Mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano wa nane wa umoja wa taasis za hali ya hewa kusini mwa Afrika, Mkuu wa Wilaya ya Monduli Mhe. Jowika Kasunga (wan ne kutoka kushoto), Mkurugenzi Mkuu wa TMA ambaye pia ni mjumbe wa Bodi ya MASA na mwenyeji wa mkutano huo Dkt. Agnes Kijazi katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano huo.
Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa niaba ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa mwenyeji wa mkutano wa kila mwaka wa umoja wa taasis za hali ya hewa katika nchi za Kusini mwa Afrika (MASA). Mkutano huo unafanyika mkoani Arusha. Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha mgeni rasmi ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Monduli Mhe. Jowika W. Kasunga alizitaka taasis za hali ya hewa kusini mwa Afrika ikiwemo TMA kushirikiana katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya hali ya hewa. ‘Wote tunakubaliana kwamba umoja ni nguvu, hivyo taasis za hali ya hewa zinapaswa kudumisha umoja na ushirikiano ili kukabiliana na changamoto zinazozikabili huduma za hali ya hewa kusini mwa Afrika’ alisema Mhe. Kasunga.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Malawi na Mwenyekiti wa umoja huo alisema, lengo kuu la mkutano huu ni kujaribu kutatua changamoto za taasis za hali ya hewa kusini mwa Afrika.
Kwa niaba ya TMA, Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi aliwakaribisha wageni wote Arusha na kuwatakia majadiliano yenye mafanikio. Dkt Kijazi alisema ni matarajio yake kwamba mkutano huo utatoa mapendekezo yatakayoweza kuboresha huduma za hali ya hewa katika nchi za kusini mwa bara la Afrika.
MASA ni umoja wa taasis zinazotoa huduma za hali ya hewa kusini mwa Afrika (SADC) wenye lengo la kuboresha huduma za hali ya hewa kwa nchi za ukanda wa kusini mwa Afrika. MASA ni umoja ulioanzishwa kisheria wenye katiba, mpango kazi na Bodi. Wajume wa Bodi ni wakuu wa taasis za hali ya hewa katika nchi za SADC ambapo nchi tano (5) ni wajumbe wa Bodi. Nchi hizo ni Malawi,Zimbabwe,Zambia, Afrika Kusini na Tanzania
IMETOLEWA NA MONICA MUTONI - MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake