ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, May 4, 2014

TIMU ZILIZOONGEZWA 2015/2016

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhqD67Iv72_dIKT6USVGV3zP2fcABIXiz_SmQDwVYJ7dtkWHGI4hf-rDqE5J8fvDTVUFtLX4APku3dW5qXciwG0NldPWcguvD-lGyX8OuE8BNKKierWbRw8_3jg_Oa45oHlFPvSUhEEWLDg/s1600/DSC_0172.jpg
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
SAA chache zilizopita, shirikisho la soka Tanzania TFF limetangaza kuwa ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuanzia msimu wa 2015/2016 itakuwa na timu 16 badala ya 14 za sasa.
Afisa habari wa TFF, Boniface Wambura katika taarifa yake kwa vyombo vya habari mchana huu ameseme mabadiliko hayo yamepitishwa na Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Mei 3 mwaka huu) jijini Dar es Salaam baada ya kupokea mapendekezo ya kuongeza idadi ya timu kutoka kwenye Kamati ya Mashindano.
 Taarifa hiyo ilieleza kuwa uamuzi huo umefanywa kwa lengo la kuongeza ushindani katika ligi hiyo, na kuwezesha wachezaji kupata mechi nyingi zaidi za mashindano. Kwa mabadiliko hayo maana yake ni kuwa Ligi ya msimu wa 2015/2016 itakuwa na mechi 240 wakati kwa sasa ina mechi 182.
Baada ya taarifa hiyo, mtandao huu umekuwa ukipokea simu na ujumbe mfupi wa simu kuuliza namna jinsi timu hizo mbili zitavyopatikana.
Ili kujibu swali hilo, mtandao huu kwa kujali wasomaji wake umelazimika kumtafuta kwa mara nyingine Afisa habari wa TFF kupata majibu ya swali hilo.
Wambura ameuambia mtandao huu dakika chache zilizopita kuwa cha kwanza kamati ya utendaji umeridhia kuongezeka kwa timu, lakini kinachofuata ni marekebisho ya kanuni.
“Cha kwanza, timu zimeongezwa katika msimu wa 2015/2016 kutoka 14 kwenda 14, lakini cha pili kinachofuata ni kwamba kanuni zitafanyiwa marekebisho”.
“Kamati imeridhia mapendekezo ya kuongezwa timu, kwahiyo mapendekezo hayo inabidi yaende rasmi kwa ajili ya marekebisho ya kanuni”.
“Marekebisho hayo yataonesha timu zinapandaje na zinashuka vipi”. Amesema Wambura.
Kwa maelezo hayo ya Wambura, wadau wafahamu kuwa mapendekezo yamepitishwa, lakini mpaka sasa haijulikani namna ya kuzipata timu zilizoongezwa mpaka marekebisho ya kanuni yatakapofanyika.
Kwasasa sheria inasema timu tatu kutoka ligi daraja la kwanza zitapanda ligi kuu na timu tatu kutoka ligi kuu zitashuka daraja.
 Kuhusu idadi ya wachezaji wa kigeni kwenye VPL, Kamati ya Utendaji itafanyia uamuzi mapendekezo katika eneo hilo baada ya kwanza kupata maoni ya klabu za VPL na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambazo Mei 11 mwaka huu zitakutana na Rais wa TFF, Jamal Malinzi.
 Mapendekezo ya Kamati ya Mashindano ni kuwa idadi ya wachezaji wa kigeni iendelee kuwa watano kama ilivyo katika kanuni za sasa za VPL.

No comments: