Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Mutungi.
Dar es Salaam. Msajili wa Vyama vya Siasa amevinusuru vyama hivyo, kuendelea kunyimwa ruzuku baada ya kuishawishi Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kutumia hekima ili kuepusha mzozo wa kisheria kutokana na uamuzi wa awali.
Katika taarifa yake, msajili huyo, Jaji Francis Mutungi, alisema kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992, utaratibu wa ukaguzi wa mahesabu ya vyama ulikuwa kwa vyama kuweka wakaguzi wake binafsi. Alifafanua kuwa mabadiliko ya sheria hiyo ya mwaka 2009 yaliweka himizo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kufanya ukaguzi huo.
“Mabadiliko hayo kutoka kwa wakaguzi binafsi kuhamishiwa kwa CAG kimsingi yameibua mgogoro na tafsiri ambayo pengine, kwa hakika ndiyo imechangia kuwepo kwa sintofahamu kwamba nani alipe gharama hizo za ukaguzi kati ya vyama na CAG.
“Kutokana na hali hii naomba basi hekima ya PAC kwa maana hiyo, Bunge kutambua kwamba ofisi ya msajili wa vyama vya siasa ikisitisha ruzuku kwa mujibu wa kifungu 18 (3) , kama nilivyobahinisha wakati wa mparaganyiko nilioutaja, haukutokana na utashi au ukaidi wa vyama, tukifanya hivyo tutakuwa tunakiuka sheria,”alisema Jaji Mutungi.
Awali akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukutana na Msajili wa vyama, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe, alisema kusimamishwa kwa ruzuku kunatokana na matakwa ya kisheria.
“Tusiporidhika kama kuna chama kinavunja sheria tuna mamlaka hayo ya kusimamisha ruzuku,” alisema Filikunjombe.
Pia alibainisha kuwa Bunge nalo lina deni la kukuza na kujenga demokrasia na uwezo wa vyama vya siasa hivyo kusitisha ruzuku kwa wakati huu, kutaigubika nchi katika lawama za ukiukwaji wa utawala bora na demokrasia.
“Tumemwomba CAG akamilishe ukaguzi wa vyama vyote tisa ndani ya miezi mitatu, hesabu alizopewa azikague na wale waliosema zipo tayari ofisini kwao wampelekee azipitie. ” alisema .
Alivitaja vyama ambavyo viliwasilisha mahesabu yao kwa CAG kuwa ni CUF, CCM, TLP na NCCR-Mageuzi.
Alisema vyama vya CUF, NCCR Mageuzi na CCM viliwasilisha mahesabu ya mwaka 2010/2011 na TLP iliwasilisha mahesabu ya mwaka 2010/2011 na 2011/2012.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake