MPENZI msomaji, Kwa nini ujute baadaye? Hicho ndiyo kichwa cha makala haya niliyoyaanza wiki mbili zilizopita, ni vizuri ukaendelea kufuatilia hadi mwisho ili upate somo la kuboresha uhusiano wa kimapenzi na uliyenaye. Endelea kutiririka...
Hapendi ziara za usiku zisizo na faida wala tija. Mnazungumza leo, kesho unarejea yaleyale. Siku zinapita anakusamehe lakini hujirekebishi. Hii ni dunia, anapokutana na mtu ambaye anamuonesha kwamba hatakuwa na shughuli nyingi za usiku, lazima atamkimbilia.
Shika kile kinachomfaa mwenzi wako, nafasi ya kuhakikisha utamu wa mapenzi ambao mnauogelea sasa ni yako mwenyewe. Yakipaliliwa, kuwekewa mbole na kumwagiliwa, lazima yatamea na kustawi. Yakitazamwa bila matunzo yoyote husinyaa.
Ikitokea unapanda mbegu wakati zinaanza kuchipua wewe lile shamba unaligeuza uwanja wa kuchezea mpira, unakanyagakanyaga, ile mimea itakufa, kwa hiyo na ile mbegu nzuri ambayo uliipanda nayo itapotea. Huo ndiyo mfano halisi wa mapenzi.
Ina maana kuwa pengine unaweza kuanza vizuri sana katika uhusiano wako, kile ambacho ulikiingiza kwa mwenzi wako ni mbegu nzuri sana. Ulipofika muda wa kuweka mbolea na kufanya umwagiliaji ili kile kilichopandwa kichipue na kustawi, mambo yanageuka kabisa.
Vitendo vyako vinakuwa sawa na yule anayekanyagakanyaga shamba lake aliyelilima na kupanda mbegu iliyo bora. Usifanye hivyo, maana kila kibaya unachomtendea mwenzi wako leo, tambua kinamuumiza sana. Kuna faida gani kwako kumfanya mwenzi wako ateseke?
Je, mateso yake wewe yanakupa ahueni ipi? Kwa walio kwenye mapenzi ya dhati ni kwamba mwenzi wako anapoteseka, na wewe pia unakuwa kwenye mateso makali. Maana furaha yake ni yako, maumivu yake yanakugusa pia. Vivyo hivyo kilichopo kwako naye kinamhusu kwa tafsiri pana.
Juu ya hapo ni kuwa hisia za maumivu katika mapenzi zina kawaida ya kuhama kutoka upande mmoja kwenda mwingine. Unamtesa sana, siku akichukua uamuzi wa kusema “mwana kwenu kwa heri”, hapo ndipo unashtuka, eti huamini kinachotokea.
Maombi ya msamaha kutoka kwako kwenda kwake yanakuwa kwa unyenyekevu wa hali ya juu sana. Kwa nini mfike huko? Akili yako itumikishe kufanya uamuzi sahihi ambao ni kumtunza mwenzi wako ambaye anakutunza hivi sasa. Maudhi ya hapa na pale jiepushe nayo.
Mdharau mwiba guu huota tende! Usione anachokilalamikia mwenzi wako ni kidogo, mfanye afurahie uwepo wako kila siku. Usimruhusu akulilie, maana ipo siku utalia wewe. Hakikisha hatoi machozi ya maumivu, isipokuwa yawe ya furaha. Kinyume chake kuna siku yatakugeuka.
SOMA KWA MFANO
Kuna uhusiano wa Hawa na Matali, vilevile Gaudensia na Reina. Kila mmoja una soma lake. Hawa alimchezea sana Matali ambaye alipoona yamezidi aliondoka. Reina naye alijiona kidume, akamtenda sana Gaudensia aliyeona mazito, akatimka. Baadaye kila mtenda alilia kwa kusaga meno.
Itaendelea wiki ijayo.
GPL
No comments:
Post a Comment