ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, September 20, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Hivi karibuni kumekuwa na tuhuma mbalimbali ambazo zimekuwa zikiripotiwa na baadhi ya Vyombo vya Habari na Mitandao ya Kijamii kuhusiana na kunyanyaswa, kutendewa vitendo visivyo vya kiungwana na kuteswa gerezani kwa Watuhumiwa wa Makosa ya Ugaidi kinyume na taratibu za Uendeshaji wa Magereza.

Kufuatia tuhuma hizo, Jeshi la Magereza Tanzania Bara limefanya uchunguzi kwa kufanya mazungumzo na Watuhumiwa wenyewe na wamekanusha tuhuma hizo dhidi ya Jeshi la Magereza. Ukweli ni kuwa taarifa hizo si za kweli na hatuelewi kusudio lao ni nini.

Jeshi la Magereza Tanzania Bara linatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa kuhusiana na Utunzaji wa Wahalifu na haki zao kwa kuzingatia misingi ya Haki za Binadamu. Vitendo vya kunyanyasa au kudhalilisha Wafungwa vinakemewa vikali magerezani na si Sera ya Jeshi la Magereza au Serikali.

Napenda kuufahamisha umma kuwa Mahabusu hao wanaotuhumiwa kwa Makosa ya Ugaidi wapo salama, wana Afya nzuri na hawana tatizo lolote gerezani.


Imetolewa na;

John Casmir Minja,
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza,
20 Septemba, 2014.

No comments: