WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe
Felix Mwagara
WAZIRI wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe amewataka
Wakimbizi wa Kambi ya Nyarugusu kuacha mara moja tabia ya kuwaozesha
watoto wao wenye umri mdogo kwani tabia hiyo inawaletea matatizo makubwa watoto
wao wakati wanapojifungua.
Akizungumza na mamia ya
wakimbizi hao katika Ukumbi wa Mikutano
katika kambi hiyo iliyopo wilayani Kasulu, Mkoa wa Kigoma, Waziri Chikawe
alisema katika maisha yake, yeye ni mpambanaji wa kupinga ndoa za utotoni
ambazo zinawaletea madhara makubwa watoto.
Chikawe alifafanua
kuwa, tabia hiyo inayofanywa na wakimbizi hao dhidi ya watoto wao
inawasababishia watoto hao kupatwa na matatizo makubwa kipindi wanapojifungua
kwani viungo vyao vya uzazi havipo tayari kwa ajili ya kuzaa hivyo aliwataka
familia za wakimbizi hao kuacha tabia hiyo ya kikatili dhidi ya watoto wao na
pia inawakosesha haki zingine za msingi watoto hao.
“Wapeni haki zao watoto
wenu, utamaduni huu sio mzuri wa kuwaozesha watoto wadogo, mnatakiwa kuuacha na
kuulaani kwani mkifanya hivyo mtakuwa mnawaletea matatizo makubwa watoto wenu
hasa wanapojifungua,” alisema Chikawe.
Aidha, Waziri Chikawe
aliwataka wakimbizi katika kambi hiyo kuwa makini na ugonjwa wa Ukimwi kwani
ugonjwa huo unaendelea kuua maelfu ya watu duniani na pia bado hauna dawa, na
kuwataka wakimbizi hao kuacha tabia ya ufuska na endapo watashindwa basi
watumia kondomu kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa huo hatari.
Kwa upande wake, Mwakilishi
Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi (UNHCR), Joyce
Mends-Cole, aliwaonya wakimbizi hao kuacha tabia hiyo ya kuwaoza watoto wao
ambao wapo chini ya miaka 18 kwani kwa kufanya hivyo Wakimbizi hao watashindwa
kupata nafasi ya kwenda nchini Marekani.
“Si mnajua tunawaandaa
kwenda Marekani?, kama mnalijua hilo basi endapo mkimbizi yeyote akimpa mimba
mtoto mdogo basi hataweza kupata nafasi ya kwenda nchini humo, hivyo kuweni
makini ili muweze kwenda nchini Marekani,” alisema Joyce.
Zaidi ya wakimbizi
30,000 wa Kambi ya Nyarugusu wanatarajiwa kuhamishiwa katika nchi ya Marekani
kuanzia mwaka 2015.
Waziri Chikawe ambaye
aliambatana na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wakimbizi nchini, Harrison Mseke
pamoja na maafisa wengine wa wizara yake, amehitimisha ziara yake ya siku mbili
mkoani Kigoma ambapo katika siku hizo alikutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama
ya Mkoa wa Kigoma.
Pia alikitembelea Kituo cha Mpito cha Wakimbizi
(NMC) kilichopo mjini Kigoma na baadaye akamalizia ziara yake katika Wilaya ya
Kasulu mkoani humo kwa kuitembelea Kambi kubwa ya wakimbizi ya Nyarugusu
inayowahifadhi wakimbizi zaidi ya 60,000 ambapo wengi wao wakiwa ni kutoka
nchini Kongo, Burundi na wachache kutoka mataifa mengine.
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake