ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 28, 2014

Wabunge wacharukia mikataba ya gesi asilia

Ni baada ya TPDC kugoma kuiwasilisha
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe

Usiri katika mikataba 26 ya utafiti na uchimbaji wa gesi umezidi kuigubika nchi, baada ya menejimenti ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kukaidi maagizo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na hivyo kuzua mvutano mkubwa kati yake na kamati hiyo kikaoni.

Maagizo hayo ambayo yalitolewa na PAC mwaka jana, yaliitaka menejimenti ya TPDC kuwasilisha taarifa ya mapitio ya mikataba hiyo pamoja na mikataba yenyewe mbele ya kamati hiyo ili ikaguliwe, katika kikao baina yao mwaka huu.

Kikao hicho kilizikutanisha pande mbili hizo jana katika Ofisi Ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuipa PAC fursa ya kukagua mahesabu ya TPDC yaliyoishia Juni 30, mwaka jana.

Hata hivyo, menejimenti ya TPDC ikiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo, Michael Mwanda, ilihudhuria kikao hicho bila ya kuwa na nyaraka hizo muhimu, kinyume cha maagizo ya kamati hiyo.


Hali hiyo ilidhihirika katika kikao hicho baada ya Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe, kuitaka menejimenti hiyo kuwasilisha nyaraka hizo mbele ya kamati yake ili kazi ya kuikagua ianze mara moja.

Hata hivyo, wakati wajumbe wa PAC wakisubiri kwa hamu na shauku kubwa kuona nyaraka hizo zikiwasilishwa, walishangaa kumsikia Mwanda akiieleza kamati hiyo kuwa taratibu zilizopo katika Ofisi ya Spika haziwaruhusu kufanya hivyo moja kwa moja kwa kamati hiyo.

Mwanda alisema TPDC walipewa kazi ya kuipitia upya mikataba hiyo na waziri wa nishati na madini, hivyo baada ya kuikamilisha kazi hiyo waliwasilisha ripoti kwa waziri huyo kama taratibu zinavyotaka.

Alisema hawawajibiki kuwasilisha ripoti wala mikataba hiyo kwenye taasisi nyingine yoyote, kwa madai kwamba, kufanya hivyo itakuwa ni kuwalazimisha wakiuke taratibu.

Hivyo, akasema kama PAC wanahitaji nyaraka hizo, basi wanatakiwa wamwandikie waziri huyo kumuomba awapatie na siyo kuwabana TPDC wafanye hivyo.

Kauli hiyo ilimfanya Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe, kuingilia kati na kumtaka Mwanda aeleze alikozipata hizo taratibu katika Ofisi ya Spika na kanuni gani ya Bunge inayoizua serikali kuwasilisha taarifa kwa kamati ya Bunge inapozihitaji na kujibiwa na Mwanda kuwa taratibu hizo hazipo.

Baada ya jibu hilo, Zitto naye alimuuliza Mwanda akimtaka aeleze kazi iliyofanywa na TPDC kupitia upya mikataba hiyo na fedha walizotumia kufanya kazi hiyo kama zilikuwa ni za umma au la na kujibiwa na Mwanda kuwa vyote hivyo vilikuwa ni vya umma.

Hivyo, Zitto akaieleza menejimenti ya TPDC kuwa kama wanatambua hayo, basi wanapaswa pia watambue kuwa Bunge linayo mamlaka ya kupata taarifa yoyote kutoka serikalini isipokuwa zile tu za kiusalama, ambazo hata hivyo, alisema viongozi wa vyombo vya dola, kama vile Mkuu wa Jeshi la Polisi, wanaweza kumuonyesha mwenyekiti wa kamati kama ikibidi kufanya hivyo.

Baada ya kueleza hayo, Zitto aliendelea kusisitiza kuibana menejimenti ya TPDC iwasilishe mbele ya kamati yake taarifa ya mapitio ya mikataba hiyo, huku Filikunjombe naye akiitaka menejimenti hiyo ieleze kwanini hawakupeleka jana nyaraka hizo wakati kamati ndiyo iliyozihitaji tangu mwaka jana.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, James Andilile, aliingilia kati na kuungana na Mwanda kwa kuieleza PAC kuwa nyaraka zinazohitajiwa na kamati hiyo zipo kwa waziri, ambaye ndiye aliiagiza bodi ya TPDC kufanya kazi ya kuipitia upya mikataba hiyo, ambayo baada ya kuikamilisha walizipeleka kwake.

“Kama kamati wanazihitaji, basi agizo litolewe kwa waziri azilete,” alisema Andilile.

Kauli hiyo ya Andilile ilijibiwa na Zitto, ambaye alisema kuwa wanaowajibika mbele ya kamati ni TPDC na siyo waziri na kwamba, kitendo cha menejimenti ya shirika hilo kutowasilisha nyaraka hizo ni cha dharau kwa kamati na pia ni uvunjaji wa sheria.

“Mnaiona hii. Hii ni taarifa ya Narco (Kampuni ya Ranchi ya Taifa) iliagizwa na Rais na siyo wa waziri iletwe hapa kwa niaba ya public (umma),” alisema Zitto, huku akiionyesha menejimenti ya TPDC kitabu cha taarifa ya Narco.

Hivyo, akasema wanaopaswa kumuandikia waziri barua awape nyaraka hizo kisha waziwasilishe kwenye kamati ni TPDC na siyo kamati.

Pia Filikunjombe aliwauliza menejimenti ya TPDC kwanini hawakwenda mbele ya PAC na waziri wala katibu mkuu wa wizara, swali ambalo halikujibiwa na menejimenti ya TPDC.

Hata hivyo, hilo pia halikufua dafu, kwani mvutano kati ya PAC na menejimenti ya TPDC ulieendelea, baada ya Zitto kuwataka kwa mara nyingine tena wawasilishe nyaraka hizo, huku Mwanda naye akisisitiza kuwa ziko kwa waziri na kwamba, mikataba yote ina utaratibu wake.

Hali hiyo ilimfanya Zitto kumtaka mwakilishi wa katibu wa Bunge katika kikao hicho kueleza sheria inasemaje, ambaye alithibitisha kuwa inalipa Bunge mamlaka ya kuitisha waraka wowote kutoka serikalini isipokuwa tu ule unaohusu masuala ya kiusalama.

Baada ya maelezo hayo ya mwakilishi wa katibu wa Bunge, Zitto alisema pia sheria namba 3, mbali na kulipa Bunge, ambalo lona jukumu la kuisimamia serikali mamlaka hayo, PAC pia inayo adhabu inayoweza kuitoa kwa kuinyima taarifa.

Kutokana na maelezo hayo, Mwanda aliisihi PAC kutofikia hatua ya kuiadhibu menejimenti ya TPDC, kwani kabla ya hapo Zitto alikuwa amekwisha kusema kuwa lengo la kukutana ilikuwa ni kuweka sawa mambo na siyo vinginevyo.

Mvutano huo ulihitimishwa na agizo la PAC, ambalo limeiagiza menejimenti ya TPDC kuhakikisha kwamba, kesho hadi muda wa kazi unapoisha, wahakikishe wawe wamewasilisha kwa katibu wa Bunge taarofa ya mapitio ya mikataba hiyo pamoja na mikataba yenyewe.

Zitto alisema taarifa ya mahesabu hayo ya TPDC inaonyesha kuwa kati ya mikataba 26, mikataba saba tu ndiyo iliyokaguliwa, huku mikataba 19 ikionyesha kuwa bado haijakaguliwa, hivyo akawataka watoe maelezo yote hayo katika siku, ambayo watawapangia kukutana na kamati.

Waziri wa Nishati na Madini, alifanya mkutano na wajumbe wa bodi ya TPDC, Septemba 15 mwaka jana na kuwaagiza kupitia upya mikataba, ambayo tayari ilishaingiwa na kuwakataza kusaini mikataba mipya hadi pale watakapokuwa wametoa ripoti ya mikataba hiyo.


Aliagiza suala hilo ili kuona kama kuna ambayo ilifanyika kinyume cha sheria ili waliohusika wachukuliwa hatua.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: