Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, alisema kwa Wizara ya Afya kukiri kwamba vipimo hivyo huchukuliwa na kupelekwa Nairobi kwa ajili ya uchunguzi zaidi ni fedheha kwa taifa ambalo linajinasibu limepeleka Afrika ya Magharibi timu ya madaktari bingwa watano kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Akiwa Kata ya Mamba Kusini, Wilaya ya Moshi, Mbatia aliwaambia wakazi wa eneo hilo kwamba Serikali bado haijaonyesha nia ya dhati ya kujikinga na maambukizi ya Ebola na wala haijutii gharama kubwa inazotumia kupeleka nje ya nchi sampuli hizo kwa ajili ya vipimo.
“Serikali yetu haina lugha moja kuhusu ugonjwa huu na bado ingali inajifedhehesha kutokana na Muhimbili kukosa mashine ya kuchunguza sampuli za damu zenye virusi vya ugonjwa wa Ebola. Je, nani tumbebeshe mzigo huu?” alihoji.
Pamoja na kuikosoa Serikali, Mbatia alimkabidhi Makamu Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Mashariki la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, Sh. milioni 10 kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa nyumba za walimu wa Shule ya Sekondari ya Stephano Moshi.
Wiki iliyopita, mfanyabiashara mmoja (jina limehifadhiwa) ambaye alitokea nchini Senegal, alizua taharuki kwa wakazi wa mji wa Moshi baada ya kuugua homa kali iliyohusishwa na Ebola na kulazimika kuwekwa karantini katika Zahanati ya Shirimatunda iliyopo mjini hapa.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii jana ilitoa taarifa ikisema kwamba majibu ya vipimo vya mgonjwa aliyewekwa karantini, yamerejea toka Kenya kuwahakikishia wananchi kwamba mfanyabiashara huyo hana Ebola.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment