ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 21, 2014

Chadema yaridhia Ukawa kuteta na JK

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeridhia kuendeleza mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete kuhusu namna ya kunasua mchakato wa katiba mpya ndani ya Bunge Maalumu la Katiba.

Tamko hilo ni moja ya maazimio yaliyopitishwa na Kamati Kuu (CC) ya Chadema, katika kikao chake kilichofanyika jijini Dar es Salaam Julai 18-19, mwaka huu.

Maazimio hayo yalisomwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.

Mbowe alisema CC imepitisha azimio hilo kwa kuzingatia kuwa Rais Kikwete ndiye msimamizi mkuu wa mchakato huo kwa upande wa serikali, huku Chadema ikiwa ni sehemu ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Alisema azimio lingine lililopitishwa na CC linatamka kwamba, wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaotokana na Chadema kama sehemu ya Ukawa watarudi kwenye vikao vya Bunge hilo endapo tu mamlaka ya Bunge yatafafanuliwa kuwa ni ya kuboresha na siyo kuibomoa au kuifuta misingi mikuu ya rasimu ya katiba mpya.

Mbowe, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Ukawa, alisema misingi hiyo ya rasimu ya katiba ilitokana na maoni ya wananchi na kuandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoteuliwa na Rais kwa ajili hiyo.

Alisema azimio lingine linatamka kwamba, wajumbe hao watarudi bungeni endapo tu baada ya ufafanuzi huo utahusisha marekebisho ya kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, inayohusu mamlaka ya Bunge Maalumu, pamoja na kanuni husika za Bunge hilo.

Azimio lingine linatamka kwamba wajumbe wote wa Chadema katika Bunge Maalumu la Katiba hawatashiriki katika kikao chochote cha Bunge hilo au kamati zake hadi hapo ufafanuzi huo utakapofanyika kwa mujibu wa maazimio ya CC.

Mbowe alisema CC pia imepitisha azimio ikitamka kwamba endapo Bunge hilo litapitisha rasimu ya katiba mpya isiyotokana na maoni ya wananchi kama yalivyoakisiwa kwenye rasimu ya katiba iliyoandaliwa na Tume, Chadema kama sehemu ya Ukawa, itafanya kampeni nchi nzima.

Alisema kampeni hiyo italenga kuwashawishi wananchi kuikataa katiba hiyo katika kura ya maoni ya wananchi.

“…Endapo, kwa sababu yoyote ile, Bunge Maalum litavunjwa kabla ya kupitisha rasimu ya katiba mpya, Chadema kama sehemu ya Ukawa, itafanya mapambano ya kupata katiba mpya ya kidemokrasia kuwa sehemu kuu ya kampeni na operesheni zote za chama kuelekea uchaguzi mkuu ujao na hata baada ya uchaguzi mkuu,” alisema Mbowe akinukuu moja ya azimio la CC.

HALI YA KISIASA NDANI YA CHAMA
Alisema CC imepata taarifa ya kujiuzulu kwa baadhi ya viongozi wa Chadema wa mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora.

Hata hivyo, alisema CC ina taarifa za mipango ya viongozi wengine kuandaliwa kujiuzulu katika mikoa mingine kwa lengo la kutoa taswira potofu kwa umma kwamba Chadema inabomoka au ina mgogoro mkubwa wa kiuongozi.

Alisema hiyo inatokana na kufukuzwa kwa waliokuwa viongozi wa chama na wajumbe wa CC, Zitto Kabwe, Dk. Kitilla Mkumbo na Samson Mwigamba.
Mbowe alisema CC inafahamu kwamba, mipango hiyo inaratibiwa na kugharimiwa na vyombo vya dola pamoja na chama kimoja cha siasa.

Alisema baada ya kutafakari taarifa hizo, CC inapenda kuwaarifu wanachama, wapenzi na wafuasi wake na wananchi kwa jumla kwamba, viongozi wa chama hicho mkoa wa Kigoma waliojiuzulu, wamekuwa kwenye uongozi wa chama katika nafasi hizo kwa muda mrefu na katika kipindi chote hicho wameshindwa kukuza chama katika mkoa.

“Tangu mwaka 1993, chama kimekuwa na mbunge mmoja tu wa kuchaguliwa kati ya wabunge tisa wa kuchaguliwa wa mkoa wa Kigoma. Kwa ulinganisho, chama cha NCCR-Mageuzi kimeongeza idadi ya wabunge wake wa kuchaguliwa kutoka sifuri mwaka 2005 hadi kufikia wanne mwaka 2010,” alisema Mbowe.

Aliongeza: “Chama kimepunguza iddi ya madiwani wake katika halmashauri ya wilaya ya Kigoma Vijijini kutoka madiwani watano mwaka 2005 hadi diwani mmoja mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

“Hii siyo mara ya kwanza kwa mkoa wa Kigoma kukabiliwa na tatizo la vyama vya upinzani kusalitiwa na viongozi wao wa kuchaguliwa kwa kujiunga na CCM au kuwa mawakala wa chama hicho….”

Alisema kuhusu viongozi wa mkoa wa Tabora waliojiuzulu, nao pia wamekuwa katika uongozi wa chama kwa muda mrefu bila kuongeza tija yoyote kwa chama.

Mbowe alisema licha ya chama kutoa vifaa vya kazi kama vile magari kwa mkoa huo kwa muda mrefu, mkoa mzima wa Tabora haujawahi kuwa na mbunge hata mmoja wa kuchaguliwa wa Chadema au wa chama kingine cha upinzani.

Alisema pia mkoa mzima wa Tabora una madiwani saba tu wa kuchaguliwa wa Chadema.

Aliwataka viongozi, wanachama, wapenzi na mshabiki wa Chadema pamoja na wananchi kwa jumla kuwa watulivu katika kipindi hiki cha mapambano makali.

Alisema CC itachukua hatua zote stahiki kuhakikisha kwamba kama, ambavyo wasaliti na mawakala wa CCM wa miaka ya nyuma hawakuathiri kukua na kujiimarisha kwa chama, wasaliti na mawakala wa sasa na watarajiwa hawataweza kufanya hivyo katika kipindi hiki, ambacho kinajiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
CHANZO: NIPASHE

No comments: