ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 19, 2013

‘Treni ya kisasa Dar kutatua tatizo la foleni’

Ni vyema viongozi wakatumia helikopta kwenye misafara yao badala ya kuliza ving’ora,”PICHA|MAKTABA

Dar es Salaam na Dodoma. Wakati Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia akiitaka Serikali kutangaza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam kuwa ni janga la kitaifa, Serikali hiyo imeshauriwa kununua treni ya kisasa itakayogharimu Dola za Marekani 6 milioni (Sh9.9 bilioni) ili kuboresha usafiri na kupunguza gharama za uendeshaji treni ya sasa.
Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR- Mageuzi, aliitaka Serikali kutangaza hali hiyo jana bungeni mjini Dodoma, wakati akichangia hoja kwenye taarifa ya Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu.
Katika hoja yake, Mbatia aliitaka Serikali kuchukua hatua za makusudi za kuondoa tatizo la msongamano huo, ikiwa ni pamoja na viongozi kutumia usafiri wa helikopta badala ya magari ambayo husababisha foleni kuwa kubwa zaidi.
“Msongamano huo unasababisha hasara ya Sh5 milioni kwa siku, ambapo ni sawa na Sh2 tilioni kwa mwaka. Ni vyema viongozi wakatumia helikopta kwenye misafara yao badala ya kuliza ving’ora,” alisema Mbatia.
Awali akiwasilisha taarifa Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Peter Serukamba alisisitiza uboreshwaji wa miundombinu kwa wakati ili kuwezesha maendeleo kupatikana katika nyanja za kiuchumi na kijamii kwa ujumla.
Treni za abiria:
Serukamba alisema changamoto inayokabili usafiri huo wa treni Jiji la Dar ss Salaam ni gharama za uendeshaji kuwa juu kulingasha na mapato yanayotokana na tozo la nauli kwa abiria.
“TRL inatumia injini za treni za safari ndefu, ambazo zinatumia mafuta mengi sana na wakati mwingine sehemu zenye muinuko mdogo tu hulazimika kutumia injini mbili kusukuma mabehewa” alisema.
Alisema Serikali imekuwa ikipoteza takribani Sh2 milioni kwa siku kama gharama za kuendesha treni hiyo na kusitiza kuwa tatizo la msongamano haliwezi kutatuliwa na treni moja, hivyo kuna haja kwa utaratibu wa kudumu ukaangaliwa.
Mwananchi

No comments: