Kama ndiyo mara ya kwanza kukutana nami katika ukurasa huu nakukaribisha kwa moyo mkunjufu ujiunge nasi katika klabu hii isiyo na mateso ya uhusiano.
Haya twende kwenye somo letu sasa. Marafiki zangu; nimesema mara nyingi sana, mapenzi hayana kanuni za moja kwa moja. Huwezi kukuta kanuni ya mapenzi mahali popote.
Kila siku ni kujifunza kitu kipya. Ngoja nikuulize kitu. Je, uko katika urafiki na msichana au mvulana kwa muda mrefu na unatamani awe wako lakini unashindwa kumwambia?
Je, umeona dalili za rafiki yako kukutaka kimapenzi lakini anakuwa mzito? Je, wewe pia unamhitaji?
Achana na hilo, inawezekana si wewe. Je, huwahi kusikia vitu kama hivyo kwa rafiki au mtu wako wa karibu? Kama ndivyo, somo hili litakuwa na umuhimu zaidi kwako.
URAFIKI
Urafiki ni muunganiko mzuri. Marafiki husaidiana na kupeana siri zao. Mara nyingi marafiki huwa wa jinsi moja lakini wakati mwingine hutokea, watu wa jinsi tofauti wakaingia kwenye urafiki na kushibana kwelikweli.
Hapo sasa ndipo kila mmoja anaweza kumjua mwenzake vizuri zaidi. Kwa sababu makubaliano ni urafiki, hakuna atakayeigiza maisha yake. Kila mmoja ataishi maisha yake halisi kwa kuwa anajua kuwa yupo na rafiki yake.
Wakati fulani hisia huweza kubadilika na mmoja wao kuanza kuhisi kumpenda mwenzake. Kwa bahati mbaya ni kwamba, huwa na uwezekano mkubwa sana wa hisia hizo kugongana.
Yaani kila mmoja anaweza kujikuta amempenda mwenzake lakini akaamini ni hisia zake mwenyewe za ndani ambazo hazihusiani na mwenzake. Hapo sasa anabaki na mzigo wake moyoni.
Wapo wengine baada ya kuona hivyo, huanza maneno mengi, mifano na mafumbo hutawala kati yao, akiamini kwamba mwenzake ataelewa na kumpokea katika himaya yake.
Wachache wanafaulu lakini ukweli ni kwamba wengi wanafeli (hasa wanaume). Ni ngumu kwa mwanamke kumfungukia mwanaume kuwa anampenda na angependa kuwa mpenzi wake (niliwahi kuandika mada huko nyuma kuwasaidia wanawake namna ya kuanzisha uhusiano kwa wanaume wanaowapenda).
Ukibaki na longolongo bila kusema ukweli, miaka itaenda mkiwa marafiki tu maana hutaki kueleza ukweli. Ngoja nitakuambia kitu muhimu rafiki yangu. Tuendelee...
UCHUNGUZI WA HISIA
Kama ni kumchunguza, kutokana na urafiki wenu utakuwa umeshamchunguza vya kutosha. Kilichobaki ni kuangalia zaidi hisia zako kama ni za ukweli. Je, unampenda kwa dhati? Moyo wako umekuthibitishia hilo?
Kama una uhakika kweli unampenda kwa dhati na unaweza kumvumilia kwa hali yoyote, kipengele kinachofuta ni muhimu sana kwako.
UNAWEZA KUMPOTEZA
Longolongo zako hazitasaidia kitu. Ukimya wako unaweza kumfanya aendelee kukuona wewe kama rafiki wa kawaida huku ukiendelea kuteseka kihisia.
Kitakachotokea ni kwamba, ataamua kutafuta au kuingia kwenye uhusiano na mwingine kwa sababu anajua wewe ni rafiki tu.
Hata kama naye anakupenda, kwa sababu husemi kitu, hawezi kujichoresha kwa kufungua mdomo wake na kuweka wazi hisia zake.
Mbaya zaidi, anaweza kukutambulisha kwa mpenzi wake baada ya kukubaliana kwa vile anajua kuwa wewe ni rafiki yake tu! Hata ukisema neno gani, hutaeleweka na utabaki na maumivu yako moyoni!
BADO UNASUBIRI TU!
Upo kwenye uhusiano wa aina hiyo? Upo na rafiki yako na una uhakika unapenda lakini bado hujamwambia hisia zako? Acha hizo...haraka sana funguka!
Mweleze hisia zako, si ajabu na yeye alikuwa akikusubiri tu wewe useme kuwa unampenda! Vipi, unaogopa kumwambia? Acha woga.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vitatu; True Love, Lets Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.
1 comment:
Lakini hata ukimuambia unampenda anazidi kwenda kwa wakenya anatoka nae out mbela za watu ,.unakuwaunmakatisha mtu tamaa .anakufanya wewe mtu wa kuifichwa,tu sio nzuri ,kama binadamu unatakiwa kufikiria
Post a Comment