TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAREHE 07.04.2014
CCM MKOA WA SHINYANGA YA LAANI KAULI YA
MBUNGE WA JIMBO LA KAHAMA JAMES LEMBELI
KUWA “CCM SIYO MAMA YANGU”
Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga
KIMELAANI vikali kauli ya Mbunge James Lembeli Mbunge wa Jimbo la
Kahama aliyoitoa kwenye vyombo ya habari hivi karibuni iliyosema “CCM
SIYO MAMA YANGU”.
Kwa hiyo Chama cha Mapinduzi Mkoa wa
Shinyanga na wana CCM wote kwa ujumla wamestushwa na kauli ya Mbunge
Lembeli anayetokana na CCM kwani kauli hii hatukutegemea sote kama
ingeweza kutolewa na Mwanachama ambaye tena ni Kiongozi ndani ya Chama.
Tunaomba ieleweke na tunautaarifu
Umma na wana CCM wote kuwa CCM haina tatizo kabisa na msimamo wa Mbunge
James Lembeli kuhusu msimamo wake wa serikali moja, mbili, tatu au nne
na hata serikali ya Tanganyika kwani huo ni uhuru wake binafsi. Tatizo
letu kubwa kwake ni kauli aliyoitoa kuwa “CCM SIYO MAMA YANGU” kwani
kauli hiyo ameitoa sio mahali pake na haihusiki na utashi wake binafsi
katika msimamo alionao katika BUNGE LA KATIBA. Kauli hii inaukakasi na
ni sawa na kukinajisi Chama.
Lakini jambo la ajabu na la
kushangaza ni kuhusu kulitumia jina la Baba wa Taifa Mwl. J. K. Nyerere
vibaya, amekuwa akijifananisha na kauli ya Baba wa Taifa tungependa
atambue kuwa Lembeli hana hadhi na sifa ya kujifananisha na Baba wa
Taifa; kwani kujifafanisha kwake na Baba wa Taifa huko ni matumizi
mabaya ya kujitwisha sifa asizostahiki kwani Baba wa Taifa Mwl. J. K.
Nyerere alikuwa na karama, hekima na busara kubwa za pekee na
aliheshimika Dunia kote pia alikuwa anatoa kauli zake kutokana na
mazingira yaliyokuwepo wakati huo.
Kwani Baba wa Taifa kila jambo
lililokuwa linahusu swala la Chama na Mstakabali wa Taifa alitumia vikao
kulizungumza sio anavyofanya Lembeli kuropoka ovyo, kutumia ubabe na
kukosa staha kwa Chama.
Tabia ya Mbunge Lembeli ya
kukidhihaki Chama imekuwa ikijitokeza mara kwa mara, lakini tunapenda
atambue na kumkumbusha kuwa Lembeli hapo alipofika na jeuri yote na
umaarufu alionao unatokana na CCM, kabla ya mwaka 2005 hakuna Mtanzania
aliyemfahamu popote nchini.
Lakini baada ya kupewa ridhaa na CCM
na hatimaye kuchaguliwa Ubunge ndipo akajenga umaarufu uliotokana na
CCM. Lakini jingine tunapenda kumkumbusha kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2010 Lembeli alikuwa na wakati mgumu sana ndani ya Chama na nje ya Chama
lakini Chama na Wanachama wakampigania kwa hali ya juu sana na kwa
mazingira magumu na hatimaye ushindi ukapatikana.
Leo shukrani anazotoa kwa Chama ni kukiambia CCM SIO MAMA YAKE.
Basi na kama Lembeli anaona CCM SIO
MAMA YAKE ni vyema akatueleza MAMA YAKE NI NANI – KISIASA na kama ana
MAMA MWINGINE KISIASA ni VYEMA AKAMFUATA HUYO MAMA HUKO ALIKO anayeona
atamfaa kumpa umaarufu zaidi ya CCM.
Mwisho CCM Mkoa wa Shinyanga
hakitakuwa tayari na hakitawavumilia wanachama na viongozi wake wenye
tabia kama ya Lembeli ya kuendelea kukidhalilisha Chama hadharani.
Lakini pia Chama kitaendelea
kuheshimu Demokrasia ndani ya Chama na Uhuru wa mawazo unaofuata
maadili, miiko na taratibu za Chama ndani ya vikao.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Taarifa hii imeandaliwa na Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga na imesomwa na:-
Ndugu Emmanuel S. Mlimandago
Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM
Mkoa wa Shinyanga
CHANZO: MALUNDE1.
05.04.2014
1 comment:
Sasa CCM waanze kujifunza kwamba msimamo wa chama si msimamo wa kila mwanachama. Huku US magavana, masenata, na macongress wanamkimbia Obama kutokana na regional politics hata hawakutani nae wakati akitembelea jimbo kwani atawachafulia na kupoteza kiti. Mwisho wa siasa za kinafiki bongo unawadia na CCM wakizidi kudharau wabunge wao watajutia. Kukomaa kisiasa sio kukubaliana na kila kitu au tuseme msimamo wa chama. Hii inatafsiri kwenye libeneke la kura za siri au za wazi katika katiba. Wajumbe wanaogopa kutoa misimamo yao kwani watatoswa kisiasa na vyama vyao. Kama kweli demokrasia ya kweli ingekuwepo bila ya wajumbe au wanasiasa kuogopa kutoswa na vyama vyao kura ya wazi ingekuwa ni jawabu na wnanchi ndio wangeamua nani awaongoze na sio chama.
Post a Comment