ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 4, 2013

Jifunze kiswahili uwafunze wengine



Nawaleteeni mwendelezo wa makala kuhusu matumizi bora ya Kiswahili fasaha. Lengo ni kuwasaidia waandishi na wanafunzi wa Kiswahili kuzingatia misingi ya lugha ya Kiswahili kwa manufaa yetu sote. Angalia sentensi zilivyokosewa na usahihi wake unavyotakiwa kuwa.
“Uamuzi huo unapeleka ujumbe wenye nguvu na udhabiti kwa jamii ya kimataifa.”
Kuchanganya maneno udhabiti na uthabiti ni athari ya lugha za asili katika Kiswahili. Kwa usahihi neno linalofaa hapa ni uthabiti kwa maana ya uimara au hali ya kuwa imara. Kwa hakika sijapata kuona neno udhabiti bali linalofahamika ni uthabiti kutoka katika neno thabiti. Maana yake ni kuwa imara au madhubuti na isiyotetereka.
“ Ili mapambano dhidi ya rushwa yafanikiwe ni budi adhabu kwa wahusika ziwe wazi na zichukuliwe hatua.”
Tunaposema ni budi lazima ifahamike kuwa tunaipotosha lugha ya Kiswahili. Ni budi maana yake ni hiyari, si lazima. Kwa usahihi tungesema ‘hawana budi’. Kwa hiyo isomeke,
“ Ili mapambano dhidi ya rushwa yafanikiwe hawana budi wahusika wapewe adhabu zilizo wazi na hatua zichukuliwe.”
“Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya imefanya kazi kubwa mpaka hadi katika mchakato huo.”
Maneno ‘hadi na mpaka’ yametumika kwa mfuatano wakati yana maana inayofanana. Ilitakiwa neno moja ama mpaka au hadi litumike na wala siyo yote kwa pamoja.
“ Kabwe amesisitiza kuwa hasabu za Chadema ni miongoni mwa ambazo hazijakaguliwa”.
Neno moja limekosekana ili kukamilisha sentensi hii. Neno hilo ni ‘hesabu’. Ingeandikwa,
“ Kabwe amesisitiza kuwa hesabu za Chadema ni miongoni mwa hesabu ambazo hazijakaguliwa”.
“ Kongamano la wawekezaji lilitayarishwa na Kituo cha Uwekezaji (TIC) Kanda ya Kaskazini kwa dhumuni la kuvutia wawekezaji.”
Limetumika neno ‘dhumuni’ kimakosa. Neno madhumuni ndilo sahihi na halina umoja. Kwa hiyo ingeandikwa “…kwa madhumuni ya kuvutia wawekezaji.”
“ Hali hiyo ilijitokeza baada ya mahakama kuhairisha kesi hiyo kufuatia maelezo ya upande wa mashtaka kuwa upelelezi haujakamilika.
Waandishi wengi wanashindwa kutofautisha kati ya kuahirisha na kuhairisha. Neno lililo sahihi ni kuahirisha kwa maana ya kuchelewesha jambo kwa makusudi ili lifanyike baadaye. Tunaahirisha mkutano, semina au hukumu ya kesi, n.k.
“Anapata mahitaji yake wakati wa usiku na kutahadharisha kuwa mara kadhaa alinunua bidhaa asiyokuwa akitarajia”
Ni jambo jema kutumia maneno machache pale inapoonekana inafaa bila kupoteza maana. Kwa mfano, kwa maneno ‘asiyokuwa akitarajia’ iwe ‘asiyotarajia’.
“Ukisikia njenjele, pesa hicho ndicho kinachotegemewa kuonekana katika msimu huu”.
Neno tegemewa limekosewa kutumika hapa. Wengi wetu hutumia neno kutegemea kuwa na maana ya kutarajia, kutazamia au kutumainia. Kutegemea ni kushikilia, kuegemea, au kuzuilia. Kwa mfano tunasema,
-Mtoto humtegemea mzazi wake kwa mahitaji ya maisha.
- Tanzania hutegemea kilimo kwa uchumi wake, n.k. Kwa hiyo isomeke,
“ Ukisikia njenjele pesa, hicho ndicho kinachotarajiwa kuonekana katika msimu huu”.
“ Kila ifikapo Septemba 22 kila mwaka hukutana na kufanya kampeni mpaka ikawekwa kwenye kalenda/shajara ya Matukio ya Dunia mwaka 2000 na sasa karibia nchi nyingi huisherehekea”.
Tunasoma maandishi yanayotumia neno karibia likiwa na maana ya karibu, takriban, nusura, n.k. Hata hivyo maana ya karibia ni sogea, jongea , jongelea, n.k. Hivyo kwa usahihi tungetumia ‘ … mwaka 2000 karibu nchi nyingi huisherehekea’.
“ Ligi Kuu inayoendelea inasubiriwa kwa hamu kubwa na washabiki wa soka nchini”.
Yako maneno mawili yanayokosewa tunapoyatumia katika wingi. Neno la kwanza ni shabiki na la pili ni mkandarasi Wingi wa shabiki ni mashabiki na wala siyo washabiki kama ilivyoandikwa hapo juu. Pia wingi wa neno mkandarasi ni makandarasi na wala siyo wakandarasi. Kwa hiyo tuwe makini tunapoyatumia.
Mwananchi

No comments: