ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 18, 2014

Marejeo ya magazeti – Serikali sasa yaweka sheria: Marufuku kufanya biashara na Afrika Kusini


Dar es Salaam, Jumatatu.

Serikali ya Tanganyika imevunja uhusiano wa namna yeyote wa kibiashara kati yake na serikali ya Afrika Kusini kuanzia tarehe mosi Octoba.

Hivyo basi wafanyabiashara na wenye mitambo wanaonywa kwamba kupeleka bidhaa au kupokea bidhaa kutoka Afrika Kusini, au usafirishaji wa bidhaa ambazo mwisho zitafika Afrika Kusini ni mwiko.

Taarifa ya serikali iliyotolewa leo inasema kwamba tarehe mosi Octoba Jamhuri ya Tanganyika inakata
kabisa uhusiano wa biashara na nchi hiyo.

Tumepima kwa makini:

Kukomesha biashara na Afrika Kusini kunatokana na siasa ya Tanganyika juu ya uhusiano na Afrika kusini. Taarifa hiyo inaendelea kusema kwamba baada ya kufikiria kwa makini matokeo ya uchumi wa Tanganyika kutokana na kuvunja biashara na nchi hiyo, amri hiyo imetolewa.

Matangazo ya sheria katika gazeti la serikali ya Tanganyika na ile ya ushirikiano wa Afrika ya Mashariki (EASCO) juu ya suala hili yatatolewa siku ya ijumaa tarehe 4 Octoba mwaka huu.

Mwandishi wetu wa siasa anadokeza kwamba tangazo hili la kuvunja uhusiano wa namna yeyote na makaburu linathibitisha nia ya serikali kwamba uchumi au fedha haviwezi kuingilia kati wakati wa kupigania jambo la muhimu.

Isitoshe kuvunja uhusiano huu kunaondoa yale mawazo kwamba si kweli kukataa uhusiano wa kiserikali na huku nyuma watu wanahusiana katika mambo mengine.

Hivi sasa waziri wa Mambo ya Ndani Bw. Kambona yuko mjini New York kuongoza ujumbe wa Tanganyika katika Baraza la Umoja wa Mataifa na bila shaka jambo moja atakalo shikilia ni kumtoa Mkaburu kwenye Baraza hilo.

Chanzo: Gazeti la Mwafrika
Tarehe: Oktoba, 1 1963
Na: 1082
Bei : Senti 10.
---
Shukurani ya marejeo haya  ya magazeti ya zamani zimwendee Ado Shaibu

No comments: