Saturday, October 26, 2013

Nyamlani,Malinzi hapatoshi

Mgombea nafasi ya urais, Jamal Malinzi PICHA|MAKTABA

Dar es Salaam. Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania unafanyika kesho kwenye Uukumbi wa NSSF Water Front jijini Dar es Salaam huku wagombea nafasi ya urais, Jamal Malinzi na Athuman Nyamlani wakigongana kwa sera ya kukuza soka la vijana, wanawake na uwekezaji katika masoko.
Msuguano na mbio za urais ulipamba moto Jumatano baada ya Malinzi kuzindua kampeni zake kwenye hoteli yenye hadhi ya nyota tano, Hyatt Kilimanjaro Kempisky akiwa na wapambe wake waliovaa suti za bei mbaya za rangi nyeusi.
Kwa upande wake Nyamlani alijibu mapigo alipozindua kampeni hizo kwenye Uukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) huku akifuatana na wapambe, baadhi yao wakiwa ni ‘makomandoo’ wa Yanga ambao walikuwa wakiranda huku na huko kwenye ukumbi huo na kugawa vipeperushi vinavyomnadi makamu huyo wa Rais wa TFF anayemaliza muda wake.
Malinzi ametoa ahadi nane nzito na akitaka kupewa siku 100 kupimwa katika utendaji wake na ahadi kuu ikiwa ni kuimarisha idara ya ufundi na kuiongezea bajeti ikiwa ni pamoja na kuajiri wasaidizi wa mkurugenzi wa idara hiyo.
Mpinzani wake, Nyamlani ambaye ni Mmakamu wa Kkwanza wa Rais wa TFF anayemaliza muda wake aliyeingia madarakani mwaka 2008.Vipaumbele vya Malinzi ni kukuza vipaji, kuboresha viwanja kwa kuanzisha kampuni tanzu itakayoingia mkataba na wamiliki wa viwanja ambao ni Halmashauri na chama tawala, CCM, kuwaendeleza waamuzi, kuwaendeleza makocha kimafunzo ndani na nje ya nchi.
Nyamlani ametoa ahadi tisa na ahadi kuu ikiwa ni kuimarisha usimamizi na menejimenti ya soka katika ngazi zote na kutaka apewe miaka minne kutekeleza ahadi zake.
“Vipengele tata vinavyokandamiza masilahi ya klabu katika baadhi ya mikataba inayosimamiwa na TFF vitarekebishwa kama ama kuondolewa kabisa kwa masilahi ya ustawi wa mpira na haki za klabu katika matangazo ya biashara zitalindwa kwa nguvu zote,”alisema.
Athuman Nyamlani (46) , kitaaluma ni mwanasheria na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya Kinondoni.
Ahadi zake
Katika kipindi cha miaka minne, Nyamlani ameahidi kuimarisha usimamizi na menejimenti ya soka katika ngazi zote kwa kupitia nafasi hiyo ya urais sanjari na kushirikiana na viongozi wa klabu na vyama vya soka vya wilaya na mikoa kwa ujumla wake.
Pia, ni kupambana na rushwa, kukuza soka la watoto, vijana na wanawake, kuimarisha uwezo wa rasilimali fedha za TFF, pia kuongeza idadi ya ubora wa waamuzi.
Mbali na wagombea hao wa urais pia uchaguzi huo wa kesho utahusisha nafasi za makamu wa rais ambazo zinawaniwa na Wakili Iman Madega, Wallace Karia na Ramadhani Nassib.
Katika sera zake, Madega anasema: “Nitahakikisha najenga taswira nzuri ya shirikisho mbele ya jamii ambayo itakuwa chachu ya wadhamini kujitokeza kwa wingi kudhamini mpira.
Karia akinadi sera zake alisema: “Nakerwa sana na mambo ya ubabaishaji, kama Jumapili nikichaguliwa Jumatatu naanza kudili na tiketi za eletroniki hasa Uwanja wa Taifa ambao mitambo imefungwa, lakini watu wanachelewesha kwa makusudi zoezi la kuanza kutumia tiketi hizi.
Naye Nassibu anasema: “Naumia ninapoona Chama cha Makocha Tanzania (TAFCA), Chama cha Waamuzi wa Soka (FRAT), Chama cha Madaktari wa Michezo (TASMA) na Chama cha Wachezaji (SPUTANZA) vikiwa kama yatima wakati uwezekano wa kuvisaidia upo. Unajua kwa nafasi ninayoiomba nitakuwa na sauti kubwa tofauti na ilivyokuwa mwanzo.
Wengine watakaochuana kesho ni wajumbe 45 ambao wanawania kuwakilisha Kanda mbalimbali wakiwania ujumbe wa kamati ya utendaji wa shirikisho hilo.
Mwananchi

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake