Baada ya mazoezi ya timu hiyo kumalizika kwenye uwanja huo majira ya saa tano asubuhi huku kukinyesha mvua, Brandts aliingia kwenye gari lake akifuatwa na Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh ambaye naye aliingia kwenye gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser na kukabidhi mkataba kwa kocha huyo.
NIPASHE lilifuatilia kwa kina kilichokuwa kinaendelea ndani ya gari hilo na kumshuhudia Brandts akitia saini mkataba huo uliokuwa na kurasa nyingi ziliozokuwa kwenye karatasi za rangi ya njano. Baada ya dakika takriban tatu. Brandts alisaini kisha Hafidh akatoka kwenye gari hilo.
Akizungumza na mwandishi wetu kabla ya kuondoka uwanjani hapo, Baransts (57), alikiri kusaini mkataba huo baada ya kumalizana na uongozi wa Yanga.
"Ndiyo, nimesaini mkataba mpya na Yanga mbele ya Meneja wa Timu (Saleh). Kama kawaida yangu, sihitaji mkataba mrefu zaidi, hivyo nimeingia nao mkataba wa mwaka mmoja tu," alisema Brandts.
Hata hivyo, alipofuatwa na mwandishi uwanjani hapo, Saleh alikataa kuzungumza chochote kuhusu suala hilo kwa kusema: "Mkataba wa kocha ni moja ya masuala ya ndani ya timu, siwezi kulizungumzia suala hilo."
Lakini Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alikiri uongozi wa klabu hiyo kumalizana na Brandts baada ya kuulizwa na gazeti hili jana mchana.
Mkataba huo unamfanya Brandts awe mali ya Yanga hadi mwishoni mwa Septemba mwakani.
Beki huyo wa zamani wa Timu ya Taifa ya Uholanzi, alijiunga na Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja Septemba 29, mwaka jana akitokea klabu ya 'maafande' wa APR ya Ligi Kuu ya Rwanda.
Brandts alianza rasmi kukinoa kikosi cha Yanga alichokipa ubingwa wa msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Oktoba 8, mwaka jana akianza na kichapo cha bao 1-0 dhidi ya mabingwa wa Kombe la Tusker 2006, Timu ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Kagera.
Kutua kwa kocha huyo Yanga, kulitokana na uamuzi wa klabu hiyo kuachana na aliyekuwa Kocha Mkuu, Mbelgiji Tom Saintfiet, ambaye licha ya kuwapa ubingwa wa Kombe la Kagame, walimtimua baada ya kuiongoza timu yao katika michezo miwili tu ya mwanzo msimu uliopita waliyotoka suluhu dhidi ya Prisons jijini Mbeya Septemba 15 kabla ya kuchapwa 3-0 na mabingwa wa Tanzania Bara 1999 na 2000, Mtibwa Sugar mjini Morogoro Septemba 19, mwaka jana.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake