Thursday, October 31, 2013

Mabadiliko yaanza kuonekana bandarini

Ripoti ya Benki Kuu ya Dunia (WB) ya mwaka 2013, imebainisha kwamba kukosekana kwa mwingiliano sahihi wa kiutendaji kwenye taasisi za umma kunakwamisha kwa kiwango kikubwa utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam.
Benki ya Dunia kupitia ripoti yake, inashauri mamlaka husika kufanya maboresho makubwa ya ukusanyaji wa mapato ili kugharimia programu za uwekezaji zenye mambo mengi ndani ya kipindi cha mwaka 2014 na 2015.
Wakati benki hiyo ikishauri hayo Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, anaitupia lawama Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) kwa kutotoa huduma katika siku saba za juma. Anasema hali hiyo inarudisha nyuma ufanisi wa bandari hiyo.
“Kinachohitajika ni TRA wanapaswa kushirikiana na taasisi za kibenki ili watoe huduma za kibenki kila siku na ikiwezekana saa 24 ili kwenda sambamba na bandari ambao wanafanya kazi saa 24, lengo ni kutochelewesha meli zinazoleta mizigo bandarini hapo,” anasema.
Dk Mwakyembe anasema kila taasisi inapaswa kutekeleza wajibu wake ipasavyo ili kuinua pato la taifa na kwenda sambamba na Mpango wa Matokeo Makubwa wa (BRN).
“Watendaji wa bandari wanafanya kazi saa 24 kila siku za juma bila kupumzika, lakini TRA wao wanalala siku za sikukuu na za mwisho mwa juma, jambo hili hatutakubali liendelee,” anasema Dk Mwakyembe.
Waziri huyo anakwenda mbali zaidi na kuzitaka Bandari za Nchi Kavu (ICDs) kutoa huduma hizo kila siku ili kuepusha usumbufu kwa mteja kuingia gharama atakazotakiwa kulipa kwa muda wakati mzigo wake utakapokuwapo sehemu hiyo.
Ufanisi wa TPA
Kaimu Meneja wa Tanzania Port Authority (TPA), Awadhi Massawe anasema katika kipindi cha mwaka 2012/2013 bandari ilihudumia tani milioni 12.5 za mizigo, ukilinganisha na tani milioni 10.9 zilizohudumiwa mwaka 2011/12 ikiwa ni zaidi kwa asilimia 15.0.
Shehena ya kichele (nafaka) iliongezeka kwa asilimia 37.4, nafaka mchanganyiko asilimia 7.8 na mafuta iliongezeka kwa asilimia 19.0 huku shehena yote kwa ujumla ikiongezeka kwa asilimia 12.6 kwa mwaka.
Anasema mgomo wa malori uliathiri upakuaji wa mizigo bandarini kwa sababu asilimia 99 ya mizigo inayopakuliwa bandarini inatumia usafiri wa barabara.
“Idadi ya siku kwa meli kusubiri kupakuliwa mizigo bandarini imepungua kutoka siku 6.1 mwaka 2011/12 hadi siku 4.9 mwaka 2012/13 huku idadi ya siku meli kusubiri nje kuingia kwenye geti imepungua kutoka siku 3.2 mwaka 2011/12 hadi kufikia siku 1.7 mwaka 2012/13.
“Idadi ya siku ya kupakua kontena bandarini ilifikia siku 10.3 kwa kontena moja mwaka 2011/12 na mwaka 2012/13 idadi hiyo ilipungua na kufikia siku 9.8, sawa na upungufu wa asilimia 4.9 kwa mwaka na kwa upande wa kontena za nje, siku zilipungua kutoka 16.1 hadi siku 15.4 kwa kontena,” ,” anasema Massawe.
Massawe akizungumzia changamoto zinazoikabili bandari hiyo anabainisha kuwa ni ufinyu wa maeneo ya kuhudumia meli na shehena pamoja na ukata wa fedha kwa ajili ya kuboresha na kupanua huduma.
“Kina kifupi cha maji na ufinyu wa lango la kuingilia meli, mabadiliko ya teknolojia ya meli na huduma hafifu ya reli ni baadhi ya mambo ambayo yanatukwamisha,”anasema Massawe.
Mpango wa BRN
Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Omari Issa anasema watawasiliana na wahusika kuona ni jinsi gani Serikali itasaidia kuondoa kasoro zilizopo na kuwezesha bandari kutoa huduma zake kwa ufanisi.
“Bandari yetu ni rasilimali kubwa kuliko hata gesi au madini kwani gesi inakwisha, lakini bandari itaendelea kuwapo hivyo ni lazima kuiboresha,” anasema Issa.
Issa anasema, mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanatakiwa kuendana na utoaji wa huduma hizo kwa njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ili kuboresha ufanisi wa utendaji kazi badarini hapo.
“Huduma zinatakiwa kutolewa siku yoyote na mahali popote haijalishi mtu yuko ndani au nje ya nchi, matumizi ya teknolojia ni ya lazima, kwani teknolojia ikitumika hukutakuwa na usumbufu kama huu uliopo,” anasema Issa.
Mwananchi

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake