Kuanzia saa 12 jioni, kidogo hali ikabadilika, upepo ukaanza kuvuma, mawingu yakajikusanya na baadaye ikaporomoka! Ilinyesha kwa hasira sana. Tangu ilipoanza kutikisa mabati ya nyumba za watu, saa mbili na dakika zake usiku, haijakatika mpaka muda huu.
Saa 7:45 usiku!
Ndani ya nyumba hii kubwa, mwanamke mrembo Vanessa alikuwa katika maumivu makali sana ya moyo. Pamoja na ukweli kwamba, mvua ile ilimtisha lakini haikuwa kwa kiasi kikubwa kama kumbukumbu juu ya mumewe mpenzi Harrison.
Kwa namna mvua ile ilivyokuwa ikipiga, mtu pekee ambaye angeweza kumpa furaha alikuwa ni mumewe mpenzi Harrison. Naam! Harisson alikuwa mwanaume wa pekee katika maisha yake.
Harrison siyo tu hakuwepo nyumbani kwake Sinza - Mori, jijini Dar es Salaam, hakuwepo Dar es Salaam kabisa. Hakuwepo nchini Tanzania. Harrison alikuwa jijini Mumbai, India kwa matibabu ya uvimbe uliokuwa tumboni mwake katika utumbo mpana.
Siku nzima iliisha bila kupata mawasiliano yoyote na mume wake mpenzi Harrison. Aliwasiliana naye kwa mara ya mwisho usiku wa kuamkia siku hiyo lakini tangu asubuhi hakuwasiliana naye na mpaka muda huo, saa nane kasoro za usiku, simu ya Harrison ilikuwa haipatikani.
“Ana nini mume wangu jamani?” akawaza Vanessa akijizidishia machungu moyoni mwake.
Aliinuka pale kitandani na kutembea taratibu hadi dirishani, akafunua pazia na kuyatupa macho yake nje. Maji yalikuwa yakipita kwa kasi sana pembeni mwa ukuta wa nyumba yao. Woga ukamwingia tena. Akafunga pazia haraka na kutoka tena taratibu hadi sebuleni.
Kulikuwa kimya kabisa. Vanessa hakuweza kupata usingizi usiku huo. Akatamani amgongee mlango msichana wake wa kazi aitwaye Anna ili wakae sebuleni wapige stori, lakini akaamua kuacha. Mvua ikazidi kunyesha kwa kasi.
Mara umeme ukakatika.
“Mungu wangu, hii mvua halafu na giza kutakuwa na usalama kweli?” akawaza Vanessa akizima kila kitu kinachotumia umeme pale sebuleni na kurudi zake chumbani.
Hapo sasa, hakuwa na sababu ya kuendelea kujipa mateso, akalazimisha usingizi kwa nguvu zake zote. Huku woga ukiwa umemjaa moyoni, taratibu usingizi ukamchukua!
Ilikuwa saa 9:18 usiku!
***
Kwa kumwangalia ilikuwa vigumu kujua kuwa Harrison alikuwa anaumwa. Alikuwa amevaa nguo zake nadhifu kabisa. Alivaa suruali ya jeans ya rangi ya bluu ya fulana nyeusi, chini alivaa raba nyeupe. Harrison alimwangalia mkewe kwa mara nyingine tena, akambusu.
“Ubaki salama mpenzi wangu,” alisema Harrison wakiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
“Ahsante dear, nakutakia safari njema na matibabu mema. Mungu akutangulie kwa kila kitu. Akulinde na upasuaji wako ufanyike salama, urudi salama mume wangu,” akasema Vanessa.
“Nashukuru sana mpenzi.”
Vanessa hakuweza kuvumilia, machozi yalikuwa yanamiminika machoni mwake. Harrison akamfuta kwa kiganja chake cha mkono.
“Nyamaza mama, halafu kumbuka sitaki watu wajue sana kuhusu hii safari, utasababisha waandishi wa habari watupige picha. Tulia, jipe moyo, nilitamani sana kuongozana na wewe mpenzi wangu lakini ndiyo hivyo tena...huwezi kumwacha Junior mwenyewe.”
“Najua dear, nalia kwa sababu ya mapenzi yangu kwako. Nakupenda sana mpenzi, nakupenda sana Harrison wangu. Baba Junior trust me, I love you darling!” akasema Vanessa, mvua ya machozi ikiendelea.
“Usilie mama, muda unazidi kwenda. Tafadhali naomba nikuache, nyie mrudi tu nyumbani sasa, nitakupigia nikifika Nairobi na baadaye kesho nikiwa Mumbai.”
“Okay darling, I love you so much my dear!” (Sawa laazizi, nakupenda sana mpenzi!)
“I love you too baby.” (Nakupenda pia mpenzi)
Harrison akataka kumwachia Vanessa, haikuwezekana. Aliendelea kumng’ang’ania pale kifuani mwake. Tayari abiria waliokuwa wakisafari kuelekea Mumbai walikuwa wakianza kukaguliwa tayari kwa safari.
“Kaka, time please. Nini maana ya kuwahi airpot?” alikuwa ni Brighton, mdogo wake na Harrison ambaye walikuwa wanaongozana pamoja kwenda India.
“Sawa, nakuja mdogo wangu.”
“Shem acha wivu bwana, inatosha sasa, mwache twende,” akasema Brighton akitabasamu.
“Upweke shemeji yangu.”
“Jitahidi basi tafadhali.”
“Sawa.”
Kweli, Vanessa alikubali kumwachia Harrison, akapiga hatua za haraka kuelekea kwenye foleni ya kuingia kwenye eneo la abiria wanaosafiri kwenda safari za kimataifa. Harrison aligeuka nyuma na kumpungia mke wake.
Tabasamu angavu lilichanua usoni mwa Vanessa, nuru ikamjaa na makunyanzi ya maumivu ya moyo, yakafutika kabisa usoni mwake. Harrison akafurahi sana kumwacha mkewe katika hali ile. Akaendelea na ukaguzi wakati akiingia kwenye chumba cha abiria wanaoondoka.
***
Asubuhi Vanessa aliamka akiwa mchovu sana. Ilikuwa tayari imeshafika saa mbili na dakika zake. Akajiinua kivivu na kukimbilia katika bafu lililokuwa mlemle chumbani mwake. Akajimwagia maji na kutoka sebuleni.
Alimkuta Anna akiendelea na shughuli zake kama kawaida.
“Shikamoo dada.”
“Marhaba mdogo wangu, vipi mtoto amekwenda shule?”
“Ndiyo.”
“Vipi, asubuhi mvua haikunyesha, maana jana ilikuwa balaa!”
“Ilikatika usiku uleule, lakini ilikuwa kubwa sana. Niliogopa sana kiukweli.”
“Sawa, mimi nipo chumbani, endelea na shughuli zako.”
“Nimekuelewa dada ila kwenye friji kuna vitu vimepungua.”
“Unajua vizuri cha kufanya mdogo wangu, hebu niandikie basi halafu utanipa ili baadaye ukachukue mahitaji yote.”
“Sawa dada.”
Familia hii ya Harrison Urassa ilikuwa na watu watano; baba, mama, mtoto wao wa kwanza wa kike aitwaye Latifa na kichanga Junior ambaye ndiyo kwanza alikuwa ametimiza mwezi mmoja na siku tatu tu. Mwingine alikuwa ni msichana wao wa kazi, Anna. Lati Green Garden Primary School ambayo ilifundisha kwa lugha ya Kiingereza.
Nini kimempata Harrison? Usikose kufuatilia wiki ijayo.
GPL
No comments:
Post a Comment