lakini nasema imekuwa CCM bubu, hata kuukemea ufisadi haiwezi. Utamaduni huu enzi za Mwalimu Nyerere haukuwapo.”
Alisema kutokana na udhaifu huo wa CCM, kuna uwezekano mkubwa wa chama cha upinzani, na hasa Chadema kutumia mwanya huo kuwashawishi wananchi na kushinda uchaguzi.
Kisumo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa CCM, alisema ingawa Chadema haijaonyesha wazi mambo kinayoyapigania, kinaweza kutumia agenda ya ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali za umma kuwavutia wananchi na kuchaguliwa.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake