Baadhi ya watu wakiwe kwenye chumba alichoingilia muuaji kama inavyoonekana juu. Picha na Editha Majura
Usiku wa Alhamisi iliyopita, mkazi wa mtaa wa Malela, Mbagala, Jijini Dar es Salaam, Anna Mbago (35) aliuawa kwa kunyongwa na mtu aliyeingia chumbani kwake baada ya kutoboa dari.
Inaelezwa kuwa mtu huyo aliingia kupitia sebuleni, Anna alisikia kishindo, alipotoka chumbani kwenda kuangalia ndipo akakutana na muuaji ambaye alimnyonga.
Hata hivyo kabla ya umauti, Anna alipiga kelele zilizosababisha baadhi ya majirani kuizingira nyumba. Kilio chake hakikuzuia asiuawe kwa vile hata majirani walishindwa kuingia kwa vile nyumba ilikuwa imefungwa; Muuaji aliendelea kumnyonga hadi kufa licha ya kuomba asiuawe.
Majirani waliosikia kilio cha kuomba msaada waliizingira nyumba hiyo wakihangaika namna ya kuingia ndani bila mafanikio, kwani milango yote ilikuwa imefungwa.
Baadaye walitoa taarifa polisi kupitia kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Malela, wakati askari wanafika Anna hakuwa anaendelea kupiga kelele za kuomba msaada, huku wengi wakifikiri labda amejificha au amekufa.
Polisi walipoingia walimkuta Anna kwenye korido, akiwa hajitambui, walipompeleka hospitali ndipo ikathibitika kwamba alikuwa amekufa.
Muuaji alikutwa amejificha chooni ndani ya nyumba hiyo, anasema Mkuu wa Upelelezi katika Wilaya ya Kipolisi ya Mbagala, Thobias Walelo.
Polisi wakiri kweli elimu haina mwisho
Wahenga walisema ‘Elimu haina mwisho’. Usemi huu umethibitika kwa kamanda wa upelelezi wa Wilaya ya kipolisi Mbagala, mkoani Temeke, Jijini Dar es Salaam, Thobias Walelo wakati akizungumzia mauaji ya Anna Mbago (35).
“Unaposikiliza maelezo ya muuaji, ukizingatia mazingira ya tukio, siyo rahisi kuamini kilichotokea, nakiri tukio hili ni la aina yake kwangu, limenidhihirishia kuwa elimu haina mwisho, napaswa kuendelea kujifunza zaidi kama ambavyo wanadamu tunapaswa kuendelea kujifunza bila kuchoka hadi siku ya mwisho wa uhai wetu,”anaeleza ASP Walelo.
Mtuhumiwa akijieleza;
“Naitwa (jina tunalo), ninafanya biashara ya sigara, naishi Mbagala” anasema mtuhumiwa wa mauaji hayo akiwa mikononi mwa polisi.
Anasema Oktoba 10 mwaka huu, saa 4:00 asubuhi aliondoka nyumbani kwao, akitembea kwa miguu kwa lengo la kutafuta riziki.
“Nikafika sehemu nisiyoifahamu, nikasogelea nyumba moja na kuchungulia dirishani, nikaona mwanamke akihesabu fedha, zikanitamanisha na kuanza kutafuta jinsi ya kuingia ndani ya nyumba hiyo,”anaeleza mtu huyo ambaye, anasema hadi wakati anakamatwa hakuwa ameiba kiasi chochote cha fedha.
Anasema tukio hilo alilifanya saa 2: 00 usiku. Ni kwamba alipofika kwenye nyumba hiyo akagundua upande wa kulia wa nyumba hiyo, kwenye dari kumeachia kidogo, hivyo akazunguka upande wa mbele ya nyumba na kukwea kwenye kibaraza.
Akaambaa na ukuta mpaka eneo ambalo dari ilionesha kuachia, akaipasua na kuingia ndani mpaka sebuleni. Anasema hapo pia alifumua dari na kudumbukia ndani kwa kutua kwenye moja ya sofa.
Anasema Anna alishtushwa na kishindo chake alipotua kwenye sofa, hata hivyo kwakuwa alishafunga milango, hakuweza kukimbilia nje zaidi ya kupiga kelele akiomba msaada.
“Nilimkimbilia na kumzuia asipige kelele lakini hakuacha, nikamkaba ili asiendelee kupiga kelele, tukapambana nikamshinda nguvu, nikamkaba mpaka alipoishiwa nguvu,” anaeleza mtuhumiwa huyo.
Mdogo wa marehemu anena
Anthony Mhando ambaye ni mdogo wa marehemu anasema awali dada yake alikuwa askari wa JWTZ Luvu kikosi 832KJ akifahamika kwa jina la Asha Mhando.
Aliacha kazi, akabadili dini na kuitwa Anna Mbago alipoolewa na Joseph Mbago ambaye kwa sasa ni mtumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT)
Anasema awali, pamoja na mume wake walikuwa wakiishi na Nelson na Samwel Kimei - watoto wa ndugu wa mume pamoja na Kombo - mtoto wa mume wake.
Lakini mpaka anapatwa na mauti, Anna kwa zaidi ya mwaka hivi alikuwa akionekana na majirani akiishi peke yake.
“Dada yangu hakuwahi kupata mtoto, ikiwa kuna mkono wa mtu, kila nafsi itaonja mauti,” anaeleza Mhando.
Majirani nao wanasema
Mmoja wa majirani aliyejitambulisha kwa jina la Edward Fransis Lijawa anasema, kwa kuwa anayetuhumiwa kumnyonga Anna mpaka kufa, yupo mikononi mwa polisi, tena akiwa hai, wanahitaji kupata jibu la maswali yaliyogubika tukio hilo.
Jirani mwingine, Salma Maleta anasema siku ya tukio aliachana na Anna saa 2:00, nusu saa baadaye alipokea simu akitaarifiwa kuwa rafiki yake huyo amevamiwa na majambazi.
“Siyo kweli kwamba aliyemuua alikuwa mwizi kwa sababu hapa mtaani tunafahamu hali ya maisha ya huyu dada, (marehemu) hata fedha ya kula tulikuwa tukimsaidia, hakuwa na kitu, ni dhahiri walilenga kumuua tu,” anaeleza Maleta.
Mume wa marehemu alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo anasema “Ninashauri kama mnataka maelezo muwasiliane na kamanda wa upelelezi kwenye kituo cha Mbagala atawaeleza kilichotokea”.
Maswali kuhusu tukio
Maswali yanayoumiza vichwa vya wengi katika tukio hilo ni je, ilikuwaje jambazi akafahamu kuwa ukuta unaotenganisha nje na ndani kwenye eneo la paa haujafika juu?
Alijiamini vipi kuingia ndani ya nyumba, tena bila hata silaha ikiwa hakufahamu kuwa mama huyo alikuwa peke yake ndani ya nyumba?
Ikiwa lengo lake lilikuwa kuiba, kwanini wakati akiombwa amuachie ili ampe chochote anachotaka, hakutekeleza hilo badala yake alimnyonga mpaka kufa?
Baadhi ya majirani wameshauri kuundwa tume ya siri kuchunguza tukio hilo kwa kushirikiana na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), kwa kile wanachosema kuwa kifo cha Anna kimejaa utata, hivyo ni vema ukweli ujulikane.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment