Katika mchezo huo ambao Yanga itawakosa Coutinho na Jerry Tegete walioumia, Maximo anataraji kumuanzisha mbrazil mwingine 'Jaja' pamoja na ama Hussein Javu au Said Bahanuzi kwenye safu ya ushambuliaji.
Akizungumzia mchezo huo, Maximo alisema anaiheshimu Azam kwa kuwa ni timu iliyofanya vizuri zaidi msimu uliopita ilipotwaa ubingwa wa Bara bila kupoteza mchezo.
"Ni timu nzuri... ina wafanyakazi, wachezaji na makocha wazuri huku pia ikiwa ni timu ambayo ina miundombinu mizuri," alisema kocha wa zamani wa Taifa Stars Maximo ambaye yupo katika mwezi wake wa tatu wa mkataba wa miaka miwili.
"Lakini kwangu naamini Azam si timu kubwa kama ilivyo Simba au Yanga."
Alisema anaamini mfumo huo wa 4-4-2 ni mzuri kwa mchezo wa kesho kwa kuwa ameiona Azam ikicheza hivyo utamletea mafanikio.
"Kutokana na wapinzani wetu mfumo huu utakuwa sawa na utakuwa na maboresho yake. Naamini tutafanya vizuri."
Kocha huyo alisema anategemea msaada wa mashabiki kwenye mchezo huo kwa kuwa anaamini wana nafasi yao katika timu kufanya vizuri kwenye mechi yoyote.
Alisema kuwa mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi kwa kuwa anakiamini kikosi chake na kitawapa raha.
"Viwango vya wachezaji wangu vimepanda lakini tunawahitaji zaidi mashabiki wetu.
"Wana mchango mkubwa kwetu hivyo waje kwa wingi, waisapoti timu na wataona kitu tofauti kutoka kwa wachezaji."
Maximo alisema pamoja na kuwakosa Tegete na Coutinho, amefarijika na kurejea kwa Hamisi Kiiza ambaye alikuwa kwenye majukumu na timu ya taifa ya Uganda.
Mchezo wa kesho ni ishara ya ufunguzi wa pazia la ligi kuu ya Bara ambayo itaanza wiki ijayo. Yanga imepangwa kuwa mgeni wa Mtibwa Sugar Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Jamhuri.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake