Msemo usemao ‘Wa kwanza atakuwa wa mwisho na wa mwisho atakuwa wa kwanza’ unatosha kuelezea shule maarufu ambazo zimeporomoka kielimu kwa miaka ya hivi karibuni.
Miaka ya nyuma shule za ufundi na za vipaji maalumu zilisifika kwa kutoa elimu bora na wanafunzi wake kufanya vizuri katika mitihani yao lakini leo hii imekuwa kinyume.
Kwa mfano shule kama Ilboru, Mzumbe, Jangwani, Pugu, Uru Seminary, Tabora Boys, Iyunga, Azania, Zanaki, Kilakala, Ifunda Girls, Consolata Seminary, Kifungilo Girls na Tambaza zimefanya vibaya katika Matokeo ya mtihani wa kidato cha sita uliofanyika Mei mwaka 2014.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Shule ya Sekondari ya Tambaza iliyopo Ilala, Dar es Salaam ni ya tatu kati ya shule 10 za mwisho katika matokeo ya mtihani huo.
Historia ya shule hii kuanzia miaka ya 1990 hadi 2000 inaonyesha kwamba Tambaza ilikuwa miongoni mwa shule zilizokuwa ziking’ara kwa kushika nafasi za juu katika matokeo ya mitihani ya kidato cha nne na sita.
Aibu hii imeikuta shule ambayo iko katikati ya Jiji kilomita chache kutoka yalipo makao makuu ya wizara yenye dhamana ya kusimamia elimu nchini pamoja na taasisi zake.
Tambaza ni kati ya shule zilizosifika kielimu katika Jiji la Dar es Salaam hasa miaka 1990. Baada ya hapo, vurugu za wanafunzi zilisababisha kufutwa kwa kidato cha kwanza hadi cha nne na kubakiza kitado cha tano ba sita tu.
Mkuu wa Shule
Mkuu Shule hiyo, Hussein Mavumba anasema taarifa za kufanya vibaya kwenye matokeo hayo ni za kushtusha ambazo hawakuzitarajia.
“Ni mapema sana kusema chochote.Bado siamini na imetuchanganya sana, tunafanya uchunguzi kubaini hasa tatizo ni nini ,” anasema na kuongeza:
“Nitatakaa na walimu wangu na tutafanya uchunguzi wa kisayansi kuchunguza nini kilikosewa hadi kusababisha matokeo haya lakini siyo rahisi kuamini hiki kilichotokea”.
Kwa upande wake, mtangulizi wa Mavumba aliyekuwa mkuu wa shule hiyo kuanzia 2004 mwishoni hadi 2009, Nicolas Buretta anasema utandawazi umechangia wanafunzi kufanya vibaya.
Buretta ambaye sasa ni Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro anasema Tambaza ni shule ya kutwa hivyo wazazi na walezi wanatakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuwasimamia ipasavyo.
“Shule hii ni ya kutwa na mzazi au mlezi anatakiwa kuwa karibu na mwanaye kwani wanaporudi nyumbani unakuta anatumia simu kuchati na rafiki zake hadi usiku wa manane badala ya kusoma na kufanya mazoezi ya nyumbani na mwisho wa siku ndiyo hayo yaliyotokea,” anasema Buretta.
Anaongeza: “Nikiwa mkuu pale nilitengeneza kitu kama mafiga matatu yaani walimu, wazazi na wanafunzi lakini nilisisitiza nidhamu ya hali ya juu kwa kila mmoja kutekeleza majukumu yake na hiyo ndiyo ilikuwa siri ya mafanikio yangu.”
Buretta anasema wanafunzi wa sasa ni tofauti na wa miaka ya nyuma wengi hawataki kutimiza wajibu wao na mzazi asipokuwa makini matokeo ya wanafunzi yataendelea kuporomoka.
“Mzazi, mwanafunzi, mwalimu na Bodi ya shule ambao ndiyo wasimamizi wa shule watimize wajibu wao kila mmoja na wakifanya hivyo Tambaza itarudi sehemu yake kama ilivyokuwa nyuma,” anasema Buretta.
Ilianza kuporomoka 2010
Takwimu zinaonyesha kuwa Tambaza ilianza kuporomoka 2010 na imeendelea hivyo kwa miaka mitatu mfululizo, hadi ilipojikuta katika kundi la shule kumi za mwisho kwenye matokeo ya mwaka huu.
Matokeo ya 2010 ni daraja la I-19, II-66, III-215, IV- 91 na waliofeli walikuwa 89. Kimkoa ilikuwa ya 40 kati ya shule 50 huku kitaifa ilishika nafasi ya 290 kati ya 337.
Mwaka 2011 matokeo yalikuwa daraja la I-15, II-51, III-189, IV-84 na waliofeli walikuwa 88. Kimkoa ilishika nafasi ya 28 kati ya shule 41 na kitaifa ilikuwa ya 282 kati ya shule 334.
Matokeo ya 2012 yanaonyesha kuwa daraja la I-12, II-71, III-235, IV-89 huku waliofeli wakiwa 91.
Kimkoa ilishika nafasi ya 30 kati ya 35 na kitaifa ilishika nafasi ya 270 kati ya shule 326
Mwaka huu 2014 daraja la I-4, II-28 , III-130 , IV-109 , waliofeli walikuwa 44. Kitaifa ilikuwa ya 266 kati ya 328 akimaanisha ilikuwa ya tatu kati ya shule 10 za mwisho.
Hali hii inaonyesha kwamba Tambaza haikufanya vibaya mwaka huu pekee bali ni mwendelezo wa matokeo kushuka tangu mwaka 2010.
Wanafunzi wasikitika
Wanafunzi wa shule hiyo ambao hawakupenda kutajwa majina yao wanasema, ni taarifa zilizowasikitisha na kutokujua hatima yao.
“Shule hii inafundisha masomo ya sayansi lakini walimu wenyewe hawapo na hata vifaa vya maabara hakuna, tatizo hili najua litakuwa limechangia kwa kiasi fulani,”alisema mmoja wa wanafunzi hao na kuongeza:
“Serikali inatakiwa kuangalia na kuchunguza nini tatizo kwani ikiachwa hivi hivi inaweza kuifanya Tambaza ikawa shule itakayoshika mkia 2015 kwani walimu nao kufundisha kwao ni tatizo.”
Kauli za wadau
Meneja Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa Hakielimu, Godfrey Bonaventure anasema ni jambo la kushangaza kwa shule iliyokuwa ikisifika kuwa ya vipaji leo inafanya vibaya.
Shule hiyo kufanya vibaya inawezeka ni masuala ya utawala kutokuwa karibu na wanafunzi na kutokutekeleza majukumu yake ipasavyo hasa suala la nidhamu kwa kila mmoja.
“Nina hakika Tambaza ina walimu wengi lakini je, wanafundisha, maabara iliyokuwapo je, inajitosheleza na vifaa vyake. Ina vitendea kazi na mwisho usimamizi unatekelezeka ipasavyo? Haya ni mambo ambayo nina hakika yanahitaji kupatiwa ufumbuzi,” anasema Bonaventure.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiel Olouch anasema tatizo linaweza kuwa katika vitendea kazi na kushuka kwa morali ya walimu kufundisha.
“Tambaza ina wanafunzi wengi lakini je, walimu wanatosha? Vitendea kazi vipo inahitaji kuangaliwa nini kimeifanya kuporomoka na siyo kuinyooshea tu kidole,” anasema Olouch aliyefundisha shule hiyo miaka ya 1990.
Mkazi wa Jijini Dar es Salaam, Alex Msafiri anasema kinachoitokea Tambaza ni mwendelezo wa shule maarufu kufanya vibaya na serikali inatakiwa kuzitupia macho kwa kutatua changamoto inazozikabili.
“Ukiangalia hata Mzumbe, Ilboru, Kifungilo, Azania, Jangwani, Makongo ni shule ambazo zilikuwa zinawika lakini leo hii zinafanya vibaya, hivyo kunahitajika uchunguzi kubaini tatizo ni nini. Madeni ya walimu nayo yanapaswa kutazamwa kwani inawezekana ni chanzo cha walimu kutotekelea majukumu yao, hivyo kuwaumiza wanafunzi,” anasema Msafiri.
Kwa umaarufu na ukongwe wake, ni dhahiri wapo watu wenye nafasi nzuri katika jamii ambao ni mazao ya Tambaza. Hawa wanaweza kutafutwa na kushirikishwa katika mikakati ya kuepusha shule hii dhid ya aibu kubwa zaidi.
MWANANCHI
1 comment:
Nimepokea taarifa hizi kwa masikitiko makubwa sana. Mimi ni mmojawapo wa "product" ya Shule ya Tambaza miaka ya 1990/91. Tulikuwa hatujui kitu kinachoitwa kufeli au daraja la nne au sifuri!
Nadhani ubinafsi na maisha magumu ya Waalimu vimechangia sana. Siku hizi Waalimu wanaangalia maslahi yao kwanza, hawana morali kama zamani. Watoto wa siku hizi nao ni kizunguzungu!, they don't know wahat they are up to, wapo wapo tu! Kazi ni uzuri, ngono na kuigaiga mambo ambayo kimsingi hayapo!
Serikali nayo imeshindwa kwa kiasi kikubwa kusimamia maswala ya Elimu. Kama hakuna mikakati dhabiti kuinusuru Elimu ya Tanzania, hali itaendelea kuwa mbaya na matokeo yake tunayafahamu. Viongozi wakuu ni mifano potofu kwa watoto wetu wa kizazi kijacho!, we need to change!
It's not going to be better any more! It's going to be worse!
Tanzania tuamke!, tusaidiane kulijenga Taifa la kesho!!!
Post a Comment