· Udahili wote kufanywa na NACTE
· Wasiruhusiwa na kuzingatia utaratibu kutotambuliwa
· Waombaji masomo ya Hesabu na Sayansi kupatiwa mikopo
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) limetangaza 6 Oktoba kuwa ni tarehe ya kuanza kwa mafunzo ya stashahada ya ualimu wa shule za msingi (Ordinary Diploma in Primary Education (ODPE)) katika vyuo teule vya majaribio na Stashahada maalumu ya Ualimu wa Sekondari kwa waliomaliza kidato cha nne (Hisabati na Sayansi) itakaendeshwa katika chuo kikuu cha Dodoma.
Zoezi la uombaji wa mafunzo hayo kwa mwaka 2014/15 lilianza rasmi tarehe 23 June 2014 na litakoma 31 Agosti 2014 na mafunzo yataendeshwa katika vyuo teule vilivyoteuliwa na Baraza (NACTE) ambavyo vitaendesha mafunzo chini ya uangalizi wa karibu wa Baraza hilo, Taasisi ya Elimu na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Dk. Primus Nkwera amesema waombaji wote wanatakiwa kuzingatia utaratibu wa uombaji ambao ni kupitia njia ya mtandao kupitia Mfumo wa Udahili wa Pamoja (Central Admission System - CAS) inayopatikana kwenye tovuti ya CAS inayopatikana www.cas.ac.tz au Barazawww.nacte.go.tz na kwamba Baraza halitomtambua mwombaji yeyote atakayeomba kinyume na utaratibu uliowekwa.
Dk. Nkwera amesema lengo la mafunzo hayo ni kutoa nafasi kwa walimu wa shule za msingi kuongeza uwezo na kujiendeleza kwa masomo ya ngazi ya juu. Kwa muda mrefu walimu wa shule wa shule za msingi wamekuwa hawana namna ya kuongeza na kuboresha taaluma yao kutokana na kutokuwapo kwa kozi ya namna hiyo. Stashahada hiyo haitamuhitaji mwalimu tarajali au yule aliyepo kazini kufanya mafunzo ya kidato cha sita na badala yake anatakiwa kufanya mafunzo ya kuendeleza ualimu wake kwa stashahada hiyo.
“Baraza linapenda kuufahamisha umma na wahitimu wa kidato cha Nne na ngazi ya cheti na stashadaha katika fani mbalimbali kwamba uombaji wa mafunzo ya ngazi ya stashahada ya elimu ya ualimu wa shule za msingi kwa mwaka 2014/15 unakoma tarehe 31 Agosti 2014.”Alisema Dk. Nkwera
Amesema kuwa maombi yatafanywa kwa njia ya mtandao kupitia Mfumo wa Udahili wa Pamoja (Central Admission System) inayopatikana kwenye tovuti ya Baraza www.nacte.go.tz au kwa kujaza fomu maalumu za maombi zinazopatikana katika tovuti ya baraza na kwamba waombaji watakuwa na uwezo wa kuchagua vyuo wanavyovipenda baada ya kulinganisha gharama za mafunzo na huduma za ziada zitolewazo na vyuo husika.
“Ili kudhibiti ubora katika programu hii, Baraza limeweka mfumo wa udahaili wa pamoja ambao ndio pekee utakaotumika katika kudahili wanafunzi kwenye vyuo husika, tunasisitiza kwamba yeyote atakaekwenda kinyume na utaratibu huu Baraza halitomtambua.”Alisisitiza
Dk. Nkwera amewataka waombaji wote pamoja na vyuo kuzingatia taratibu za uombaji na udahili zilizowekwa ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza ikiwemo kutotambuliwa kwa wadahaliwa kwa kuwa vyuo kwa sasa haviruhusiwi kudahili wanafunzi moja kwa moja kwa kuwa jukumu hilo sasa ni la Baraza.
Kuhusu walimu wa masomo ya sayansi, Dk. Nkwera amezungumzia jitihada zinazochukuliwa na serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika kukabiliana na upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi ikiwemo shule za msingi.
Amesema serikali imeamua kuwa waombaji wote waliomaliza kidato cha Nne wenye ufaulu wa daraja la kwanza na la pili na wenye ufaulu wa masomo ya sayansi na walimu wenye cheti cha ualimu daraja la “A” wenye ufaulu wa masomo ya sayansi na ambao wanafundisha masomo hayo watapatiwa mkopo na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.
“Serikali inaguswa sana na changamoto iliyopo ya uhaba wa waalimu wa masomo ya sayansi na ina imani kuwa kwa kuwapatia mikopo waombaji wote wanaokidhi sifa na vigezo ni chachu mojawapo ya kulipatia suluhu tatizo hilo kwa kuwapa motisha wote wanaofaulu na walio tayari kufundisha masomo hayo.”Aliongeza Katibu Mtendaji huyo wa NACTE.
Amesema maelezo ya kina kuhusu sifa za udahili, nafasi za udahili kwa kila chuo pamoja na ada inayotozwa yanaonekana katika mtandao mara mwombaji anapobofya kitufe cha uchaguzi wa chuo.
Waombaji wote wanaweza pia kutumia ofisi za kanda za NACTE zilizofunguliwa hivi karibuni Zanzibar na Arusha (Kwa mikoa Kaskazini), Mbeya (Mikoa ya Kusini), Dodoma (Mikoa ya kanda ya kati) na Mwanza kwa ajili ya mikoa ya kanda ya Ziwa.
Wadau wote walio jirani na mikoa hiyo wanaweza kupata huduma zote pasipo kulazimika kwenda Dar es Salaam. Pia waombaji wote wa programu za shahada wanaoendelea kutuma maombi yao kwa njia ya mtandao wanashauriwa kuwasiliana na ofisi za kanda kwa kupata msaada wa haraka zaidi pale wanapokutana na matatizo ya kiufundi.
Namba za simu na mahali ofisi zilipo vinapatikana kwenye tovuti.
No comments:
Post a Comment