Msimamo huo ulitangazwa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, akieleza kuwa ni maamuzi yaliyofikiwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho iliyokutana mwishoni mwa wiki mjini Dodoma.
Uamuzi huu unakuwa ni mwanzo wa safari ngumu na itakayohitaji ushawishi mkubwa ndani ya Bunge hilo ili mfumo wa serikali mbili ukubalike hasa kutokana na upande wa Zanzibar kuwa na msimamo thabiti wa kutaka kupata mamlaka makubwa zaidi ndani ya mfumo wa Muungano.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, uamuzi wowote kupitisha katiba hiyo utatakiwa kuungwa mkono na walau theluthi mbili ya wajumbe wa Bunge hilo kutoka kila upande.
Suala la muundo wa Muungano limekuwa nyeti na tete kwa miaka mingi ya uhai wa muungano tangu kuasisiwa kwake mwaka Aprili 26, 1964, huku zikiundwa tume na vyombo mbalimbali vya kushughulikia kile kilichpachikwa jina la kero za muungano, lakini kero hizo zingalipo hadi leo miaka 50 ya Muungano huo.
Kwa upande wa Bara, CCM inaonekana wazi kuwa haitapata kazi kubwa kupata theluthi mbili ya wajumbe wa Bunge hilo kutokana na ukweli kuwa ina wabunge wengi.
Hali ni tofauti kwa upande wa Zanzibar kwani mara kadhaa wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka kisiwani humo huonekana kuwa na msimamo moja bila kujali itikadi za vyama vyao suala la Zanzibar linapokadiliwa.
Kwa ujumla, idadi ya wajumbe wanaotoka katika Baraza la Wawakilishi wanapaswa kuwa 82, hiyo ikiwa ni wawakilishi 50 wa majimbo pamoja na nafasi 10 za wawakilishi wa kuteuliwa na rais, viti maalum 20, spika na mwanasheria mkuu wa serikali.
Aidha, wapo wabunge wa Zanzibar 83 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kati yao ni 35 kutoka Chama cha Wananchi (CUF).
Katika wajumbe 201 wa Bunge la Katiba wa kuteuliwa na Rais, 67 wanatoka Zanzibar. Ingawa ni vigumu kujua itikadi ya kila mmoja, kwa ujumla siasa za Zanzibar zimegawanyika kwa mstari ulio dhahiri miongoni mwa chama tawala na upinzani wakigawana nafasi sawa katika maeneo mengi. Vyama vinavyoshindana Zanzibar ni CCM na CUF ambacho ni chama kikuu cha upinzani kisiwani humo tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.
Ukweli unadhihirishwa na chaguzi kuu nne zilizopita mwaka 1995, 2000, 2005 na 2010 CCM na CUF wakipishana kwa asilimia ndogo sana. Mwaka 2010 walilazimika kuunda serikali ua umoja wa kitaifa.
Mgawanyo huu wa wajumbe watokao Zanzibar ndiyo utakaoipa kazi kubwa CCM katika kushawishi hoja yake ya serikali mbili ipate uungwaji mkono wa theluthi mbili kwani kwa mujibu wa sera za CUF, muundo wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unapaswa kuwa wa serikali tatu; kwa maana ya Bara, Zanzibar na Jamhuri yenyewe.
Katika mkutano na waandishi wa habari jana, Nape alisisitiza kuwa CCM inasimamia mfumo wa Muungano wa serikali mbili, ambazo zitakuwa zimefanyiwa marekebisho kuliko ilivyo sasa ili kukidhi changamoto za sasa za muundo wa Muungano.
Nape alisema kuwa katika kikao hicho, wajumbe wa Nec walijadili kwa kina rasimu ya katiba mpya kwa kupitia kifungu kwa kifungu na kutoa msimamo wao ili Watanzania wajue.
Nnaye alisema kuwa Watanzania wakumbuke kuwa mwaka huu yanafanyika maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano na kwamba kuna changamoto ambazo ziliainishwa na kuibuliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, watu na taasisi nyingine akisema zote Nec imezitafakari.
“Kuna baadhi ya marekebisho ambayo zile changamoto zote tumezitafakari na ndiyo ambazo zilichukua muda mrefu kujadiliwa, tumeona jibu lake siyo serikali tatu, jibu lake ni kufanya marekebisho katika serikali mbili tulizonazo,” alisema Nape na kuongeza:
“Sisi ni waumini wa serikali mbili zilizofanyiwa maboresho na siyo serikali za awali ambazo zilikuwa na changamoto. Tumejiridhisha tukifanya hivyo tutajibu zile hoja zilizokuwa na zitakazoibuliwa,” alisema Nape.
Alipoulizwa iwapo ikitokea mfumo wa serikali ukashindikana na kupitishwa wa serikali tatu Chama hicho kimejipangaje? Nnauye alisema:
“Sitaki kuwa Sheikh Yahya (marehemu Sheikh Yahya Hussein) kutabiri kitakachotokea, tusubiri itokee tuvuke daraja tunapolifikia, lakini Chama kimekuwa wazi tangu mwanzo kuwa kitaunga mkono katiba itakayoungwa mkono na Watanzania.”
Jana wabunge wa CCM walifanya kikao cha kuwekana sawa chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete tangu ssa tano hadi 12 jioni na kutoka na msimamo wa muundo wa Muungano wa serikali mbili.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa baada ya mjadala mrefu, wajumbe waliafikiana kwenda katika bunge la Katiba na masimamo huo.
Hata hivyo, vyanzo vyetu vilieleza kuwa walikubaliana kuwa ikitokea kundi kubwa la wajumbe wa bunge hilo kupendekeza serikali tatu, wataunga mkono.
MAMBO YA MUUNGANO
Kwa mujibu wa Ibara ya 63 ya rasimu mpya ya katiba mambo ya Muungano yatabaki kuwa,Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Uraia na Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyma vya Siasa na Ushuru wa Bidhaa na Mambo yasiyo ya Kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano.
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
CCM huu sio wakati wake acheni kuiburuza ZANZIBAR. Yaani mmekaa kutetea mambo ambayo hayana msingi kwani katiba inatengenezwa ya nini sasa kulinda CCM au kwa manufaa wa waTanzania!!/
Post a Comment