Katibu wa GDSS, Badi Darusi (katikati, aliyeshika rasimu ya pili ya Katiba) akizungumza na waandishi wa habari leo. Mwenyekiti wa GDSS, Amina Mcheka (mwenye mtandio) akisisitiza jambo katika mkutano na wanahabari. Sehemu ya Wanaharakati wa GDSS wakiwa katika mkutano huo.
Mwanaharakati kutoka GDSS, akichangia jambo katika mkutano huo.
Mmoja wa wanaharakati hao akichangia jambo katika mkutano na wanahabari.
Mwanaharakati kutoka GDSS, akichangia jambo katika mkutano huo.
Na Mwandishi Wetu WANAHARAKATI wa ngazi ya jamii na washiriki wa Jukwaa la wazi la Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) linaloratibiwa na TGNP Mtandao wameitaka Serikali kuhakikisha mchakato wa maridhiano kati ya wabunge wa kundi la UKAWA na Tanzania Kwanza unafanyika ili kunusuru mchakato na bunge la katiba. Wanaharakati wa GDSS wametoa kauli hiyo leo walipokuwa wakizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam eneo la Mabibo, baada ya kutoridhishwa na mwenendo mzima wa Bunge la Katiba lililomaliza vikao vyake hivi karibuni kupisha bunge la kawaida. Akisoma tamko hilo, Katibu wa GDSS, Badi Darusi alisema pamoja na ombi hilo wameitaka Serikali
kuhakikisha pia awamu ya pili ya Bunge la Katiba matumizi yapungue ili fedha zielekezwe katika kugharamia masuala ya maendeleo. "Kutokana na bunge maalum kutumia fedha nyingi kinyume na ilivyotarajiwa na kazi walioifanya ipo chini ya matarajio ya watanzania, tunadai awamu ya pili ya Bunge hili matumizi yapungue ili fedha zielekezwe katika kugharamia masuala ya maendeleo," alisema Darusi. Aidha alisema kwa kuwa wananchi walitoa maoni yao na ndio msingi wa chimbuko la madaraka na mamlaka yote ya nchi, GDSS inadai maoni ya wananchi yaliopo katika rasimu ya katiba, yaheshimiwe na kuwa mwongozo wa majadiliano. "...tunataka vitendo vya dharau, ubabe, vijembe, vitisho, matusi, kashfa na ubaguzi wa kijinsia unaokuzwa na kulelewa na kanuni za bunge maalum la katiba, viundiwe kanuni mpya kwa ajili ya kuondoa na kuvikemea vitendo hivyo," alisema. Pamoja na hayo, GDSS imelaani malumbano yasio na tija yenye lengo la kupoteza muda vinavyofanywa na wahusika ili wajumbe wa bunge maalum la Katiba waongezewe siku na posho jambo ambalo si la kizalendo. "...Bunge la katiba limejipa madaraka makubwa yakubadili rasimu ambayo imebeba maoni ya wananchi. Tunadai maoni yaliopo katika rasimu ya katiba ilioandaliwa na tume ya Warioba yaheshimiwe.” "...Kama hayo yote hayakuheshimiwa na kuzingatiwa, tunadai bunge hili la Katiba livunjwe na kuundwa kwa bunge jipya la Katiba litakalobeba uwakilishi wa wananchi wenyewe hasa makundi ya walio pembezoni," alisema Katibu huyo wa GDSS. Akifafanua zaidi alisema kundi hilo la wanaharakati limeshtushwa na namna bunge la Katiba lilivyoendeshwa kwa kile kugubikwa na kasoro mbalimbali jambo ambalo lisipochukuliwa hatua madhubuti kuna uwezekano wa kutopata Katiba au kupata Katiba ambayo haitokani na mapendekezo au maoni ya wananchi walio wengi. Aliongeza kuwa tayari Bunge la Katiba limetumia bilioni 27 kwa siku 67 walizokaa kujadili kanuni za bunge maalum la katiba na sura mbili za rasimu ya katiba, hali ambayo inaonesha dhahiri kuwa limewanyima watanzania fursa ya masuala ya msingi yanayowahusu kutojadiliwa. Hata hivyo alibainisha kuwa hali hiyo imewaweka Watanzania wengi njia panda kwani hadi sasa hawajafanya kazi waliotumwa. *Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment