Ni wazi kwamba isingekuwa sawa. Bila vitabu vya Mungu wala mahubiri ya kiimani, bado kuchukua mume au mke wa mtu, lisingekuwa tendo zuri. Hii ina maana kuwa kuna mambo mengi yapo kimsingi zaidi, kuliko tu dhana ya makatazo kwa mujibu wa mafundisho ya kidini.
Hata bila serikali kula rushwa haliwezi kuwa jambo jema. Kutoa uhai wa mtu isingekubalika kwa namna yoyote ile hata kama Mungu kupitia vitabu vyake asingekataza. Mambo ambayo kwenye uso wa binadamu hayana sura nzuri, hayana kisingizio cha kujitetea.
Usaliti haukubaliki, unayumbisha nyumba nyingi, unaweka rehani ndoa na nyingi zimevunjika. Wapo wanaothubutu kutamka kuwa usaliti una nguvu sana. Katika makala haya, nitaonesha jinsi ambavyo tendo hilo lilivyo dhaifu na ukweli kuhusu Shetani wa usaliti.
Tafakuri katika kitu kinachodhihirisha ukweli; Mke wa mtu anatoka na mwanaume wa pembeni tofauti na mumewe. Kama mwanaume huyo angembaka kwa mara ya kwanza, bila shaka asingemuona ni mpenzi sahihi, angemchukulia ni mbakaji, mnyama.
Ipo siri inayojitosheleza katika usaliti kwamba hutimia kutokana na nguvu ya ushawishi. Lazima mmoja aanze mwingine ashawishike. Kuna wakati ingawa siyo mara kwa mara, hutokea wahusika wawili kushawishiana kwa ishara, hii tunaita kutegana.
Haitokei mara moja tu mtu kutembea na mke wa rafiki yake. Lazima kabla ya hapo kuwepo mwanzisha mwendo ambaye anaweza kufikisha ujumbe kwa kuzungumza au dalili za mitego dhidi ya mhusika. Kama hakutakuwa na vitu vinavyoweza kukemea hali hiyo, baadaye lazima ‘machafuko’ yatokee.
Msemo wa ukicheka na nyani utavuna mabua una mantiki kubwa hapa; Hutokea mwanamke kutoka na mwanaume ambaye mwanzoni hakumfikiria. Pengine alikuwa anamtumatuma kazi hapa na pale, awali alimchukulia kama mdogo wake au pengine mke wake.
Hulka za michezo isiyofaa na utani usio na maana, ukawafanya wawe karibu zaidi. Utani ukapamba moto wakawa wanataniana mpaka kwa kushikana na kusukumana. Safari moja huanzisha nyingine, hitimisho lake likawa wawili hao kufanya mapenzi, kinyume na matarajio ya awali.
Siyo rahisi kwa watu wenye kujitambua, mtu na shemeji yake wanaweza kuangukia kwenye dhambi ya mapenzi. Mume kwenda kutembea na mdogo au dada wa mke wake. Ukiona hilo limetokea, lazima pande zote zinazohusika ziwe kwenye lawama.
Mume na mke, dada au mdogo mtu, wote wana makosa. Watenda makosa, dhambi yao ni ukosefu wa aibu na kuamua kusaliti. Kosa la mke ni kucheka na nyani, mwisho akajikutana anavuna mabua. Nani ambaye hajaambiwa abiria chunga mzigo wako?
Mpaka kufikia hatua ya mume kutoka na shemeji yake, kabla kunakuwa na viashiria vingi vya hatari. Mathalan, mume anakuwa hodari wa kumtoa shemeji yake ‘out’, mke anaona hilo ni sawa na anachekelea. Imani yake eti wanaishi Kizungu.
Mke amelala, anamruhusu mume wake aende chumbani kwa dada yake (iwe mkubwa au mdogo), wanachozungumza huko hakijui. Baadaye anapokuja kubaini kwamba kati yao kuna uhusiano usiofaa, anabaki kulia kwa kusaga meno, majuto na masikitiko. Majuto ni mjukuu!
Yupo mwanamke ambaye mwanzoni alikuwa akimchukia mwanaume fulani. Walipoanza kuwa karibukaribu, historia ikabadilika. Pale huwezi kuthubutu kutamka kwamba kilichowafanya wawe wapenzi ni nguvu ya usaliti, isipokuwa ni udhaifu wa nyoyo zao.
Msomaji wangu Lauryin Joe (siyo jina lake halisi), alinisimulia kisa chake cha kutoka kimapenzi na kijana mpangaji mwenzake, mumewe akajua na kusababisha uhasama mkubwa. Anasema: “Mwanazoni sikuwa na wazo kabisa, nilijiamini mimi ni mwanamke imara katika ndoa yangu.
Itaendelea wiki ijayo Jumamosi
GPL
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake