ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 19, 2013

ETI WANANDOA, MBONA KILA MTU SIMU YAKE INA PASSWORD?


NI matumaini yangu kwamba mu wazima kabisa na mnaendelea vyema na majukumu yenu ya kila siku kama kawaida. Mimi mzima, nashukuru Mungu kanifanya kuwa kati ya wale wanaoendelea kuvuta hewa yake bila malipo yoyote.

Mpenzi msomaji wangu, tatizo la simu za mkononi kuwa chanzo cha migongano ndani ya ndoa limekuwa sugu katika siku za hivi karibuni. Si kitu cha ajabu kusikia wanandoa wameachana, wamenuniana au hata kupigana kisa kikiwa ni simu ya mkononi.
Mke atakuta sms ambayo haielewielewi kwenye simu ya mumewe, atashindwa kuvumilia, atauliza na matokeo yake kuibua zogo. Mume atamsikia mkewe anaongea na simu na mwanaume atahoji ni nani na akipewa jibu lisiloeleweka, lazima pachimbike.

Kwa kifupi wengi wamekuwa wakituhumiana kwa usaliti kwa sababu tu kila mwanandoa anahisi mwenzake ana mawasiliano yasiyofaa na watu wa jinsia nyingine hata kama katika uhalisia mawazo hayo hayana ukweli.
Utakumbuka kupitia safu hiihii niliwahi kuzungumzia mambo ambayo unatakiwa kuyafanya pale unapoona mwenzako anahisi siyo muaminifu kisa umekuwa hutaki aiguse simu yako au hutaki kabisa kushirikiana naye simu, yaani kila mmoja awe na yake kwa matumizi yake binafsi.

Lakini sasa, baadhi ya dini zinaeleza kuwa, wawili wanapofikia hatua ya kufunga ndoa wanaunganishwa na kuwa mwili mmoja. Yaani wanashirikiana kwa kila jambo.
Kibaya ni kwamba, katika siku za hivi karibuni dhana hii haifanyi kazi tena. Licha ya ndoa kufungwa, wengi kila mmoja anabaki kuwa yeye, wanashirikiana katika yale ambayo yana ulazima tu.

Katika hili ndiyo maana ni wachache sana ambao wanaweza kusema kwa kuwa wameoana basi watumie simu moja au hata kama kila mmoja atakuwa na yake basi linapokuja suala la matumizi, mke aweze kuchukua ya mumewe na kutumia au mume achukue ya mkewe, aweke vocha, atume sms au apige. Hilo ni gumu katika ndoa nyingi za sasa.

Baadhi wamewekeana masharti kabisa kwamba kila mmoja na simu yake na ya mwenzake inapoita hata kama yuko mbali asipokee. Vivyo hivyo kwa sms. Ikitokea mmoja akaenda kinyume na makubaliano hayo lazima patachimbika! Hayo yanatokea huko mtaani na huenda wewe unayesoma makala haya inakugusa pia.

Katika kuonesha kwamba bado kuna walakini kwa wanandoa wengi, licha ya kuwekeana masharti kwamba kila mmoja na simu yake, wengi wamekuwa hawaaminiani.
Kila mmoja anahisi mwenzake anaweza kuichukua simu yake na kusoma sms zilizoingia na kutoka hivyo kuweza kuleta matatizo. Kutokuaminiana huko ndiko ambako kumewafanya wengi kuzifunga simu zao kwa kitu kinachoitwa password.

Ukijaribu kufuatilia utabaini kuwa asilimia kubwa ya wanandoa kila mmoja simu yake ina password hivyo kuwa ngumu kuwepo kwa ushirikiano kwa namna yoyote wa simu hizi za mkononi. Swali la kijiuliza hapa ni kwamba, kwa nini tunafikia hatua hiyo kama kweli tunapendana na kuaminiana?

Itaendelea wiki ijayo.

GPL

No comments: