ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 27, 2014

Maalim Seif awasha moto Zanzibar

Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ametangaza kuwa njia pekee ya kunusuru Muungano ni kuuundwa kwa kwa serikali ya mkataba ambayo itaifanya Zanzibar iwe na mamlaka kamili na kuapa kuwa Wazanzibari hawatorudi nyuma katika madai hayo.

Maalim Seif alitoa kauli hiyo jana jioni wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa chama hicho katika viwanja vya Demokrasia Kibanda Maiti na kusema kuwa hakutegemea kama Rais wa jamhuri ya Muungano, Dk. Jakaya Kikwete, angeonyesha msimamo wa chama chake-CCM wakati akizindua Bunge Maalum la Katiba la Ijumaa iliyopita.


Maalim Seif alisema katika mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa Kamati ya Maridhiano kuwa Zanzibar inahitaji mamlaka yake kamili na kwamba Tanganyika pia ifufuliwe.

Alisema kwa kufanya hivyo, baadhi ya kasoro zilizoko katika Muungano huo zitarekebika na kuunda Muungano mpya wa ushirikiano kwa mkataba maalum.

Huku akishangiliwa na wananchi katika mkutano huo, Maalim Seif alikosoa mwenendo wa CCM na Rais Kikwete katika kushughulikia malalmiko ya muda mrefu kutoka zanzibar bila kujali matakwa ambayo Wazanzibari wamekuwa wakiyataja katika kipindi cha miaka 50 ya Muungano huo.

Hata hivyo, aliipongeza iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba kwa kuhakikisha inaingiza mapendekezo ya muundo wa serikali tatu katika rasimu.

Alisema ikiwa Bunge Maalum la katiba litapitisha muundo wa serikali mbili hawatakubaliana nayo.

Alisema baadhi ya Watanzania aikiwemo Rais Kikwete hawajapendezewa na marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar yaliofanyika katika uongozi wa awamu ya sita ya Dk. Amani Abeid Karume.

Alisema marekebisho ya katiba hiyo yanasema Zanzibar ni nchi ambayo inaweza kujiendesha wenyewe kutokana na rasilimali zilizopo.

Alisema suala la kuwapo kwa serikali tatu haliwezi kukwepeka na kwamba Wazanzibari wataendelea kutetea Muungano wa mkataba.

“Mimi nasema Zanzibar kwanza na siyo Tanzania kwanza kama alivyosema Rais Kikwete, mimi nahisi angesema Tanganyika kwanza,” alisema Maalim Seif.

Mjumbe wa Mamati ya Maridhiano Zanzibar Mansor Yussuf Himid, alishauri kuwa Wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba wanaotoka katika vyama vya upinzani wafunge virago vyao na kurudi kwa sababu ya mizengwe inayoendelea bungeni na kusisitiza nyia pekee ni mkataba.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: