ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, August 6, 2014

NYEPESI NYEPESI KUTOKA LIGI KUU YA UINGEREZA HIZI HAPA

Tetesi za usajili leo..
By Israel Saria on August 5, 2014


Van Gaal hawataki Nani, Kagawa, Zaha, Chicharito …
*Arsenal wamkaribia Carvalho, ila Vermaelen akataa


Wachezaji wa Manchester United wamejawa shauku wakisubiri hukumu ya Kocha Louis van Gaal aliyekwishadokeza wale anaotaka kuwatupa nje ya Old Trafford.

Majina yanayotajwa kuwa miongoni mwa asiowataka kocha huyo Mdachi ni pamoja na winga Nani, Anderson, kiungo Marouane Fellaini, Mjapani Shinji Kagawa, Javier Hernandez ‘Chicharito’ na hata Wilfried Zaha, kinda lililosajiliwa na Sir Alex Ferguson.

Van Gaal atatumia uzoefu alioupata kwa siku chache za ziara nchini Marekani na pia taarifa za kiitelijensia alizopata kutoka kwa wasaidizi wake jinsi mambo yalivyokuwa yakiendelea kwenye uwanja wa mazoezi uliopo Carrington.
Fellaini alisajiliwa kwa pauni milioni 27 mwaka jana kutoka Everton na sasa wapo tayari kupokea hata pauni milioni 15 ili waondokane naye. Napoli ya Italia wanafikiria kumchukua kwa mkopo.

Kagawa alisajiliwa kutoka Borussia Dortmund ya Ujerumani Juni 2012 kwa pauni milioni 12 na sasa United wanatarajia kupata kati ya milioni 10 au nane kutoka kwa watakaomnunua, ambapo anahusishwa na Dortmund na Atletico Madrid.
Zaha aliyesajiliwa Januari mwaka jana kwa pauni milioni 15 kutoka Crystal Palace na kutolewa kwa mkopo mara mbili anafikiriwa bei yake sasa ni pauni milioni 10, lakini United wanadhani ingekuwa vyema zaidi kumtoa kwa mkopo.

Klabu za Queen Park Rangers (QPR), Crystal Palace, West Ham na Newcastle wanataka kujitosa, hata kama anaweza kuwagharimu pasipo kuwazalishia chochote.

Mreno Nani aliyesajiliwa Julai 2007 kwa pauni milioni 19 kutoka Sporting Lisbon amecheza mechi 146 na kufunga mabao 25. Old Trafford watakuwa tayari kupokea pauni milioni 12 na klabu zinazomtaka ni Juventus, Inter Milan, Valencia na Arsenal.

Anderson alisajiliwa Julai 2007 kutoka Porto kwa kitita kikubwa cha pauni milioni 20 lakini amegeuka garasa, ambapo licha ya United kutafuta mnunuzi imekuwa shida kumpata, na wanasema watachukua hata pauni milioni tano tu. Klabu za Ureno na Brazil zinamtaka.

Chicharito alisajiliwa Julai 2010 kutoka Guadalajara kwa pauni milioni sita, akaja kujulikana kama ‘super sub’ lakini sasa hatakiwi, baada ya kufunga mabao muhimu 37 katika mechi 101. Van Gaal anasema pauni milioni 12 ni haki kwao na klabu za Juventus, Inter Milan, Atletico Madrid, Tottenham na Southampton zimejipanga kumchukua akitupwa.

Ashley Young aliyetarajiwa kuachwa anadaiwa kwamba amemvutia bosi mpya na atawekwa kwenye mikakati yake kwa msimu ujao.

Tetesi nyingine za usajili zinaonesha kwamab Arsenal wanaongoza katika vita ya kumnasa kiungo wa Sporting Lisbon, William Carvalho (22) wakimpa kisogo kiungo wa Real Madrid na Ujerumani, Sami Khedira (27) kutokana na madai yake ya mshahara mkubwa na pia kuumia mara kwa mara.

Liverpool na Tottenham wanapigana vikumbo kwa ajili ya kumnyakua mpachika mabao wa Ivory Coast anayechezea Sansea, Wilfried Bony (25), ambapo Swansea wapo tayari kumwachia kwa dau la pauni milioni 19.

Kiungo wa Manchester City, Jack Rodwell (23) amekamilisha uhamisho wake kujiunga na Sunderland kwa dau la pauni milioni 10, akiingia mkataba wa miaka mitano. Alijiunga City akitoka Everton 2012 kwa pauni milioni 12 lakini amecheza mechi 16 tu na kufunga mabao mawili kutokana na, pamoja na mambo mengine, majeraha.

Nahodha wa Arsenal na beki wao wa kati, Thomas Vermaelen (28) amekataa kukaa na klabu hiyo kufanya mazungumzo ya kuongea mkataba wake, akitaka aachwe aondoke kujiunga na ama Barcelona au Manchester United wanaomtaka kwa pauni milioni 10. Arsene Wenger anasema ataruhusiwa kuondoka wakishapata mbadala wake, lakini pia inaelezwa angependa kumuuza Barca au klabu ya nje ya England, badala ya kuwapa washindani wao kwenye ligi kuu.

Barcelona wamesema wanataka kumsajili mlinzi wa Bayern Munich, Jerome Boateng (25) kwa kitita cha pauni milioni 31 ili kuimarisha timu ambayo baadhi ya wachezaji wake wanaelekea kupitwa na wakati.

No comments: