NILIPATA kuzungumza na dada mmoja ofisini kwetu wikiendi iliyopita ambaye alinieleza namna anavyoteseka katika mapenzi. Ni hapo mada hii ilipozaliwa.
Sitaki kueleza sana juu ya tatizo la msomaji wangu huyu mkazi wa Tabata-Kisukulu, jijini Dar es Salaam lakini kwa juujuu, ni kwamba, yeye ni binti mwenye umri wa miaka 28, ana mtoto mmoja ambaye baba yake alimkana!
Anaishi kwa taabu kwa sababu hana kazi, kila siku amekuwa akianzisha uhusiano na wanaume lakini wamemtumia na kumuacha!
Ni mwanamke mzuri kwa kumtazama, anavutia na anaweza kumshawishi mwanaume yeyote aliye mkamilifu lakini changamoto anazokutana nazo ndiyo hizo.
Ameshalia mpaka machozi yamekauka, mwisho akafikiri huenda amelogwa! Lakini nilizungumza naye akaondoka akitabasamu, badala ya machozi aliyokuja nayo!
Alikuja na mwanaye anayeitwa James (4), mwenye afya nzuri na mchangamfu sana. Sitapenda kutaja jina lake, lakini alichovuna kwangu anajua mwenyewe!
Inawezekana kabisa na wewe upo katika mateso kama ya dada yetu huyo na hujui njia ya kutokea, usijali. Mimi nakuambia futa machozi yako. Inawezekana kabisa, kuna mahali ulikosea katika maisha yako ndiyo maana leo hii mapenzi kwako yamekuwa mateso, lakini hiyo isiwe sababu.
Bado unayo nafasi ya kujipanga na kuanza upya kufurahia mapenzi. Kila kitu kinawezekana rafiki yangu. Lakini lazima tukubali kwamba, wakati mwingine mapenzi ni mateso, ni chanzo cha kuingia kwenye matatizo maishani mwako.
Ndiyo maana Mjasiriamali mmoja alisema, ukikosea kuchagua mke/mume, basi tarajia maisha mabaya siku zote. Hii ndiyo kusema kwamba, mwanzo wa mafanikio bora maishani ni kuwa na mwenzi sahihi.
Unayempenda, anayekupenda na unayefurahia kuwa naye. Wataalamu wa Mambo ya Saikolojia ya Uhusiano na Mapenzi wanakubaliana moja kwa moja na hoja hii. Kwamba wakati mwingine mapenzi yanaweza kuwa chanzo cha mateso katika maisha ya binadamu.
Kauli hii inashibishwa na hoja kwamba, mateso hayo yatasababisha na jinsi wewe mwenyewe utakavyokuwa umeingia na unavyoendesha uhusiano wako.
MATESO KIVIPI?
Wapo ambao wanashangaa hoja hii, wanashangaa kwa sababu tangu wamefahamu mambo ya mapenzi hawajawahi kuwa na uhusiano zaidi ya mpenzi mmoja ambaye pengine hivi sasa wapo katika ndoa yenye watoto kadhaa!
Kwao hili hawakubaliani nalo. Lakini wakati huohuo kuna ambao walianza uhusiano wa kimapenzi kwa matatizo na hivi sasa bado wapo kwenye matatizo katika maisha yao ya kimapenzi.
Kwa ufafanuzi zaidi hebu soma visa vifuatavyo ambayo ni vya watu wawili tofauti, hapana shaka utakuwa na jipya la kujifunza.
Mosi: Hiki kinamhusu Ben, alipokuwa anasoma elimu ya sekondari alitokea kumpenda sana Lucy na kwa bahati nzuri Lucy naye alikuwa akimpenda sana, wakawa katika uhusiano kwa misingi ya upendo na uaminifu.
Wapenzi hawa walikuwa wakipendana sana na wakati wakianzisha uhusiano wao walikuwa kidato cha nne. Mpaka wanamaliza kidato cha sita hawakuwahi kukutana kimwili, baadaye kila mmoja akiwa anasoma chuo chake, walikutana nyumbani kwao Mbeya wakati wa likizo.
Wikiendi moja wakaenda club, hiyo ndiyo ikawa siku yao ya kwanza kufanya mapenzi na wote wawili ilikuwa mara yao ya kwanza kushiriki katika sayari ya wapendao.
Siku zikaenda na walipomaliza chuo na kupata kazi wakaoana, wanaishi kwa furaha na amani, ingawa kuna matatizo madogo madogo ya hapa na pale ambayo huwa wanayamaliza wenyewe.
Hivi sasa Ben ana miaka 38 na Lucy miaka 34 wana watoto wawili katika ndoa yao ya amani na mapenzi ya dhati.
Wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!
GPL
No comments:
Post a Comment