Walisema maneno aliyoyatoa Rais katika hotuba yake yamejaa busara na hekima ya kuwahakikishia wananchi wanapata Katiba Mpya kwa njia ya amani na utulivy.
Wakizungumza na NIPASHE, baadhi wa wahadhiri wa vyuo vikuu nchini, walisema alichosema Rais Kikwete, ni maneno ya busara na hekima.
Katika hotuba yake ya kila mwezi, Rais Kikwete aliwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, waliojiundia kundi la Ukawa, warudi katika Bunge hilo, watumie mifumo maalumu waliyojiwekea na kanuni walizojitungia wenyewe, kutafuta maridhiano.
Rais alisema yupo tayari kusaidia pale watakapohitaji msaada wake kuhusu suala hilo, ili Watanzania wapate Katiba bora wanayoihitaji.
Wanazuoni hao walisema kitendo cha Ukawa kung'ang'ania kususia vikao vya Bunge la Katiba, haitaleta tija kwa Watanzania, badala yake inaonyesha jinsi gani wasivyo na nia njema na nchi.
Akizungumza kwa njia ya simu, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Benson Bana alisema kauli ya Rais Kikwete, inatakiwa kuheshimiwa na kila mtu kwa sababu ina lengo la kujenga nchi na kuweka umoja.
Alisema kitendo cha kukubali kukutana na kundi hilo ni wazi anaonyesha jinsi gani anavyoendelea kutoa fursa nyingine kwa umoja huo, ingawa Ukawa bado hawajaonyesha moyo wa dhati kutumia vizuri nafasi wanazozipata.
"Kwa maoni yangu Rais ametumia busara, hekima na ukweli katika kile alichosema, hotuba yake ilijaa maridhiano kitu ambacho Watanzania tunaamini ndio kitu pekee kitakachopelekea upatikanaji wa katiba mpya," alisema Dk. Bana.
Hata hivyo, alisema hatua ya viongozi wa Ukawa kumpatia masharti Rais ili wakutane naye, halikubaliki kwa sababu hakuna nchi yoyote duniani kiongozi wake wa nchi akapewa masharti kutoka vyama pinzani.
Mhadhiri mwingine wa chuo hicho, Dk. Kitila Mkumbo, alisema kinachoendelea kuonekana katika mchakato wa kuandika katiba mpya ni wanasiasa kupora jukumu hilo badala ya kuwaachia makundi mbalimbali ya wananchi.
Alisema Rais kikwete, anachokifanya ni kusimamia katika kutafuta muafaka wa kitaifa, hivyo anapaswa kuungwa mkono.
Alisema sababu wanazotoa Ukawa ni dhaifu na haziwezi kujitosheleza na kusababisha wabunge wake kususia vikao.
Alisisitiza kwamba hata rasimu ya Katiba Mpya ambayo imependekeza serikali tatu, haimaanishi wajumbe wasijadili uzuri na ubaya wake.
Kwa upande Dk. Kamugisha alihoji kitendo cha wajumbe wa Ukawa kukimbia mazungumzo ndani ya Bunge, akisema hatua hiyo italeta manufaa kwa nani.
Alisema yeye ni muumini wa majadiliano, hivyo anakubaliana na Rais Kikwete kwa wajumbe hao kurudi bungeni kwa kujadiliana na wenzao wa CCM kwa ajili kupata katiba mpya inayozingatia matakwa ya wananchi.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment