Advertisements

Tuesday, December 3, 2013

WAATHIRIKA WA VVU WILAYANI MAKETE WASUSA KUNYWA DAWA ZA ARV

Mkuu wa wilaya ya Makete Josephine Matiro akihutubia kwenye maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani katika kata ya Mbalatse wilaya ya Makete. 
Wakazi wa Mbalatse wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Makete akitoa hotuba yake.
Diwani wa kata ya Mbalatse Sikumu Msigwa akisoma Risala ya wanaoishi na VVU mbele ya mgeni rasmi.
Akimkabidhi mkuu wa wilaya hotuba yao.
 
Pamoja na jitihada za kuhakikisha kila pembe ya nchi hii dawa za kupunguza makali ya VVU zinapatikana kwa urahisi, kioja kimejitokeza wilayani Makete mkoani Njombe kwa baadhi ya wanaoishi na virusi vya ukimwi ambao walikuwa wanatumia dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo (ARV) kuacha kutumia dawa hizo kwa makusudi.
Pamoja na hayo wengine wanakataa kuzinywa dawa hizo licha ya kushauriwa na wataalamu wa afya kuanza kutumia kutokana na afya zao kuanza kuzorota

Hayo yamebainika katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yakliyoadhimishwa kiwilaya katika kata ya Mbalatse wilayani Makete mkoani Njombe.Akisoma risala ya wanaoishi na virusi vya UKIMWI katika kata ya Mbalatse, diwani wa kata hiyo Mh. Sikumu Msigwa amesema miongoni mwa mambo yanayosababisha kasi ya maambukizi mapya ya VVU katani hapo ni pamoja na mila potofu za kurithi wajane na wagane, wanaume kuoa wake wengi, ngono zembe, wenye vvu kukataa kutumia dawa za kupunguza makali ya virusi na kujiingiza katika ulevi wa kupindukia na kufanya ngono bila kondomu.

Akihutubia mamia ya wakazi wa Mbalatse waliofika kwenye maadhimisho hayo mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Makete Josephine Matiro amekemea vitendo vinavyochangia ongezeko la VVU ikiwemo kuwasihi waviu kutumia dawa za kupunguza makali ya VVU kama walivyoshauriwa na wataalamu wa afya ili waimarike afya zao na wazidi kujenga nguvu kazi ya Taifa.

Amesema endapo watatumia dawa hizo kwa usahihi upo uwezekano wa kuishi zaidi ya miaka 20 na wakaendelea kufanya shughuli zao kama kawaida, ikiwemo kuitunza familia ambayo inamtegemea kwa kiasi kikubwa.

"Ukitumia arv ndugu zangu lazima maisha yako yatakuwa marefu, na uzuri serikali yetu inawajali wananchi wake na dio maana hizo dawa zinafika mpaka huku, kwa kweli naombeni tubadilike, mkoa wetu ndio unaoongoza kitaifa, lakini bado jitihada tunatakiwa sisi ndio tuongeze, tukikubali kubadilika sisi, hata hizi kampeni za kupamban na VVU zitafanikiwa sana" alisema Matiro

Maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani huadhimishwa Desemba Mosi ya kila mwaka, ambapo mwaka huu kauli mbiu ilikuwa Tanzania bila maambukizi mapya ya VVU, na vifo vitokanavyo na UKIMWI inawezekana.
Habari na Edwin Moshi, Blobu ya jamii Makete.

No comments: