Thursday, December 5, 2013

Tanzania yatengewa tiketi 260 Kombe la Dunia

SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (FIFA), limeipa Tanzania mgawo wa tiketi 260 za fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu, Watanzania wanaohitaji tiketi hizo wanatakiwa kutuma maombi kwa maandishi wakieleza aina ya tiketi na mechi wanazotaka kushuhudia.

Wambura alisema hakuna tiketi za fainali hizo zitakazoombwa FIFA bila kuwepo maombi kwa maandishi.

Alisema tiketi zilizopo kwa Tanzania ni za hatua ya makundi ukiondoa mechi ya ufunguzi, raundi ya 16 bora, robo fainali na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu, ambazo ziko 250.

Aliongeza kuwa kwa mechi ya ufunguzi, nusu fainali mbili na fainali, ni tiketi 10 tu ndizo zitakazopatikana na kuwa bei ziko katika viwango vitatu tofauti.

Mechi ya ufunguzi tiketi zake ni dola 495, dola 330 na 220 za Marekani, wakati hatua ya makundi bei ni dola 175, dola 135 na 90, huku hatua ya 16 bora ni dola 220, dola 165 na 110.

Robo fainali ni dola 330, dola 220 na 165, wakati nusu fainali ni dola 660, dola 440 na 275 huku mechi ya mshindi wa tatu ni dola 330, dola 220 na 165 ambapo fainali itakuwa dola 990, dola 660 na 440.

Wambura aliongeza kuwa watawasilisha maombi ya tiketi hizo FIFA kuanzia Desemba 8 hadi Februari 7 mwakani, kwani idadi ambayo itaombwa itatokana na Watanzania waliowasilisha maombi TFF.

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake