Tuesday, January 14, 2014

KCC BINGWA KOMBE LA MAPINDUZI

Utabiri wa kocha mpya wa Simba, Zdravko Logarusic kwamba timu itakayotangulia kufunga goli katika mechi ya fainali ya Kombe la Mapinduzi ndiyo itakayotwaa ubingwa ulitimia wakati Wekundu wa Msimbazi walipolala kwa bao 1-0 dhidi ya KCC ya Uganda katika mechi ya kuhitimisha michuano hiyo kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa jana.

Simba ilikuwa haijaruhusu bao katika michuano hiyo, lakini goli pekee walilofungwa mapema katika dakika ya 20 kutoka kwa Herman Waswa aliyeunganisha krosi ya winga Tony Odur, lilitosha kuzima ndoto zao za kulibakisha kombe nchini. Lilikuwa pia ni bao la tatu la Waswa katika michuano hiyo.

Bao hilo lilivunja rekodi zote za Simba, ikiwamo ya Simba kutopoteza mechi msimu huu, ya kocha Loga kutopoteza pambano tangu akabidhiwe kuifundisha klabu hiyo ya Msimbazi baada ya kumtimua Abdallah 'King' Kibadeni na ya kipa Ivo Mapunda ya kutoruhusu mabao.

Hata hivyo, Ivo alitwaa tuzo ya Kipa Bora baada ya kuruhusu goli hilo moja tu katika mechi tano alizocheza na kuzawadiwa Sh.300,000 kutoka kwa waandaaji Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hakucheza mechi moja tu dhidi ya KMKM ambayo langoni alisimama Mghana Yaw Berko.

Owen Kasule wa URA ya Uganda aliibuka kuwa Mfungaji Bora baada ya kutupia magoli manne katika mechi alicheza mechi tano alizocheza, ingawa ya tano alitolewa kwa kadi nyekundu wakati walipolala 2-0 dhidi ya Simba katika nusu. Pia alizawadiwa Sh.300,000 na 'music system'.

Tuzo ya Mchezaji Bora wa Michuano ilikwenda kwa Mwinyi Mngwali wa Clove Stars (Combine ya Pemba) ambayo ilitolewa na Azam FC katika robo fainali, ambaye alizawadiwa Sh. 300,000 na 'music system'.

Baada ya mechi hiyo ambayo ni kwa ajili ya kuhitimisha sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar, kocha Loga wa Simba alikataa kuzungumza chochote. "No comment," alisema kwa ufupi kocha huyo Mcroatia wakati kocha msaidizi Selemani Matole alisema wameyakubali matokeo na sasa wanaweka nguvu katika michuano ijayo ya Ligi Kuu ya Bara.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake