Thursday, December 5, 2013

Urais wawaponza Lowassa,Sumaye

Mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na Edward Lowassa.
Vita ya urais wa mwaka 2015 imewaponza mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, baada ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mbeya kuwashtaki kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana.

Waliowashitaki Sumaye na Lowassa ni wajumbe wa Halmashauri ya CCM Wilaya ya Mbeya Vijijini ambao wamesema kuwa mawaziri hao wastaafu wamekuwa wakitoa kauli zinazokidhalilisha CCM na serikali yake.

Wamekitaka chama hicho kuchukua hatua za haraka ili kudhibiti kauli ambazo zinatolewa na viongozi hao wawili wastaafu kwa lengo la kulinda heshima ya CCM.


Katika kikao chao na Kinana, walimeleza kwamba wanasikitishwa na kauli za viongozi hao.

Wajumbe hao walimueleza Kinana kuwa hakuna jambo baya kama kuona viongozi ambao wamewahi kushika nafasi za ngazi za juu serikalini wakizungumza bila utaratibu na matokeo yake kuifanya jamii kutoelewa dhamira yao.

Akizungumza kwa niaba ya wajumbe hao wa Wilaya ya Mbeya Vijijini, kada mstaafu wa chama hicho, Mzee Patrick Inswira, alisema Sumaye amekuwa akisikika kila mara akikemea rushwa wakati alishindwa kufanya hivyo alipokuwa madarakani na matokeo yake anakidhalilisha chama hicho.

“Sumaye alikuwa madarakani kwa miaka 10 akiwa Waziri Mkuu, alikuwa wapi kukomesha rushwa?” Alihoji na kuongeza:

“Hili jambo Katibu Mkuu tunaomba tuseme tu baadhi yetu hatupendi maana ni kama viongozi wetu wameamua kukidhalilisha chama chetu.”

“Wakati yupo madarakani hakuwa akizungumzia athari za rushwa, leo ametoka kwenye nafasi hiyo amekuwa akipiga kelele hadi inakuwa kero kwa nchi kuona viongozi wastaafu wakipiga kelele badala ya kutafuta suluhisho,” alisema Inswira.

Kuhusu Lowassa , Inswira alisema kuwa kiongozi huyo amekuwa akizungumzia kushuka kwa elimu tena kwenye mikutano ya hadhara na kauli zake za vijana kukosa ajira.

“Unaposikia kiongozi ambaye amewahi kushika nafasi za juu serikalini anazungumza hadharani kuhusu kushuka kwa elimu yetu maana hatutakii mema kwa vijana wetu,” alisema.

"Hivi nchi nyingine zinaposikia kwamba elimu ya Tanzania imeshuka, nafasi ya vijana wetu kupata ajira nje ya nchi haitakuwapo, maana hakuna nchi ambayo itakuwa tayari kuchukua watu ambao hawana elimu,” alisema.

Alisema kuna viongozi ambao nao wamewahi kushika nafasi hizo za uwaziri mkuu, lakini wamekuwa kimya na kuhoji sababu za Sumaye na Lowassa kusikika kwenye vyombo vya habari wakitoa matamko na kauli ambazo hazina tija kwa CCM na serikali yake.

“Sijawahi kumsikia Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya, John Malecela na Salim Ahmed Salim, wakifanya vitendo ambavyo vinafanywa na mawaziri wakuu hao wastaafu,” alieleza.

Alisisitiza kuwa viongozi hao wanaposimama kujifanya wanazungumzia rushwa na elimu maana yake wanaifanya Tanzania kuwa na sifa mbaya jambo ambalo alidai si kweli na bado wanayo nafasi ya kuishauri Serikali kwa utaratibu unaoeleweka.

Aliushauri uongozi wa juu wa chama hicho kupitia Katibu Mkuu Kinana, kuchukua hatua dhidi ya viongozi wake wenye kuzungumza bila kufuata utaratibu.

Akizungumzia malalamiko hayo, Kinana aliwataka viongozi na wananchama kuwa na subira kwani suala hilo atalifikisha kwenye vikao vya juu.

Lowassa na Sumaye ni miongoni mwa makada wa CCm ambao wanatajwa kuwa wana nia ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Wengine wanaotajwa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; nNaibu Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia, January Makamba na Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, Dk. Asha-Rose Migiro.

Kuhusu wanachama na makada wanaotaka kugombea udiwani, ubunge na urais ambao wameanza kujipitisha kwa wananchi kuandaa mazingira ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Kinana watachukuliwa hatua kali ikiwamo ya kukata majina yao.

Alisema ni vema wenyeviti wa CCM katika wilaya zote nchini wakafuatilia wanachama wa aina hiyo na kwamba hata kama wana nguvu kiasi gani bado majina yao hawatarudi yakifika kwenye meza yake huku akisisitiza kuwa wanaotaka uongozi wasubiri wakati ukifika ambao ni Mei, 2015.

“Kama muda wa kugombea bado, ni marufuku kuanza kampeni za kuchafuana ndani ya chama, na kama ukibainika chama hakitakupa nafasi ya kugombea kwani unaonekana hautufai kwa kosa la kutokufuata sheria na kanuni za chama,” alisema Kinana.

Kinana aliamua kutoa tamko hilo baada ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi, kutoa taarifa kuwa kuna mpasuko katika chama hicho katika baadhi ya majimbo ya mkoa huo kutokana na kuwapo kwa watu wanaopita kuchafua hali ya hewa kwa sababu tu ya kutaka majimbo hayo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake