Wednesday, October 30, 2013

Nyamlani amvulia kofia Malinzi TFF

Aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Rais wa Shirikisho la Soka (TFF), Athuman Nyamlani

Aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Rais wa Shirikisho la Soka (TFF), Athuman Nyamlani amesema uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo ulikuwa huru na haki huku 'akimvulia kofia' mpinzani wake pekee, Jamal Malinzi ambaye ameshinda nafasi hiyo.

Akizungumza katika mahojiano maalum na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Nyamlani, ambaye alikuwa makamu wa kwanza wa rais katika uongozi uliomaliza muda wake chini ya aliyekuwa Rais wa TFF, Leodegar Tenga, alisema amekubali kuwa ameshindwa kihalali katika kinyang'anyiro hicho.

"Nimekubali kushindwa, na nampongeza Malinzi kwa kushinda kwani uchaguzi ulikuwa huru na wa haki. Kilichotokea ni matakwa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF ambao ndiyo wapiga kura," alisema Nyamlani na kusisitiza.

"Niko tayari kusaidia uongozi wa Malinzi pale nitakapohitajika kwa sababu lengo si kuingia madarakani, bali kuiinua nchi yetu kimichezo na hasa mpira wa miguu."

Malinzi ambaye aliingia katika kinyang'anyiro hicho akiwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha Kagera (KRFA), alishinda wadhifa huo katika Uchaguzi Mkuu wa TFF uliofanyika usiku wa kuamikia juzi jijini Dar es Salaam.

Seneta na Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Yanga, aliibuka na ushindi wa kura 73 dhidi ya kura 52 za mpinzani wake pekee, Nyamlani ambaye pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka cha Dar es Salaam (DRFA).

Nafasi ya Makamu wa Rais ilitwaliwa na aliyekuwa mwenyekiti wa iliyokuwa Kamati ya Ligi ya TFF, Wallace Karia aliyepata kura 67 na kuwashinda aliyekuwa Makamu wa Pili wa Rais kipindi cha uongozi wa Tenga, Ramadhan Nassib kura 52 huku aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega akiambulia kura sita.

Katika hatua nyingine, Nyamlani alikanusha taarifa zilizozagaa jana zikidai kuwa, amelazwa katika moja ya hospitali kubwa za jiji la Dar es Salaam baada ya kuugua ghafla kutokana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa TFF.

Mapema jana, kulienea taarifa kuwa Nyamlani ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alipatwa na mshtuko na kulazimika kulazwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.

"Ni uvumi tu, watu wamekosa cha kuzungumza hasa baada ya uchaguzi kumalizika. Mimi ni mtu wa soka, matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa TFF ni sehemu ya mpira wa miguu. Kwa nini nishtuke na kuugua?" Alihoji Nyamlani katika mazungumzo yake na gazeti hili.
CHANZO: NIPASHE

No comments: