ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, December 4, 2013

Zanzibar `out`, Kili Stars vs Burundi kazi ipo leo


Wakati Kikosi cha Zanzibar Heroes jana kikitupwa nje kwenye michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea jijini hapa baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Kenya (Harambee Stars), leo ndugu zao Kilimanjaro Stars watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Burundi.

Kwa matokeo hayo ambayo wenyeji wa Kombe la Chalenji, Kenya wameyapata katika Uwanja wa Afraha, Nakuru uliopo umbali wa kilomita 200 kutoka jijini Nairobi, wameungana na Ethiopia kutinga hatua ya robo fainali huku Zanzibar Heroes sambamba na Sudani Kusini zikiaga kutoka Kundi A.

Allan Wanga aliifungia Kenya bao la pili la ushindi dakika ya 59 kwa shuti kali baada ya washambuliaji wa timu hiyo kugongeana pasi safi kabla ya mpira kumfikia mfungaji ambaye alifumua shuti hilo lililompita kipa Abdallah Rashid wa Zanzibar Heroes.

Kenya ilikwenda mapumziko ikiongoza kwa bao 1-0 lilofungwa kwa mkwaju wa penalti na mchezaji wa Azam FC, Joackins Atudo mwanzoni mwa mchezo.

Katika mchezo wa awali uliochezwa kwenye Uwanja wa huo wa Afraha, Ethiopia walikata tiketi ya kusonga mbele katika hatua ya robo fainali baada ya kuinyuka Sudan Kusini mabao 2-0. Mabao hayo yalifungwa na Yousuf Yassin dakika ya 54 na Baruk Kalbore.

Kilimanjaro Stars leo inatarajia kuivaa timu ya Taifa ya Burundi katika mechi ya mwisho ya Kundi B ya mashindano itakayofanyika kuanzia saa nane mchana mjini Nakuru.

Kilimanjaro Stars inashuka katika mchezo huu ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 iliyoupata dhidi ya Somalia wakati Burundi yenyewe ilichapwa 1-0 na mabingwa wa mwaka jana wa mashindano ya Afrika, Zambia (Chipolopolo).

Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen, alisema mechi hiyo itakuwa na upinzani mkali kwa sababu timu zote zinasaka ushindi ili kujihakikishia tiketi ya kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.

Poulsen alisema ameiona Burundi, hivyo amejiandaa kukabiliana na changamoto mbalimbali katika mchezo wao wa leo.

"Haitakuwa mechi rahisi, Burundi ina wachezaji wazuri na wanaocheza kwa kujuana. Ni timu iliyoko pamoja na inayocheza kwa kushambulia wakati wote, tuko tayari kupambana ili tupate pointi," alisema kocha huyo raia wa Denmark.

Mdenmark huyo aliongeza kuwa, timu yake imeanza kuimarika na anaamini leo wataonyesha kiwango cha juu kuliko mchezo uliopita ambao walionekana kuanza kutengeneza nafasi nyingi za kufunga.

"Sasa wachezaji wangu wamebadilika na nimewaambia wawe makini zaidi wanapokuwa na mpira, Burundi wanacheza kwa kasi na hawakai na mpira, naamini ujio wa Samatta (Mbwana) na Thomas Ulimwengu utakuwa umeongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji, tunatarajia matokeo mazuri na si jambo lingine," aliongeza.

Samatta na Ulimwengu hawakuwapo katika mechi mbili za kwanza kutokana na kuchelewa kujiunga na wenzao kufuatia timu yao ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuwa na mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho iliyofanyika Novemba 30 mwaka huu.

Kocha Msaidizi wa Burundi, Amaars Niyongabo, alisema wachezaji wake wako tayari kuikabili Kilimanjaro Stars na wana kiu ya kupata mafanikio mwaka huu.

Niyongapo alisema licha ya kuja na wachezaji wapya mwaka huu ambao atawatumia kwenye fainali za CHAN baadaye mwakani, hawataki kuona timu yao inashindwa kufika fainali.

"Mwaka jana tulitoka robo fainali, mwaka huu tunataka kusonga mbele zaidi, tuko na wachezaji wachanga na wazoefu ila tunawaamini watapambana na kuifunga Tanzania (Kilimanjaro Stars), aliongeza.

Mechi nyingine inayotarajiwa kuchezwa leo mjini Nakuru ni kati ya Somalia ambayo inaburuza mkia katika kundi dhidi ya Zambia wanaolingana pointi na idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa na Kilimanjaro Stars.

Timu mbili zitakazomaliza zikiwa juu kwenye kundi hili leo zitafuzu moja kwa moja hatua ya robo fainali ambayo itaanza kuchezwa Jumamosi Desemba 7, mjini Mombasa.

Kili Stars na Zambia, leo zinahitaji sare yoyote ama ushindi ili kuweza kusonga mbele, lakini Burundi kutinga kwake robo fainali kutatokana na ushindi tu, Somalia hata ikishinda haina nafasi ya kusonga mbele.
CHANZO: NIPASHE

No comments: