ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 18, 2014

Mtuhumiwa wa ugaidi atoa madai mazito mahakamani



Mtuhumiwa wa kesi ya ugaidi mkoani Arusha, Abdallah Maginga, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani humo, kumruhusu kutohudhuria siku za kesi na abaki magereza kutokana na maumivu makali anayopata sehemu za siri alikodai kuminywa na polisi, pamoja na kuingiziwa mti sehemu ya haja kubwa.

Mshtakiwa huyo alitoa ombi hilo jana mbele ya Hakimu aliyesikiliza kesi hiyo, Devota Msofe.

“Mheshimiwa Hakimu naomba mahakama yako inipe ruhusa ya kutohudhuria siku ya kesi, sababu ninapopanda gari napata maumivu makali sana sehemu za siri kunauma, kwa sababu polisi walinitesa kwa kuniingizia mti kwenye haja kubwa na kuminya sehemu zangu za siri,” alisema.

Alidai kuwa mbali na maumivu ya sehemu za siri pia mguu wake uliokatwa hospitalini bado una maumivu makali.


Maginga pia aliiomba Mahakama iagize Magereza wamruhusu akatibiwe hospitalini, kwani alitakiwa kwenda kupata matibabu Septemba 5 mwaka huu lakini amezuiwa hadi sasa.

Akijibu ombi hilo, Hakimu Msofe, alisema suala la kwenda mahakamani ni lazima na mahakama haiwezi kumpa ruhusa hiyo.
Pia alimshauri mshtakiwa huyo kuwa kama ana maelezo mengi amweleze hakimu anayesikiliza kesi yake Mustapher Siyani, ambaye kwa siku hiyo hakuwapo.

“Sikiliza Maginga suala la kuja mahakamani ni lazima na sio hiyari wala majadiliano, ila kuhusu kwenda hospitalini liwasilishe Magereza ndiyo mtaona kwa pamoja mnafanyaje,” alisema hakimu huyo.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, washtakiwa hao wameshtakiwa kwa makosa yaliyo chini ya Sheria ya Kuzuia ugaidi Namba 22 ya Mwaka 2002 na kwamba upelelezi ukishakamilika, Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kuisikiliza na kutoa uamuzi.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya kuua, kujaribu kuua, kusajili na kusafirisha vijana kujiunga na kundi la Al-Shabaab.

Mbali na mashitaka hayo pia wanahusishwa na tukio la mlipuko wa bomu lililotokea katika baa ya Arusha Night Park jijini Arusha na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine 16.

Washtakiwa hao ni Abdallah Athumani, Abdallah Thabiti (yupo wodini Hospitali ya Mount Meru), Ally Hamisi, Abdallah Wambura, Rajabu Hemed, Hassan Saidi, Ally Hamisi, Yasini Sanga, Shaabani Wawa, Swalehe Hamisi, Abdallah Yasini, Abdallah Maginga na Sudi Nasibu Lusuma.

Wengine walioongezwa katika shauri hilo ni Shaban Musa, Athuman Hussein, Mohamed Nuru, Jafari Lema, Abdul Mohamed na Said Michael Temba .
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Inna lillahi wainna illahim rajiun,Allah akakuvuweni salaama kwenye hili na lile,amin thumma amin. Allah ndo atakaye kuliepusheni na shari zao na ndo peke wa kumuomba na peke ndo atakaye kulindeni na kukuteteeni msichoke kumlilia na kushika kamba yake kwake yeye hili ni dogo.

waislamu popote pale mlipo je mnaridhika na hali kama hii na madhilaa ndugu zenu wanayo yapata,kesho mbele ya haki mtakuja kuulizwa je mliwasaidiaje.

tuzingatie ni wazi kabisa sheria hii tumetungiwa sisi waislam kuteswa na kuonewa haitatokea wakristo kudhalilisama hivi hata kama watafanya jinai ya aina gani
jee wasialam tumeridhia.

kila lenye mwanzo lina mwisho wake Allah yupo pamoja na nyinyi.

inasikitisha sana kuona kesi za kubambikiziwa ndugu zetu na za kisanii.Allah atakulipeni na mtawashinda madhaliim.amin thumma amin