ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, April 12, 2014

TAIFA STAR YA KESHO KAMBINI TUKUYU JE MAFANIKIO YATAFIKIWA KUTOKA KWENYE TIMU HII YA VIJANA WACHANGA?

By SOSTHENES NYONI 

Ukweli ni kwamba, kambi hiyo yenye jumla ya wachezaji 33 walioibuliwa kupitia mpango maalum wa kung’amua wachezaji wenye vipaji kwa ajili ya kuiboresha Taifa Stars inaendeshwa kitaalam na imewekwa mahali sahihi.
YEYOTE aliyefika kwenye kambi ya Taifa Stars iliyoko Tukuyu kwenye Makao Makuu ya Wilaya ya Rungwe, Mbeya atakiri kuna kila dalili njema za mafanikio ya soka la Tanzania.
Ukweli ni kwamba, kambi hiyo yenye jumla ya wachezaji 33 walioibuliwa kupitia mpango maalum wa kung’amua wachezaji wenye vipaji kwa ajili ya kuiboresha Taifa Stars inaendeshwa kitaalam na imewekwa mahali sahihi.
Kwa kuwa, Watanzania wengi wanapenda kujua undani wa timu hiyo, hivi karibuni Mwanaspoti lilisafiri hadi Tukuyu na kujionea jinsi kambi hiyo iliyopo kwenye Hoteli ya Land Mark inavyoendeshwa.
Ratiba ya mazoezi
Timu hiyo inafanya mazoezi mara mbili kwa siku, yaani asubuhi na jioni kwenye Uwanja wa Chuo cha Ualimu Tukuyu na siku zilizopangwa ni kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi, Jumapili ni siku ya mapumziko.
Mazoezi ya timu hiyo huanza saa 1:00 asubuhi hadi saa 3:00 asubuhi, lakini kabla ya mazoezi bendera ya taifa hupandishwa sambamba na wachezaji na viongozi kuimba wimbo wa taifa.
Baada ya mazoezi kumalizika, timu hurejea kambini ambako wachezaji na viongozi hupata kifungua kinywa na muda uliotengwa ni saa moja.
Baada ya kunywa chai, wachezaji hupewa muda wa kupumzika katika vyumba vyao huku wakisubiri chakula cha mchana saa 7:00.
Baada ya chakula cha mchana wachezaji hupewa tena muda wa kupumzika hadi ya saa 9:00 Alasiri ambapo hupewa chai kisha 9:30 hurudi mazoezini yanayoanza saa 10:00 jioni na kumalizika saa 12:OO.
Baada ya mazoezi, bendera ya taifa huteremshwa, kisha timu hurejea kambini, saa 1:30 usiku wachezaji hula chakula cha usiku kisha hupewa muda wa kupumzika hadi saa 3:0O usiku ambapo wote hutakiwa kuwepo vyumbani mwao.
Kifungua kinywa
Katika kifungua kinywa, wachezaji hao huchagua kati ya chai ya rangi na ya maziwa, supu ya samaki na viazi mviringo, mayai ya kukaanga na kuchemsha, chapati, mihogo, viazi vitamu na juisi ya tikiti maji.Chakula cha mchana
Mlo huo hujumuisha ugali, wali na ndizi, huku mboga zikiwa ni nyama, kuku wa kienyeji na mboga za majani ambapo mchezaji ataamua kulingana na kile anachopenda kula.
Chakula cha usiku
Hapa utayakuta makaroni, wali, ugali, ndizi na juisi ambacho ni kinywaji cha kawaida katika mlo wowote wa timu hii, mboga ni pamoja na samaki, kuku wa kienyeji pamoja na mbogamboga.
Meneja wa Taifa Stars, Boniface Clemence amesema chakula huwa kinabadilika kulingana na programu ya kocha kwa siku husika.
“Suala la chakula si la hiari, kila mchezaji ni lazima ale isipokuwa tu kama kutakuwa na maagizo ya daktari wa timu.
“Pia, tunasisitiza umuhimu wa kuheshimu ratiba, muda wa kula ni kula wa mazoezi ni mazoezi na kulala ni kulala,”alisema meneja huyo.
Miongozo ya kambi
Ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa na malengo yanafikiwa, wachezaji wamepewa miongozo au taratibu 10 wanazopaswa kuzitii na anayekiuka anachukuliwa hatua za kinidhamu.
Baadhi ya taratibu hizo ni kila mchezaji kutakiwa kuimba wimba wa taifa kabla ya mazoezi ya asubuhi na jioni, kuzingatia muda wa chakula, kutotumia aina yetote ya kilevi na marufuku kuingiza mgeni hotelini.
Pia, unyoaji wa nywele usio na staha umepigwa marufuku katika kambi ya timu hiyo.
“Tunafahamu kwamba kipaji pekee hakitoshi bila nidhamu na kwa kuzingatia hilo tumeweka miongozo 10 ambayo kila mchezaji anatakiwa kuifuata na tumeibandika kwenye vyumba vyote vya wachezaji,” aliongeza Clemence aliyewahi kuwa mhasibu wa Yanga enzi za uongozi wa Francis Kifukwe.Kocha wa Mkuu wa Taifa Stars (wa muda), Donald Koroso ‘Dan Koroso’ amezungumzia kiufundi maendeleo ya timu hiyo.
“Tulianza kambi yetu Machi 22, mwaka huu na na programu yangu ya kwanza imetimia, wiki mbili ilikuwa ni kujenga stamina na pumzi kwa wachezaji.
“Programu ya pili imeegemea kwenye mambo ya kiufundi zaidi, nadhani umeona muda mwingi tumetumia kuchezea mpira na hakika wachezaji wangu wamebadilika sana na inatia moyo,” alisema Koroso ambaye amewahi kuifundisha Ushirika ya Moshi na Simba ya jijini Dar kabla ya kwenda Botswana.
“Tulipoanza ilikuwa tabu kidogo, wachezaji waliona mazoezi ni magumu, kuna kipa(hamkumbuki jina)kutoka Kagera aliondoka, ajabu Wazanzibar ambao wengi hudhani ni legelege hakuna aliyekimbia na wanafanya vizuri,” alisema Koroso.
Koroso aliongeza :”Lengo ni kuwachuja ili wabaki 15 ambao wataungana na 15 wa timu ya zamani na kuunda timu itakayocheza dhidi ya Burundi.
“Baada ya mchujo watakaobaki hawatatupwa watapelekwa timu ya vijana kwavile wengi wa wachezaji walioko hapa ni vijana wadogo.”
Daktari wa Taifa Stars, Nasoro Matuzya kwa upande wake alisema kuna faida kubwa kufanya mazoezi katika sehemu zenye miinuko.
“Kuna faida kuliko Dar es Salaam ambako hali ya hewa ni joto na hewa ni ndogo. Mbeya City inafanya vizuri kwa sababu ina wachezaji wazuri na inafanya mazoezi katika mazingira ya baridi na miinuko.”
Daktari huyo amewatoa shaka watu wenye wasiwasi kwamba timu hiyo itapata tabu pindi ikicheza sehemu za joto.
“Hakuna tatizo kwani kitaalam siku tatu mpaka tano zinatosha mtu kuzoea hali ya hewa,”aliongeza.
Kauli za Wachezaji
Kipa wa timu hiyo, Mtindi Elly aliyetokea Zanzibar amesema kuwa mwanzo alipata wakati mgumu kwa vile hali ya hewa ni tofauti na ile ya kwao lakini sasa amezoea na matarajio yake ni kufika mbali.Straika, Ayub Lipati kutoka Dar es Salaam alisema: “Mwanzo mazoezi yalikuwa magumu lakini nikajitahidi ili nitimize malengo yangu, kama nitachaguliwa katika kikosi kitakachocheza na Burundi kila mtu atakubali uwezo wangu.”
Straika, Paul Bundala ambaye ni nahodha anayetokea Dar alisema: “Kulikuwa na changamoto ndogondogo kama baadhi ya wachezaji kusumbuliwa na misuli na mafua lakini sasa kila kitu kinakwenda sawa.”
Mji wa Tukuyu
Mji huu unapatikana Kusini mwa Jiji la Mbeya, umezungukwa na zao la migomba pamoja na miti ya asili.
Katika mji huu ni nadra kuonekana kwa jua, hali yake ya hewa ni ya baridi, Kaskazini unapendezeshwa na Mlima Rungwe ambao ni wa tatu kwa urefu nchini baada ya Mlima Kilimanjaro unaoongoza na Meru unaokamata nafasi ya pili.
Credit:Mwanaspoti

No comments: