Lindi. Watu wawili wamefariki dunia papohapo na wengine saba kujeruhiwa baada ya gari la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), maalumu kwa ajili ya kubeba askari, kuacha njia na kugonga nyumba mbili za raia katika Kijiji cha Mnolela Manispaa ya Lindi.
Tukio hilo lilitokea saa 11:30 alfajiri katika Barabara ya Mingoyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Renatha Mzinga alisema jana kuwa gari lililosababisha tukio hilo ni la Kikosi 83 cha Jeshi lililokuwa likiendeshwa na Shandili Nandonde.
Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni askari namba MT 10728 Pascal Komba na raia ni Somoe Kamteule, mkazi wa kijiji hicho ambaye alikuwa ndani ya moja kati ya nyumba zilizogongwa.
Aidha, kamanda huyo aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni wanajeshi, Simon Edward, Feruzi Hadji, Omary Makao, Mbaruku Duchi, Simon Masele, dereva Nandonde na askari mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Ndekenya.
Alisema kuwa majeruhi hao walipelekwa katika Hospitali ya Mkoa ya Ligula, Mtwara kwa matibabu. Hata hivyo, chanzo cha ajali hakijafahamika na polisi inaendelea na uchunguzi. Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Robby Kisambo alithibitisha kupokewa kwa majeruhi wa ajali hiyo.
Akizungumza na gazeti hili hospitalini hapo, Dk Kisimbo alisema kuwa majeruhi wote waliopokewa ni wanaume na kwamba hali zao haziridhishi.
Alisema mmoja wa majeruhi hao, amehamishiwa katika Hospitali ya Nyangao, Lindi kwa matibabu zaidi na wengine wataendelea kupatiwa huduma hospitalini hapo.
Taarifa ya JWTZ
Taarifa ya JWTZ kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana ilisema ajali hiyo imetokea wakati wanajeshi walipokuwa katika msafara wa kawaida kwa kutumia magari maalumu ya kubeba askari kutoka Mtwara kwenda Masasi na kusema uchunguzi wa kina kuhusu chanzo cha ajali unafanyika kwa kushirikiana na Polisi.
Mwananchi
1 comment:
Kwa nini ajali ajali kila siku hadi wanajeshi wanakuwa wazembe....ukiuliza tatizo utakuta ni haya mambo ya speed na ulevi. Sijui lini tutajifunza....lini?....lini? Kila mtu anafanya mambo ya ajabu..Viongozi wanalewa na kufanya ajali na kuua raia wasio na hatia hakuna linalofanyika, mkuu wa kikosi cha usalama barabarani anashangaa kuongezeka kwa ajali na vifo badala ya wao kukomesha tatizo anamlalamikia nani? Kikwete, Pinda na huyo makamu wa rais(sijui anafanya kazi gani....kufungua na kufunga semina na warsha?) wanalalamika lakini hakuna solutions.
Post a Comment