Monday, October 28, 2013

Sumaye apigwa zengwe

Waziri Mkuu mstaafu,Frederick Sumaye

Vita ya urais wa mwaka 2015 ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imeendelea kuwavuruga vijana nchini. Safari hii mvutano huo umejidhihirisha kwa vijana wa asasi isiyo ya kiserikali inayojihusisha na kuelimisha jamii kuhusu usalama na amani (Public Terrorism Awareness Trust Fund and Human Welfare (PTA-HW).

Asasi hiyo jana ilijikuta ikigonganisha wageni rasmi ambao walialikwa kufungua tamasha la siku moja la Mbio za Amani kwa kumzuia Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, kwa kumueleza kuwa tamasha hilo limeahirishwa.

Hata hivyo, badala yake asasi hiyo ilimkaribisha Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kutoka Wilaya ya Bukoba Vijijini, Nazir Karamagi, kulifungua.

Asasi hiyo iliandaa tamasha hilo lililofanyika katika viwanja vya Mnanzi Mmoja jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na vijana kutoka vikundi 41 vya Zanzibar, Dar es Salaam na Pwani.

Dalili za kuwapo kwa mgawanyiko miongoni mwa waandaaji zilionekana baada ya kuwasili kwa Karamagi ambaye hakuwa ametarajiwa na waandaaji pamoja na washiriki wa tamasha hilo.

Mgeni rasmi aliyekuwa akitajwa kwenye tamasha hilo ni Sumaye, lakini badala yake alijitokeza Karamagi.

Baadhi ya vijana na wajumbe wa kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, walisikika wakilaumu uwapo wa Karamagi na kuzua minong’ono baina ya washiriki huku kundi moja likisema kuwa lilimtaka Sumaye na lingine likimtaja Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, ambaye walisema ndiye aliyealikwa awali.

NIPASHE iliwasiliana na Sumaye kwa njia ya simu kutaka kujua kilichosababisha asiende kufungua tamasha hilo bila taarifa, lakini alionekana kushangazwa na taarifa za kufanyika kwa tamasha hilo wakati alielezwa kuwa limeahirishwa.

“Jamani! Tamasha limefanyika? Nikiwa najiandaa kwenda nilielezwa na mmoja wa walinzi wangu kuwa limeahirishwa, hivi ndiyo nasikia kutoka kwako kuwa tamasha limefanyika,” alisema huku akionyesha kushangazwa na hatua hiyo.

Sumaye alisema tangu awali alijua kuwa yeye ndiye mgeni rasmi na viongozi wa taasisi hiyo walikuwa wakiwasiliana kwa karibu na wasaidizi wake.

Alifafanua zaidi kwamba alishaandaa hata hotuba ya ufunguzi na kusisitiza kwamba hakuwa na taarifa za kuahirishwa kwake.

“Nilichoelezwa ni kuwa mambo hayakwenda ilivyotarajiwa, hivyo tamasha limeahirishwa hadi wakati mwingine…ukiniambia limefanyika, nawashangaa, ila nitaitisha mkutano na waandishi wa habari hivi karibuni kulizungumzia hilo na mengine,” alisema Sumaye.

Kwa upande wake, Karamagi alipoulizwa alisema viongozi wa tamasha hilo walifika ofisini kwake na kumuomba awe mgeni rasmi na akakubali.

“Sikujua lolote zaidi ya vijana hawa kufika ofisini kwangu na kuniomba niwe mgeni rasmi, kwa kuwa sikuwa na kizuizi, nilifika na kufungua na kuwapa Sh. milion 10 ili waimarishe taasisi yao,” alisema Karamagi ambaye alijiuzulu Uwaziri wa Nishati na Madini mwaka 2008 kutokana na kashfa ya Richmond.

Mratibu wa Taifa wa PTA, Fanuel Sabuni, alisema alikuwa nje ya nchi na baada ya kurejea juzi, alielezwa kuwa mawasiliano na Sumaye hayakuwa mazuri kwa kuwa hadi dakika za mwisho alishindwa kuthibitisha hivyo waliamua kubadili mgeni rasmi.

Alisema awali mgeni aliyependekezwa na kamati ya maandalizi ni Makamu wa Rais, lakini ilishindikana kumpata kutokana na mwingiliano wa ratiba na ndipo wajumbe wa kamati walipotakiwa kupendekeza mgeni mwingine.

Aliyepewa jukumu la kuwasiliana na Sumaye, Peter Celestine, alipoulizwa alisema mtu wa karibu na Waziri Mkuu mstaafu huyo ambaye hata hivyo, hakumtaja jina, ndiye aliyewaeleza kuwa hawawezi kuonana naye na kwamba wiki moja kabla walishindwa kuonana naye ili kumueleza lengo la tamasha na mambo ambayo wangependa ayazungumzie.

“Tamasha hili limeahirishwa zaidi ya mara moja, awali lilikuwa lifanyike Oktoba 13 na ya pili Oktoba 20, mwaka huu kila mgeni tuliyemtafuta ratiba zake hazikuendana na zetu,” alisema.

Celestine aliongeza kuwa alipewa jukumu la kuwasiliana na Sumaye, lakini watu wake wa karibu walimkatisha tamaa na kwamba aliamua kurudisha jibu kwenye kamati watafute mgeni mwingine.

“Mimi mwenyewe nimeshtuka Karamagi akiwa getini, sikujua kama ndiye mgeni wetu. Kwenye kutafuta wageni rasmi tuliangalia watu ambao hawajihusishi na siasa moja kwa moja, mfano Sumaye ameshastaafu, Karamagi naye alishatoka kwenye siasa, lengo tusiingize siasa kwenye taasisi,” alifafanua.

Pamoja na Celestine kusema kuwa Karamagi ameshatoka kwenye siasa, lakini ukweli ni kuwa ni mjumbe wa NEC Wilaya ya Bukoba Vijijini mkoani Kagera na alishinda nafasi hiyo katika uchaguzi wa CCM wa mwaka jana.

Akizungumza na vijana hao, Karamagi alisema ni vyema jamii ikaondokana na imani kuwa kila panapotokea vurugu washiriki wakubwa ni vijana na iwapo watapewa elimu na michezo ya kuwaleta pamoja itasaidia kuwajenga kifikra.

Vita ya kusaka urais ndani ya CCM inaendelea kuyatesa makundi kadhaa likiwamo la vijana.

Katika uchaguzi wa CCM mwaka jana, baadhi ya makada wanaousaka urais walidaiwa kuzitumia jumuiya za vijana, wanawake na wazazi kwa ajili ya kuimarisha mitandao yao.

Hata hivyo, chaguzi za Jumuiya ya Vijana wa Chama hicho (UVCCM) katika ngazi zote yaliibuka malalamiko ya baadhi ya wanaosaka urais kupenyeza fedha kutaka kuungwa mkono na vijana huku vijana wenyewe wakiwa katika mgawanyiko mkubwa.

Mbali na kuwalenga vijana wa CCM, makada hao pia wamekuwa wakitafuta kuungwa mkono na makundi ya vijana kutoka asasi mbalimbali wakiwamo wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu.

Tukio la jana nalo linaelezwa na wachambuzi wa siasa kwamba lina mkono wa makundi yanayohasimiana kisiasa hususani yanayousaka urais katika uchaguzi wa mwaka 2015.

Karamagi anatajwa kuwa ni mtu wa karibu wa mmoja wa makada wanaousaka urais.

Wanaotajwa kuwa na nia ya urais ni Sumaye; Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa; Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Wengine wanaotajwa ni aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa (UN), Dk. Asha-Rose Migiro na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake