Kadhalika, ametoa wito kwa wakandarasi nchini kujenga barabara zenye viwango huku akiwataka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kusimamia sheria kwa yeyote atakayekiuka makubaliano ya mkataba.
Aliyasema hayo jana wakati wa uwekaji saini wa mradi wa ujenzi wa barabara za Dodoma-Babati na Tunduru, Mangaka- Mtambaswala kati ya Tanzania na Benki ya Maendeo Afrika (ADB) na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (Jica) wenye thamani ya Sh. bilioni 538.8 Dk. Magufuli alisema barabara nyingi za nchini zinaharibika kutokana na magari ya mizigo kuzidisha uzito.
Alisema serikali isiposimamia sheria hiyo barabara zitakuwa zinaharibika kila mara, na mwishowe mikopo hiyo italipwa na Watanzania maskini katika kodi zao huku barabara hizo zikiwa mbovu.
“Hizi fedha tumekopeshwa sisi na watakaolipa ni Watanzania, hivyo wakandarasi mnatakiwa kujenga barabara zenye viwango na nyie Tanroads mhakikishe mnayabana magari yaliyozidisha uzito,” alisema Dk. Magufuli.
Aliongeza kuwa serikali haitakuwa tayari kurudia rudia kujenga barabara moja mara mbili kutokana na uzembe wa watu wachache wanaoharibu barabara, na kuwataka wakandarasi nchini kujenga barabara zenye ubora.
Dk. Magufuli alisema katika nyingine magari ya mizigo yana viwango vya uzito akitolea mfano Marekani kuwa ni tani 36.2, Uingereza tani 40, Ujerumani tani 40. Ufarasa tani 40, Urusi tani 38, lakini kwa Tanzania ni tani 56 ambacho ni kiwango kikubwa.
“Na nitaendelea kusema ukweli pasipo kumwogopa mtu hadi naenda kaburini, gari lolote litakalozidisha mzigo nitalitoza faini kwa mujibu wa sheria, tunataka barabara zetu zidumu kwa miaka mia moja,” alisema Dk. Magufuli.
Dk. Magufuli alisisitiza kuwa ikiwa serikali itaamua kuyaachia magari ya mizigo kuzidisha kiwango cha uzito, barabara zitaendelea kuharibika kila siku.
Waziri Magufuli aliwataka wahandisi wa mikoani kusimamia miradi hiyo ya barabara na kueleza kuwa miradi hiyo ikifeli na wahandisi wao watakuwa wamefeli.
Dk. Magufuli ametoa kauli hiyo wakati mgogoro baina ya serikali na wasafirishaji nchini kabla haujapata ufumbuzi.
Wasafirishaji hao Chama cha Wamiliki wa Malori (Tatoa) na Chama cha Wamilikiwa Mabasi (Taboa) Oktoba 8 na 9, mwaka huu waligoma wakipinga kufutiwa msahama wa kutozwa faini asilimia tano kwa kuzidisha uzito.
Mgomo huo ulifuatia tangazo la waziri magufuli Oktoba Mosi, mwaka huu kufuta msamaha huo na kurejesha sheria ya mwaka 1973.
Baada ya mgomo huo uliotikisa nchi, Oktoba 10, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliingilia kati na kusitisha tangazo la Dk. Magufuli huku akitoa mwezi mmoja kwa serikali kukutana na wadau wa usafirishaji kupata mwafaka.
Hata hivyo, hadi kumalizika kwa muda huo mwafaka haujapatikana huku serikali ikisema timu hiyo imeanza kazi wakati wadau wa usafirishaji wakisema hawajashirikishwa.
Jana NIPASHE lilimtafuta Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu, ambaye alisema kwa sasa hawatozwi tozo yoyote isipokuwa wanaiomba serikali kuyaruhusu mabasi kutoingia kwenye mizani kama nchi zingine za Afrika Mashariki zinavyofanya.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Florence Turuka, alisema timu ya kusaka mwafaka wa mgogoro huo na wadau wa usafirishaji inaendelea na vikao, na kueleza kuwa kikao cha mwisho kilifanyika Novemba 29, mwaka huu.
Aliongeza kuwa wiki hii timu hiyo iliyojumuisha wanasheria kutoka Wizara ya Uchukuzi, Ujenzi, Wizara ya Viwanda na Biashara, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Taboa na Tatoa wanatarajia kukaa tena.
Alisema timu hiyo inatarajia kumaliza vikao vyake Desemba 10, mwaka huu, na mpaka sasa wameshapitia hadidu za rejea mbalimbali zilizowasilishwa na wajumbe wa timu hiyo.
ATHARI ZA MGOMO
Mgomo wa wasafirishaji ulisababisha Bandari ya Dar es Salaam kuelemewa mizigo.
Takribani tani 23,165 za mbolea ambazo zilikuwa zimeshushwa bandarini hapo zilikwama kutokana na kutokuwapo kwa malori.
Kadhalika, takribani meli tisa za mizigo zilikwama kushusha na kupakia mizigo bandarini.
Vile vile, uwezo wa kushusha makontena katika bandari hiyo ulishuka kutoka makontena 800 kwa siku hadi 300.
CHANZO: NIPASHE
Mheshimiwa waziri wa Ujenzi, kwa heshima na taadhima ninakuunga mkono kwa uzalendo na nchi yako na msimamo wako, vinginevyo tutakuwa tunapiga ''marktime'' bila kusonga mbele. Ni mfano wa kuigwa kwa taifa la Tanzania.
ReplyDeletehaiwezekan gar zispte kwny mizan hii nchi itakuwa inakaliwa na watu au wanyama?
ReplyDelete