TUNAENDELEA kujifunza mbinu za kumsogeza mwenzi wako karibu. Tumeshaona mengi katika matoleo yaliyopita. Rafiki zangu, wakati mwingine majukumu ya kikazi husababisha wenzi au wanandoa wakaa mbalimbali.
Jambo hilo huwa changamoto kubwa sana kwa wengi, hushindwa kujua namna ya kuboresha uhusiano wao ili waweze kuendelea kuwa na uhusiano wenye nguvu. Katika matoleo yaliyopita tuliona jinsi mwanamke anavyoweza kufanya kwa mwanaume wake.
Niliishia pale ambapo mwanamke anaweza kumzawadia mwenzi wake ili kunogesha uhusiano. Nikasema katika zawadi hizo ambazo nilitaja zinazopendekezwa zaidi ni vyema kusindikiza na manukato mazuri ambayo unayatumia ili ahisi harufu yako.
Tuendelee kujifunza...
Maua...
Hii ni kati ya zawadi zinazopendekezwa na wataalamu wa mapenzi. Maua ni mazuri sana kwa mwenzi aliye mbali, lakini ni vyema kuzingatia na umbali aliopo, kwani maua huweza kusinyaa kabla ya kumfikia (hasa kama ukimtumia maua halisi, kwani ndiyo haswa mazuri zaidi).
Zingatia matakwa yake zaidi!
Hii ni njia pekee ya kuonesha ubunifu wako na jinsi unavyomjali hata akiwa mbali kwa kumtumia vitu ambavyo huwa anavipenda lakini alipo hawezi kuvipata! Mathalani, anapenda sana zabibu, lakini amekwenda mkoa ambao zao hilo halipo, hii ni nafasi yako kumtumia.
Mathalani unajua kabisa anapenda sana kusoma vitabu, lakini sehemu aliyopo hawezi kupata, basi nunua majarida, magazeti na matoleo yote ambayo hajayapata kisha mtumie, hakika utakuwa umemfurahisha sana na kumfanya afurahi kupata vitu hivyo.
UAMINIFU NI NGUZO!
Ukitaka kufurahia mapenzi, lazima usiwe msaliti. Upo msemo usemao, ukimsaliti mpenzi wako ujue nawe utasalitiwa, sasa ili uepukane na hilo ni vyema ukajiwekea dhana ya uaminifu wewe kama wewe kwanza.
Jichunge mwenyewe, usikubali kabisa kuharibu thamani yako kwa kumruhusu mtu mwingine aujue mwili wako (kwa wanaume na wanawake).
Kumbuka kwamba mwili wako ni kwa ajili ya mpenzi wako pekee, endelea na dhana hiyo siku zote, utafurahi!
Hutaona faida yake kwa haraka lakini fikiria hili kwa makini, kama wewe umeamua kuwa mwaminifu kwa mwenzi wako kwa kutambua thamani yake, kwa nini Mungu asikulindie huko alipo?
Lakini lazima ufahamu jambo moja; Mungu anaweza kukulindia mwenzi wako ikiwa naye anakupenda kwa dhati na ana nia ya kuishi na wewe hapo baadaye.
Hata hivyo, kama mwenzi wako ni tapeli, Mungu atakuonyesha, ukweli utakuwa wazi na utajua kitu cha kufanya. Achana na usaliti na huo utakuwa mwanzo wa kuelekea kwenye kuujua ukweli.
MWAMINI
Hili halikinzani sana na kipengele kilichopita, baada ya kuhakikisha kwamba humsaliti, sasa ni wakati wako wa kuhakikisha kwamba unamwamini katika kiwango cha mwisho. Usimwoneshe mashaka sana na nyendo zake. Wakati mwingine unaweza kumpigia simu asipokee, hilo lisikupe shida!
Kuna baadhi ya watu, akimpigia simu mpenzi wake akiona hajapokea, tayari hisia zake zinakuwa mbali na muda huo huo anamwandikia meseji mbaya za ukali na kumtuhumu kwamba anajua wazi kwamba yupo mahali anamsaliti!
Acha. Huna haja ya kufanya hivyo, onyesha kumwamini.
Kama umempigia na simu yake haipatikani, ni wakati wako wa kumwandikia ujumbe na kumpa pole kwa kazi kutokana na kutambua kwako kwamba muda huo alikuwa bize na majukuu yake.
Rafiki zangu, nafasi yangu ni finyu, wiki ijayo nitakuwa hapa katika sehemu ya mwisho ya mada hii, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vitatu; True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani
No comments:
Post a Comment