Thursday, May 15, 2014

UEFA-SHERIA MPYA: WACHEZAJI WANAOUMIZA WENZAO KUTOLEWA NJE YA UWANJA KWA MUDA!


COLLINAUEFA imependekeza Sheria mpya ambayo Mchezaji atatolewa nje ya Uwanja kwa muda ikiwa Faulo aliyocheza itamuumiza Mpinzani wake.
Mkuu wa Marefa wa UEFA, Pierluigi Collina, akiongea kwenye Mkutano huko Turin, Italy, amesema mabadiliko hayo yatapelekwa kwa IFAB [International Football Association Board], Chombo pekee chenye Mamlaka ya kubadili Sheria za Soka, mwamzoni mwa Mwaka ujao.
Collina amesema: “Tutapendekeza Sheria hii mpya kwa
IFAB ambapo Mchezaji anaemuumiza mwenzake atatolewa nje ya Uwanja kwa muda hadi yule Mchezaji alieumia anamaliza kutibiwa na kuwa tayari kurudi Uwanjani. Yaani, wote wawili watakuwa nje ya Uwanja pamoja na watarudi tena Uwanjani pamoja. Mtindo wa sasa hautendi haki. Mchezaji anaecheza Faulo anaonywa na anabaki Uwanjani lakini yule aliefanyiwa Faulo na kuumia anatoka nje ya Uwanja na kuiacha Timu yake pungufu Uwanjani. Hili linaisaidia Timu iliyocheza Faulo!”
Collina amefafanua kuwa Sheria hiyo mpya itahusu tu zile Faulo zinazoonekana ‘hatari’ na zinazostahili Kadi ya Njano.
UEFA wanatarajiwa kuwasilisha Mapendekezo yao kwa IFAB ambayo itakutana kati ya Februari na Machi Mwaka 2015.
FAHAMU:
IFAB inaundwa na Vyama vya Soka vya Visiwa vya Uingereza, yaani vile vya England, Wales, Scotland na Ireland, ambao ndio wanachukuliwa kama waanzilishi wa mchezo wa Soka, na Wawakilishi kutoka FIFA.
Mabadiliko yeyote ya Sheria za Soka lazima yapitie IFAB ambako hupitishwa ikiwa tu Kura 6 kati ya 8 zilizopo zitaunga mkono na mgawanyo wa Kura hizo 8 ni moja kwa kila Chama cha Soka cha England, Wales, Scotland na Ireland huku FIFA wakiwa na Kura 4.
Kawaida mabadiliko yeyote ya Sheria huanza kutumika kuanzia Julai Mosi kabla Msimu mpya wa Soka haujaanza.

No comments: