Karim Wade
Ahmed RajabToleo la 321
16 Oct 2013
NCHINI Senegal kuna kitu kinachoitwa Cour de répression de l’enrichissement illicite(CREI) yaani Mahakama Dhidi ya Wanaojitajirisha kwa njia za haramu, kwa ufupi Mahakama ya Kupinga Ufisadi. Hivi sasa Mahakama hayo yanaisikiliza kesi dhidi ya Karim Abdoulaye Wade, mtoto wa Rais wa zamani Abdoulaye Wade.
Hivi ninavyoandika Karim yuko kwenye gereza la Rebeuss mjini Dakar. Alitumbukizwa humo Aprili 17 baada ya polisi kupiga hodi nyumbani kwake na kumkamata.
Gereza la Rebeuss si pahala pa mchezo. Humuombei adui yako atiwe humo seuze aliye wako. Karim, mwenye umri wa miaka 44 na aliyekuwa waziri babake alipokuwa Rais (2000-2012), anakabiliwa na kesi ya wizi. Anashtakiwa kuiba takriban dola za Marekani bilioni moja na nusu alizozichota alipokuwa akisimamia miradi mikubwa mikubwa ya miundombinu na ya nishati.
Kuna wasemao kwamba serikali ya sasa ya Senegal inayoongozwa na Rais Macky Sall, inamuonea tu Karim kwa vile yeye ni mtoto wa babake na kwamba dhamiri hasa ya serikali ni kulipiza kisasi.
Ufisadi una sura nyingi: kuwapatia kazi jamaa zako; kuwapatia kandarasi rafiki zako; kuwalisha fedha wote wale wataokusaidia upate nyadhifa za kisiasa, mfano ubunge.
Kama haujadhibitiwa ufisadi unaweza ukalifilisi taifa. Tumeona mwaka jana jinsi kisiwa cha Sicily, kilicho Ulaya ya Kusini, kilivyokuwa nusura kifilisike. Na si Sicily pekee lakini nchi kadhaa za Ulaya ya Kusini nazo pia nusura zifilisike.
Katika Afrika ya Magharibi si Senegal peke yake iliyochukua hatua ya kuwafikisha mahakamani mawaziri na vigogo wengine waliofumwa wakijitajirisha kwa njia za kifisadi.
Nina orodha, kwa mfano, ya mawaziri wa zamani 19 wa Cameroon, wakiwa pamoja na waziri mkuu wa zamani Inoni Eprhaim, wanaoionja jela baada ya kupatikana na hatia za ufisadi. Baadhi yao wamepewa vifungo vya maisha; wengine vifungo vya muda mrefu vya miaka isiopungua 15.
Kuna wenye kusema kwamba hata huko Cameroon mawaziri na wakubwa wengine walionaswa kwa ufisadi wamechukuliwa hatua kwa sababu waliwakwaa wenzao serikalini.
Juu ya hatua hizo kali ufisadi bado ungali unaendelea nchini Cameroon. Hata hivyo hatua hizo ni onyo kwa wananchi wengi wa Cameroon. Na ingawa serikali ya huko inapaswa kupongezwa kwa hatua hizo bado ina mengi ya kufanya ili iweze kurejeshewa pesa zilizoibiwa zipate kutumika katika miradi ya maendeleo.
Haja ya kutunga sheria za kupinga ufisadi imezusha mijadala yenye kubabaisha katika nchi nyingi za Kiafrika kwa vile wanaotakiwa kutunga sheria hizo wamekuwa wakizingatia zaidi maslahi yao ya kibinafsi. Wakubwa hao wamekuwa wakitumia masuala tata ya kisheria kuzidi kuwababaisha watu na kuonyesha, kwa mfano, kama kuna ugumu wa kutunga sheria kama hizo.
Lakini zipo nchi zinazojitahidi kupambana na ufisadi. Mfano mmoja ni Msumbiji inayojitahidi kutunga sheria zitazouzuia ufisadi usifurutu ada na zitazovifanya vyombo vya serikali na wakuu wa serikali wawe na uwazi zaidi kwani uwazi ni moja ya mambo yanayosaidia kuuzuia ufisadi.
Asasi za kiraia na wafadhili wote hao nao wamechangia kuishinikiza serikali ya Msumbiji ichukue hatua ya kupambana na ufisadi kwa kutunga sheria za kuuzuia, ikiwa ni pamoja kutunga mwongozo wa maadili wa kufuatwa na watumishi wa serikali.
Hivyo, ni wazi kwamba kuna haja Msumbiji ya kuuimarisha mfumo wake wa kisheria ili uweze kupambana na mafisadi wanaohatarisha usalama wa taifa hilo.
Mfano mwingine wa nchi zinazochukua hatua za kupambana na ufisadi ni Rwanda. Huko tumewashuhudia watu wa nyendo mbalimbali za maisha — wakulima, askari, madereva na watumishi wa serikali —wakifikishwa mbele ya mahakama ya kawaida na kushtakiwa kwa ufisadi.
Wakipatikana na hatia na kupewa adhabu majina yao huchapishwa kwenye magazeti ili wakashifike.
Ubaya wa mambo ni kwamba aghalabu majina tunayoyaona ya wanaokashifiwa kwa ufisadi ni yale ya vijifisadi vidogo. Vijisamaki si mijipapa ya ufisadi. Majina ya mifisadi hatuyaoni.
Hata hivyo, Rwanda hii leo ni nchi yenye kiwango cha chini cha ufisadi ikilinganishwa na nchi nyingine zilizo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mahakama Maalumu ya kusikiliza kesi za ufisadi yamebuniwa katika nchi kadhaa zikiwa pamoja na Kenya, Uganda, Pakistan, Philippines na Indonesia, ambako hivi majuzi tu Oktoba 3, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Kikatiba, Akil Mochtar, alikamatwa na Tume ya Kuufyeka Ufisadi, aina ya Mahakama Dhidi ya Ufisadi, na akashtakiwa kwa kosa la kupokea hongo.
Polisi wanasema wana ushahidi kwani walipoingia nyumbani kwake kumkamata walikuta fedha taslimu zenye thamani ya dola za Marekani 260,000.
Jumuiya za kimataifa zimependekeza Mahakama kama hayo yaliyo maalum na ya kuupinga ufisadi yaanzishwe pia katika nchi nyingine kama vile Nigeria, Romania, Morocco na Bangladesh.
Nchini Tanzania pia kumetolewa miito ya kutaka mahakama hayo yaundwe. Lakini kuna wenye kulipinga wazo hilo. Moja ya hoja zinazotolewa na wapinzani wa dhana hiyo ni uwezekano wa mahakama hayo kutumiwa kisiasa. Wanasema kwamba hayo ndiyo yanayojiri Pakistan.
Hoja nyingine inayotolewa kupinga mahakama maalum ya ufisadi ni ile ya kwamba wanaopandishwa mbele ya mahakama kama hayo, kwa mfano nchini Kenya, si wakubwa wa ufisadi.
Wenye kuhoji hivyo wanaongeza kusema kwamba Rwanda imepata mafanikio yake dhidi ya rushwa na ufisadi licha ya kutokuwa na Mahakama Maalum Dhidi ya Ufisadi.
Miongoni mwa wanaopinga kuanzishwa kwa mahakama kama hayo nchini Tanzania ni Profesa Issa Shivji. Yeye amenukuliwa akisema kwamba haoni haja ya kuanzishwa kwa mahakama maalum ya kusikiliza kesi za ufisadi ila anataka mahakama haya ya kawaida yaimarishwe ili yawe na nguvu za kupambana na kesi za ufisadi. Pia anataka pafanywe mageuzi katika Ofisi ya Dk. Edward Hosea ya kupambana na ufisadi (PCCB).
Yeye mwenyewe Hosea amependekeza paundwe mahakama maalum kuzisikiliza kesi za ufisadi.
Ninavyohisi ni kwamba ingawa hoja za kupinga kuanzishwa kwa Mahakama Maalum Dhidi ya Ufisadi nchini Tanzania zinaingia akilini, hata hivyo ni dhaifu. Ni dhaifu kwa sababu ni wazi kwamba mfumo wa mahakama uliopo sasa umeshindwa kuuzuia ufisadi.
Moja ya sababu zilizopelekea kushindwa kwa mahakama ya kawaida kuzishughulikia kesi za ufisadi ni kwamba mahakama yamelemewa. Na ndio maana inachukua muda mrefu sana kabla ya kesi za ufisadi kusikilizwa na kuhukumiwa.
Ninakubaliana moja kwa moja na wenye kuhoji kwamba paundwe mahakama maalum ya kuzisikiliza kesi za ufisadi, hasa ule ufisadi wa viongozi wa serikali na wakuu wengine katika jamii.
Wananchi wanaoona utajiri wao unaporwa mchana kweupe, mbele ya macho yao, wana kila haki ya kuwaona waporaji hao wakifikishwa mbele ya Mahakama Maalum na kesi zao zinasikilizwa kwa haraka ili waweze kuhukumiwa kwa haraka. Taifa halitendewi haki iwapo hukumu za kesi za ufisadi hazitolewi kwa haraka.
Chanzo: Raia Mwema
No comments:
Post a Comment