ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, July 9, 2014

UNYAMA WA BOMU ARUSHA


  Bomu latupwa kwenye mgahawa jirani na Ikulu
  Lajeruhi watu wanane,wanne familia moja
  Mmoja akatwa mguu,hali yake mbaya

Mlipuko mwingine wa bomu umejeruhi watu wanane jijini Arusha usiku wa kuamkia jana na mmoja kati yao amelazimika kukatwa mguu katika Hospitali ya Rufaa ya Selian na hali yake ni mbaya.

Tukio la juzi lilitokea siku tano tangu bomu lingine liliporushwa Julai 3, mwaka huu, saa 5 usiku na kuwajeruhi watu wawili; Sheikh Sudi Ally Sudi (37) nyumbani kwake, mtaa wa Majengo Chini wakati akipata daku pamoja na rafiki yake, Muhaji Hussein Kifea (38), ambaye ni mkazi wa Sinza, jijini Dar es Salaam aliyekuwa akitokea Nairobi, Kenya.

Sheikh huyo wa Msikiti wa Qiblatan, uliopo eneo la Kilombero, jijini Arusha na rafiki yake, walijeruhiwa vibaya maeneo ya miguuni na kulazwa Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, lakini sasa wamehamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi.


Akizungumzia tukio la juzi, Mkurugenzi wa Tiba katika hospitali hiyo, Dk Paul Kisanga alithibitisha kuwapokea majeruhi wanane waliofikishwa hospitalini hapo juzi usiku, kuanzia saa 4:30 hadi saa 5.

Alisema majeruhi hao walilipukiwa na bomu hilo wakiwa katika mgahawa wa Kituo cha Vama Indian Traditional, kilichopo kwenye majengo ya Gymkhana, kinachotazamana na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mtaa wa Uzunguni, ambako kuna Ikulu ndogo na nyumba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

Kuhusu hali za majeruhi, Dk. Kisanga alisema wamelazimika kumkata mguu wa kushoto, Deepak Gupta (25), baada ya kuona hali yake inazidi kuwa mbaya.

“Deepak hali yake siyo nzuri, kwa sasa yupo chumba maalumu cha uangalizi wa madaktari, amepoteza mguu wake wa kushoto baada ya kuukata, hali yake ni mbaya,” alisema.

Dk. Kisanga alisema kati ya majeruhi hao, wanne wanatoka familia moja, ambao ni Mahush Gupta (baba), Manisha Gupta (mama) na watoto wao Manci (mtoto wa kike mwenye umri wa miaka14) na Deepak (25) aliyekatwa mguu.

Alisema mtoto mwingine aliyejeruhiwa ni wa kiume aliyejulikana kwa jina la Ritwik Khamdahra (13), ambaye amejeruhiwa mkononi.
Aliwataja wengine kuwa ni Vinod Suresh, Raj Rajin na Prateesh Jarey.

Alisema kazi kubwa, ambayo madaktari wa hospitali hiyo wanayoifanya tangu walipowapokea juzi usiku, kuanzia 4:30 ni kuwapa tiba na kutoa vipande vya vyuma mwilini mwao.

Haikuweza kufahamika mara moja iwapo majeruhi hao wote ni Watanzania au la kwani baadhi yao hawajui hata kuzungumza kwa lugha ya Kiswahili.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, ambaye pia Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC), Liberatus Sabas ni miongoni mwa vigogo wa mkoa waliowatembelea majeruhi hao hospitalini hapo juzi usiku.

Kaimu Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Kati, Solomon Masangwa, naye aliwatembelea majeruhi hao jana asubuhi.

Si RC wala RPC walioweza kuzungumzia tukio hilo kama ambavyo imekuwa kawaida yao pale inapotokea milipuko ya mabomu.

Wakati RC hakuwa akipokea simu yake, RPC alisema tukio hilo litatolewa taarifa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Isaya Mungulu jijini Dar es Salaam.

WAWILI MBARONI
Kufuatia tukio la juzi la mlipuko wa bomu lililotokea katika Mgahawa wa Vama Traditional Indian Cusino, majira ya saa 4 usiku, jirani na viwanja vya Gymkhana, mkoani Arusha, Jeshi la Polisi linawashikilia watu wawili wanaosadikiwa kuhusika na tukio hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Issaya Mngulu alisema baada ya tukio hilo walifanikiwa kuwakamata watu hao, ambao walirusha bomu kupitia mlangoni, ambalo lilijeruhi watu wanane.

“Kufuatia kutokea kwa tukio hilo, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya usalama, tumewakamata watuhumiwa wawili wanaosadikiwa kuhusika moja kwa moja na ulipuaji wa bomu hilo. Uchunguzi zaidi unaendelea ili kuwabaini wengine walioshiriki,” alisema Mngulu.

Alisema kutokana na kukithiri kwa matukio hayo nchini, jeshi hilo linaendelea na upelelezi wa kina ili kuhakikisha wote walioko kwenye mtandao huo wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Mngulu alisema katika matukio mengine ya nyuma, watu 20 wamekamatwa, wakiwamo sita wanaosadikiwa kuhusika na mlipuko wa bomu uliotokea Julai 3, mwaka huu, nyumbani kwa Sheikh Sudi Ally Sudi, mkoani Arusha, huku wengine 14 wakikamatwa Zanzibar.

Alisema mbali na hao, wengine zaidi ya 25 wanatafutwa kwa tuhuma za kuhusika katika matukio yaliyotokea mkoani Arusha na visiwani Zanzibar, ambayo yaliua na kujeruhi watu wasio na hatia.

Aliwataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kuepuka mikusanyiko isiyokuwa ya lazima.

Vile vile, aliwataka watu kuwa makini na mtu au kitu chochote wanachotilia shaka pamoja na kuendelea kutoa taarifa zitakazosaidia kuwabaini na kuwakamata wahalifu.

Wakati huo huo; Jeshi la Polisi nchini limesema kuwa bomu alilosema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwa limetengenezwa nchini China limeshindwa kujua lilifikaje nchini.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: